Makampuni ya kuchapisha vitabu hayakusita kuchapisha kitabu baada
ya ithibati ya kamati kupatikana, kwa sababu hiyo ilikuwa thibitisho
kwamba kitabu hicho kitatumiwa katika shule za serikali na zile zenye
kupata ruzuku ya serikali. Ithibati ilionyesha kwamba kitabu kitapata
wanunuzi, jambo ambalo lilisaidia kupunguza gharama ya kuchapisha
vitabu vya Kiswahili ambavyo havikuwa, na hadi sasa havina, wasomaji
wengi nje ya shule. Waandishi walipata moyo wa kuandika walipojua
kwamba vitabu vyao vitatumiwa kote katika Afrika Mashariki. Vitabu
viliuzwa kwa wingi. Kwa mfano, vitabu vinne vya Ronald Snoxall
viliuzwa takriban nakala 1,000,000. l6*

Nguvu za ithibati hazikuishia Afrika Mashariki tu. Uwezo wa ithibati
wa Kamati ulikuwa ukiheshimiwa kote ulimwenguni, kama asemavyo
Ratcliffe:

"Wachapishaji wa Ulaya, Marekani na sehemu zingine za ulimwengu
wamekuwa wakitegemea ithibati iliyotolewa na kamati ya Kiswahili
ya Afrika Mashariki kwa miswada waliopelekewa na waandishi
binafsi, Waafrika na Wazungu ili kuwasomea na kuwasahihishia."
(Ratcliffe, ILC Bulletin Na 21, 1951: 3).

Ili kuwatia moyo Waafrika waweze kuandika kusudi watosheleze
mahitaji ya vitabu vya fasihi, Kamati ilianzisha mashindano ya kuandika
insha mnamo 1935. Ili kuwapa motisha ya kuendeleza vipawa vilivyo-
gunduliwa katika mashindano ya insha, mashindano ya uandishi yalianzi-
shwa katika mwaka wa 1939. Kutokana na mashindano hayo miswada
mingi ilipelekewa Kamati. Mashindano hayo yalianza kuwashirikisha
washindani Wazungu katika mwaka 1942 ili kukuza uandishi wa Kiswahili
miongoni mwa watawala wa siku za baadaye. (Ratcliffe 1942: 9). Kwa
hivyo, kamati ilikuwa ikitekeleza malengo iliyokusudiwa.

Ilikuwa ikichapisha vitabu vya Kiswahili sanifu ili iwashawishi waandishi
wapya, na ilihakikisha kwamba vitabu vilikuwa vikitafsiriwa kwa
Kiswahili. Kamusi ya Kiswahili-Kiswahili ilichapishwa mnamo 1935 hali
kamusi ya Kiswahili-Kiingereza na ya Kiingereza-Kiswahili zilichapishwa

--
16* Mahojiano ya mwandishi na R. A. Snoxall Februari 10, 1984. Vitabu hivyo ni: Elimu ya
Kiswahili Kitabu cha Kwanza. Kitabu cha Pili na Kitabu cha Tatu vilivyoandikwa na E. G.
Morris na R. A. Snoxall; na Kitabu cha Nne kilichoandikwa na R. A. Snoxall na E. A. Ibreck
vilivyochapishwa na Longman (hadi 1959.)

28

mwaka 1939. Kamati iliendelea kujibu maswali ya umma kuhusu maneno
mapya, asili ya maneno, maneno yaliyoazimwa n.k., na maneno yaliyo-
kubaliwa yalichapishwa katika jarida la l.L.C. Bulletin. Hapo awali
nakala za l.L.C. Bulletin zilikuwa zikitolewa bure kwa wale waliokuwa
wakipenda. Baadhi ya vitabu vya sayansi vilikuwa vimetafsiriwa kwa
Kiswahili. 17* Vitabu hivyo vilikuwa msingi bora ambao ungetumiwa
kuanzisha utafiti wa masomo ya Kiswahili na uchapishaji.

2.2 Othografia

Katika utangulizi wa kitabu kinachoitwa A Handbook of the Swahili
Language, Askofu Steere alijadali suala la tahajia au hati za maandishi ya
Kiswahili, kwa undani. Karibu maandishi yote ya Kiswahili kabla ya
wakati wake yalikuwa yameandikwa kwa hati za Kiarabu. Mengi kati ya
maandishi hayo yalikuwa ni tenzi na mashairi ya kidini na mambo ya
kawaida yaliyoandikwa kwa lahaja ya kishairi ya Kaskazini ambayo
Steere alishuku iwapo ilieleweka na watu wengi. Ingawa Kiswahili cha
wakati wake kilikuwa kikitumiwa katika kuandikiana barua, Steere
anasema kwamba barua kama hizo zilianzia na salamu kwa Kiarabu na
pia maneno na vifungu vya maneno ya Kiarabu vilikuwa vikichanganywa
na Kiswahili.

Steere alitambua kwamba hati za Kiarabu hazifai kuandikia Kiswahili
kwa sababu lugha ya Kiswahili inazo irabu tano ikilinganishwa na irabu
tatu za Kiarabu. Kuhusu konsonati, hati za Kiarabu zinao upungufu wa
konsonanti cha, g, p, na v. Steere aliandika hivi:

"Kwa hivyo, Waswahili wanalazimika kuandika ba, f, au p waki-
kusudia kuandika mb au b; wanaandika ghain badala ya g, ng, ng'; fa
badala ya v, mv na f; ya badala ya ny na y; shin badala ya ch na sh; pia
wanaiwacha n inapozitangulia d, j, y na z." (Steere 1870: 5)

Kwa hivyo, ni wazi kwamba hati za Kiarabu hazifai na hazitoshelezi
maandishi ya Kiswahili kwa sababu ya kutatanisha. Ili kuonyesha
matatizo ya hati hizi, Steere anaandika hivi:

"Nilipokuwa Zanzibar, kulikuwa na barua iliyotoka Kilwa kuhusu
vita. Barua ilitaja kwamba mtu mmoja kati ya wale waliopigana

--
17* Baadhi ya vitabu hivyo ni Mafunzo Katika Hygiene ya Kuwafunza Watu wa Afrika ya
Mashariki, London 1924; Stronomia - Elimu ya Dunia na Jua na Mwezi na Nyota, UMCA
Zanzibar 1901; Jiolojia, UMCA Zanzibar 1901; Lojiki - Mlango wa Filosofia 1, UMCA
Zanzibar 1901 na Mlango wa Filosofia 2, UMCA Zanzibar 1901.

29

alikuwa amekufa au amevuka na hakuna aliyeweza kusema kile
kilichokuwa kimetendeka. Konsonanti mbili za mwisho zilikuwa fa
na gaf zikiwa na vitone vitatu juu yake. Ikiwa vitone viwili vilikuwa
vya herufi ya kwanza, mtu huyo alikuwa amekufa. Ikiwa vitone
viwili vilikuwa vya herufi ya pili alikuwa hai, lakini vitone hivyo
vilikuwa katikati hivi kwamba hakuna aliyeweza kuvigawanya.
Iwapo Kiarabu kingekuwa na herufi v ingekuwa wazi." (Steere
1870: 6).

Zikilinganishwa na hati za Kiarabu, hati za Kirumi hazileti matatizo
yoyote katika kuandika Kiswahili. Sababu yake ni kwamba wasomi wengi
wa Kiswahili waliokuja baada ya Krapf na Steere waliamua kutumia hati
za Kirumi walizokuwa wamezizoea badala ya hati za Kiarabu zilizokuwa
zikitumika kuandika Kiswahili. Maneno na mizani katika Kiarabu mara
nyingi huishia kwa konsonati. Hili pia ni jambo lingine linalozifanya hati
za Kiarabu zisifae kukiandika Kiswahili.

Dhehebu la UMCA lilichapisha vitabu kufuatia mtindo uliotumiwa
katika kuchapisha vitabu vya Steere. Misheni wa Kizungu walifanana na
waanzilishi wa uchunguzi wa Kiswahili kwa kuwa ilikuwa rahisi kwao
kutumia hati za Kirumi badala ya zile za Kiarabu. Mkutano wa Dar es
Salaam wa 1925 uliamua kutozitumia hati za Kiarabu pamoja na
konsonanti za Kiarabu kama vile kh. 18* Uamuzi huu wa l925 uliwakasirisha
wengi wakiwa ni pamoja na gazeti la Mombasa, Al-Islah, kama ilivyo-
jadiliwa kwa kireru katika sehemu ifuatayo.

Profesa Carl Meinhof alipohudhuria mkutano wa Mombasa wa 1928,
waliohudhuria walikuwa na nafasi ya kushauriana naye kuhusu othografia
ya Kiswahili. Meinhof alikubaliana na nyingi kati ya tahajia iliyopendeke-
zwa kwa kuwa ilikuwa rahisi bila kutatanisha, isipokuwa katika herufi ch
na ng'. Meinhof alipendekeza c itumiwe badala ya ch. Badala ya kutumia
alama tatu za maandishi (ng') kusimamia sauti moja, alipendekeza
kutumiwa kwa n yenye mkia itumiwe kama ilivyo katika maandishi ya
kifonetiki.

Lakini mashauri haya ya Meinhof hayakukubaliwa. Wasomi wa
Kiswahili wakati huo walijiona kuwa sahihi, na kwamba mapendekezo ya
Meinhof yalifaa tu katika maandishi ya kifonetiki katika isimu lakini
hayakufaa othografia ya kawaida ya Kiswahili. Katika majadiliano yao

--
18* Baadaye matumizi ya kh yalikubaliwa. Katika makala ya mhariri ya kitabu cha Hemedi
Abdalla - Utenzi wa Vita vya Wadachi Kutamalaki Mrima (uk. 7) Allen anaandika: "Kwa
hivyo ninatumia othograria sanifu ikiwa ni pamoja na kutumiwa kwa herufi kh iliyoidhini-
shwa kutumiwa kwa hiari mnamo 1958".

30

walitaja kwamba ingekuwa vigumu kupiga taipu n hiyo yenye mkia.
Tatizo hili lingetatuliwa hapo mwanzoni kwa kupiga taipu herufi j juu ya n
wakingojea kurekebishwa kwa mashine. Suluhisho hili halikukubaliwa,
na kwa hivyo tatizo la kuandika sauti ya kwanza ya neno ng'ombe kwa
sauti mbili na alama (ng') lingali laendelea.

Upungufu mwingine wa othografia ya Kiswahili unaoweza kutajwa
hapa ni kule kukosa kutofautisha konsonanti za kipua (nazali) ambazo
ni mizani kamili na zile ambazo huambatana na irabu ili ziunde
mizani kamili. (Taz. Mkude 1982). Mifano ya konsonanti za kipua
(nazali) ambazo ni mizani kamili ni m na n za kwanza katika maneno
mmea na nne. Sauti n ya neno nguruwe ni sawa na sauti ya n yenye mkia.
Kwa hivyo, kama tungefuata othografia sanifu kikamilifu badala ya
nguruwe tungeandika ng'guruwe.

Othografia ya Kiswahili sanifu haikukosa malalamiko. Kulikuwa na
upinzani na kutoelewana hata kati ya misheni. Kasisi Roehl katika makala
yake "Hali ya lugha katika Afrika Mashariki" (Africa Vol.3, Na.2, 1930),
anaeleza masikitiko yake kwamba Idara ya Elimu huko Dar-es-Salaam
ilikuwa imeanzisha othografia kinyume cha mapendekezo ya wataalamu
wa isimu wa misheni. Roehl analalamika kwamba, kati ya makosa
mengine, othografia inazipa nafasi za kipekee sauti za Kiarabu na
kulazimisha zitumike babala ya kuwapa wazungumzaji wa Kiswahili
uhuru wa kuzitamka kutegemea vile wanavyotamka sauti za lugha yao na
kuziandika sauti hizo vile wanavyozitamka. Roehl 19* anaeleza kwamba
othografia ya Kiswahili yatakikana iwe ya Kiswahili wala si ya Kiarabu au
ya Kiingereza.

Kasisi Roehl anaeleza zaidi kwamba katika kuunda othografia ambayo
inafaa Kiswahili zaidi, isiwe ni Tanganyika pekee ambayo inatoa uamuzi.
Anapendekeza Kenya, Uganda na Congo (Zaire) zihusike ili kuunda
othografia sanifu kwa watu wote wanaotumia Kiswahili. Kama tunavyojua
sasa upungufu mkubwa uliofanywa na nchi za Afrika Mashariki katika
kusanifisha Kiswahili ulikuwa ni kushindwa kushirikisha Zaire katika
shughuli za Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki kama alivyo-
pendekeza Kasisi Roehl. Upungufu huo, licha ya jitihada za Ronald
Snoxall, unaeleza kuwepo kwa tofauti kadha kati ya Kiswahili cha Zaire
na Kiswahili sanifu.

Kama inavyofahamika na kuelezwa wazi na wasomi kama vile John
Williamson katika uchambuzi wake wa Kingwana cha maandishi (I.L.C.

---
19* Roehl hakutaja sauti za Kiarabu alizokuwa akimaanisha. Yawezekana alimaanisha sauti
kama vile dh katika fedheha dhulumu na adhibu au gh katika ghadhabu gharika na lugha
ambazo hazipatikani kwingine ila katika maneno yaliyoazimwa kutoka Kiarabu.

31

Bulletin Na. 21, 1951: 15-16), lahaja ya Kingwana haifuati upatano
maalum kwa sababu ya kukosa kusanifishwa. Williamson alipata kwamba,
katika makala moja herufi y na j zilitumiwa moja badala ya nyingine. Kwa
hivyo maneno kama vile miji, jina, pamoja na kijana yalitumiwa katika
sehemu moja ya makala, na kwingine katika makala hiyo hiyo maneno
hayo yangeandikwa kama muyi, yina, pamoya na kiyana. Herufi r na l pia
zilitumiwa moja badala ya nyingine. Habari, mara na hubiri yaliweza
kupatikana katika makala moja na habali, mala na hubili. Herufi k na g
zilichanganywa hivi kwamba maneno miziko na mizigo, ukonjwa na
ugonjwa pia yalipatikana katika makala moja.

Kupatikana kwa maneno kama vile muyi, habali, miziko, ukonjwa
katika makala moja na mji, habari, mizigo na ugonjwa katika othografia ya
Kingwana yaonyesha kwamba ni rahisi kusanifisha. Iligunduliwa kwamba
ilikuwa rahisi kusoma na kuelewa maandishi ya Kiswahili sanifu cha
Afrika Mashariki kwa kutujia ujuzi wa Kingwana:

Snoxall 20* anaeleza kwamba alijaribu mara mbili kukifanya Kingwana
kifuate taratibu za Kiswahili sanifu cha Afrika Mashariki. Kwanza
alimtuma C. G. Richards aliyekuwa mkurugenzi wa East African Literature
Bureau kwenda Belgian Congo (Zaire) kuwahimiza wasanifishe Kingwana.
Richards alienda huko lakini hakufanikiwa. Snoxall alitamani kusambaza
Kiswahili sanifu cha Afrika Mashariki ambacho chatumiwa na watu
wengi zaidi. Maoni yake ni kwamba, Kingwana chatumiwa katika sehemu
moja ya nchi moja, na kwa kuwa wanaokizungumza wanafahamu
Kiswahili sanifu, ingekuwa rahisi kuwaleta pamoja na wale wanaotumia
Kiswahili sanifu cha Afrika Mashariki: "Ingekuwa kazi rahisi ikifanywa
kwa bidii". (Snoxall ibid.)

Jaribio la pili alilofanya Snoxall lilikuwa ni kuwaalika Wabelgiji wawili
kutoka Kongo (Zaire) kuhudhuria mkutano wa Kamati ya Kiswahili ya
Afrika Mashariki mjini Nairobi. Wabelgiji hao waliitikia mwaliko lakini
walishangaa kuona kwamba kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki
ilikuwa na wajumbe Waafrika. Wabelgiji hawakufikiria kwamba wajumbe
wa Kiafrika kama vile Shaaban Robert wangeweza kuwa wataalam wa
lugha yao. Kwa hivyo Wabelgiji hawakutaka kujiunga na Kamati ya
Kiswahili ya Afrika Mashariki. Hawakuona kama ingekuwa vizuri
kufanya hivyo.

Ingawaje, Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki, iliweza kuwajulisha
watawala wa Kongo ya Ubelgiji kwamba tofauti kati ya Kingwana na
Kiswahili sanifu ilikuwa ni matamshi yasiyofuata kanuni za safuri. Maoni

--
20* Mahojiano na mwandishi February 10 1984. Hali imebadilika sasa kwa kuwa Kiswahili cha
Zaire kimesanifishwa.

32

hayo ya Kamati yalipelekewa watawala wa Kongo na Bwana Sandrart wa
kutoka Rwanda aliyetumwa na Kongo ya Ubelgiji kuhudhuria mkutano
wa kumi na tatu (13) wa Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki mnamo
1950. Bwana Sandrart aliweza kuifahamisha Kamati mambo kadha
kuhusu Kingwana. Tofauti za kimatamshi hazikutatiza kueleweka kwa
Kiswahili katika kukisanifisha ndiko kulikopendekezwa na Roehl katika
Zaire, Rwanda na Burundi.

Iwapo Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ingefaulu kuwashawishi
watawala wa Kibelgiji kutumia Kiswahili sanifu, hali hiyo ingewezesha
kutumiwa kwa vitabu vya Kiswahili sanifu katika eneo kubwa zaidi.
Kiswahili kingepata matumizi mapya ya kuwaunganisha Wazungu wenye
asili za Uingereza na Ubelgiji mbali na kuwaunganisha Waafrika wa
makabila na mataifa mbalimbali, kwa kuwa kungekuwa na lugha moja ya
mawasiliano katika Afrika Mashariki na Kati. Pia Wakongo wangekuwa
na Kiswahili sanifu. Kushirikishwa kwa Kongo na nchi zingine zinazotumia
Kiswahili katika kukisanifisha ndiko kulikopendekezwa na Roehl katika
makala yake ya 1930.

Canon G. W. Broomfield alijibu makala ya Kasisi Roehl kwa haraka
alipoiandika makala yake "Kukifanya Kiswahili kiwe cha Kibantu"
(Africa Vol.4 Na. 1,1931). Broomfield anaanza kwa kumfahamisha Roehl
kwamba othografia ambayo Roehl anaizungumzia ilifanywa na kamati
mjini Dar es Salaam mwezi Oktoba 1925. Kwa hivyo, anaeleza kwamba
othografia hiyo haikubuniwa na Idara ya Elimu kama alivyodai Roehl.
Anasema kwamba Tanganyika pamoja na Zanzibar zilihudhuria na
kwamba Kenya haikuhudhuria kutokana na kutoelewana hata ingawa
ilikuwa imealikwa.

Anaendelea kueleza kwamba othografia iliyoidhinishwa ni ile ambayo
ilikuwa ikitumiwa kwa miaka mingi na UMCA isipokuwa kutokutumiwa
kwa kh. Maneno ambayo hapo awali yalikuwa yakiandikwa kwa kutumia
konsonanti mbili zikifuatana kama vile hatta, milla na marra ingebidi
yatumie konsonanti moja: hata, mila na mara. Kutumiwa kwa kh katika
maneno kama vile khabari, khatia na khalisi, ilibidi yatumie h pekee:
habari, hatia na halisi.

Katika makala hiyo Broomfield anataja pia kwamba mmishonari
mmoja alipinga othografia hiyo katika mkutano wa Dar es Salaamu wa
1925, lakini wanachama watano waliiunga mkono. Maelezo haya yana-
onyesha kwamba ni watu wachache sana waliohusika katika kuamua
suala la othografia. Yawezekana kwamba kanisa la Roehl, misheni ya
Lutheran, haikualikwa kutoa maoni yao au kuhudhuria mkutano huo
wa 1925.

Kuhusu msamiati wa Kiarabu katika Kiswahili ambao unasababisha

33

kuwepo na konsonanti za Kiarabu katika othografia ya Kiswahili,
Broomfield anaeleza kwamba maneno yenye asili ya Kiarabu ni maneno
ya Kiswahili. Anadai kwamba maneno yenye asili ya Kiarabu ni maneno
ya Kiswahili hivi kwamba Kiswahili hakijawahi kuwepo bila ya maneno ya
Kiarabu na kwamba hakiwezi kuyaondoa. Kwa hivyo hakubaliani na
maoni ya Roehl, ya ukweli kwamba hapo mwanzo Kiswahili kilikuwa
lugha safi ya Kibantu na kwamba maneno ya Kiarabu yaliazimwa. Ukweli
kwamba Kiswahili kilikuwepo kabla ya kuja kwa Waarabu hauwezi
kubishaniwa. Hii ndiyo sababu mhariri wa jarida la Africa alisahihisha
maoni ya kupotosha ya Broomfield katika maoni ya mhariri yaliyotangulia
makala hiyo.

Majadiliano ya othografia yaliendelea wakati wa vita vya pili vya dunia.
Mjadala huo wa wanakamati ulihusu mageuko ya irabu yaliyosababishwa
na mfuatano wa irabu mbili katika neno moja. Mageuko hayo ni kama vile
kuenda na tuataka kuwa kwenda na twataka. Kasisi A. R. Pittway kutoka
Kenya, aliyefanya uchunguzi wake katika lahaja ya Kimvita, aliuanzisha
mjadala katika jarida la Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki Bulletin
Na. 13 la 1939.

Pittway anaeleza kwamba kwa kuwa usanifishaji unahusu lahaja tofauti
kusiwe na lahaja yoyote muhimu itakayopuuzwa. Anasema kwamba
maneno ambayo si ya Kiunguja, semi, na miundo ya kisarufi, yastahili
kukubaliwa kutumiwa sambamba na Kiswahili sanifu ili kutajirisha lugha.
Kwa maoni yake, kukubaliwa kwa matumizi hayo ya kilahaja kutasaidia
kufanya Kiswahili kipendwe sana na watu.

Pittway anaendelea kupendekeza kwamba mw inayotangulia u igeuzwe
kuwa mu. Anaeleza kwamba ni kawaida mu kugeuka kuwa mw inapo-
tangulia a,i,e na o, lakini kifonetiki si jambo la kawaida kwa mu kugeuka
kuwa mw inapotangulia u. Pittway alitaka mabadiliko hayo kwa sababu
dhehebu lake la C.M.S. Iililokuwa limeamua kusanifisha Biblia na Kitabu
cha Maombi lilihitaji muongozo. Alisema kwamba mabadiliko hayo
yalikuwa muhimu kwa sababu matumizi ya mu na mw katika vitabu
vilivyopitishwa na Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki yaelekea
hayakufuata kanuni yoyote.

Kama ilivyotarajiwa, makala ya Pittway iliyoandikwa mara tu baada ya
kuchapishwa kwa kamusi za Kiingereza-Kiswahili na Kiswahili-Kiingereza,
ilipingwa mara moja. Katika jarida, Bulletin Na. 14 la 1948, Ronald
Snoxall anatahadharisha dhidi ya othografia inayokwenda kinyume cha
kamusi sanifu iliyoichukua kamati miaka mingi kutayarisha. Kwa hivyo
pendekezo la Pittway halipaswi kukubaliwa kuvuruga othografia iliyo-
kubaliwa. Snoxall anapendekeza othografia iliyotumika katika kamusi
ikubaliwe vile ilivyo.

34

Maoni mengi kuhusu pendekezo la Pittway yalitolewa na Kasisi Fr.
Alfons Loogman wa Bagamoyo aliyetahadharisha dhidi ya kukubali kanuni
za lugha zibadilishe othografia iliyokubaliwa. Loogman anaeleza kwamba
kusanifishwa kwa Kiswahili kuna maana kwamba lahaja moja ilichaguliwa
kuwa msingi wake na kwamba inabidi lahaja zingine ziwe tayari kupoteza
baadhi ya miundo na kanuni za sarufi zao licha ya umuhimu wa lahaja
hizo. Hata hivyo Loogman anaunga mkono kanuni ya mgeuko wa sauti
uliotajwa na kusema kwamba hakuna mtu angependa kusema yaitu, waivi
au maino badala ya yetu, wevi na meno.

Katika kukomesha mjadala huu, katibu wa kamati Kasisi B. J. Ratcliffe
anakiri kwamba hakuna othografia inayoweza kutosheleza mahitaji yote
ya lahaja zote. Anatoa msimamo rasmi kueleza hivi:

"'M' ya Kiswahili kwa kawaida husimamia 'm', 'u' hutoweka kabla
ya konsonanti, na mara nyingi huwa 'w' inapotangulia irabu ila
wakati inapotangulia kiini cha neno linaloanzia kwa 'u' au kabla ya
'w' au hugeuka kuwa 'w' wakati mwingine iwapo maneno yanahitaji
kugeuka huko." (ibid. uk. 6).

Ni jambo zuri kwamba Kamati ilipinga mabadiliko ya othografia.
Kama watu wangekuwa huru kurekebisha othografia katika siku hizo,
hatungejiepusha na makosa. Tungekumbwa na othografia ya kizamani
kama ile ya Kiingereza ambapo maneno yanaandikwa kwa njia tofauti
sana na vile yanavyotamkwa. Nikitoa mifano miwili tu, neno Leicester
hutamkwa Lesta, na Gloucester hutamkwa Glosta.

2.3 Maoni kuhusu usanifishaji

Kumbukumbu iliyojulikana kwa jina "Kiswahili cha Kisasa", I.L.C.
Bulletin Na. 7 1934, iliandikwa na afisa wa Idara ya Elimu nchini Kenya.
Kumbukumbu hiyo ilipelekewa katibu wa Kamati ya Kiswahili ya Afrika
Mashariki na Mkurugenzi wa Elimu ili ijadiliwe katika mkutano wa
Kamati. Mwandishi ambaye hakutaja jina lake alitahadharisha Kamati
kwamba Kiswahili walichokuwa wakishughulikia kilikuwa kikiendelea
kuwa lugha ngeni kwa Waswahili wenyewe kwa kutengenezewa kanuni
mpya na wageni. Sehemu moja ya kumbukumbu hiyo ilisema hivi:-

"Tumesanifisha Kiswahili, na katika shughuli za kufanya hivyo
yaonekana Kiswahili kimekuwa lugha mpya. Bila shaka sote tunakiri
kwamba kama lugha zingine Kiswahili kitaendelea na kitapanuka

35

katika nyanja za muundo, semi na msamiati kwa kuathiriwa na
ustaarabu wa walowezi. Lakini maendeleo hayo yafaa yatokane na
mawazo ya Waswahili; haifai kuwalazimisha kuyapokea. Lakini
hivyo ndivyo ilivyo; tuko katika harakati za kuwafunza Waswahili
Iugha yao kupitia vitabuni, vingi ambavyo si vya Kiswahili kimuundo
au kimawazo, na ambavyo lugha yake inafanana kidogo sana na
lugha inayozungumzwa. Labda tuna haraka sana kuhepa ukweli
kwamba Waswahili wenyewe wana uwezo wa kurekebisha lugha yao
kufaa mahitaji ya siku hizi na kwamba tayari wanafanya hivyo kwa
haraka ya kustaajabisha. Hivi ndivyo hali ilivyo huko Mombasa na
inaweza kudhihirishwa na wachunguzi wengi. Jambo muhimu sana
ni kwamba jitihada zetu hizi za kupata mwana haramu huyu,
Kiswahili cha Kiingereza, zina matokeo ya kututenganisha na jamii
tunaojaribu kuelimisha. Au tukieleza kwa maneno mengi, tunafikiria
kwa Kiingereza hadi wao wanafikiria kwa Kiswahili na hatuwezi
kuziba pengo hili." (I.L.C. Bulletin Na. 7 1934: 4).

Mwandishi anafikiri kwamba sifa nyingi zisizo na kifani zilitolewa
kuwasifu wachunguzi wakuu wa Kiswahili kama vile Krapf, Steere,
Sacleux, Taylor, Veltten na Beech bila ya kujali kazi zao ambazo
zingetumiwa shuleni. Anafikiri kwamba kamati ilikuwa na haraka sana ya
kuandika vitabu na kutafsiri vingine na kwamba katika kufanya hivyo
wakaguzi wasiokuwa na ujuzi waliajiriwa. Anaendelea kusema kwamba
wale wanaoitetea hii lugha mpya wanasema kwamba ndiyo ya pekee
inayoweza kueleweka na makabila yasiyokuwa ya Waswahili. Anakanusha
wazo hili kwa kusema kwamba ni rahisi kwa Waafrika kujifunza Kiswahili
kuliko Kiswahili hiki kilichochanganywa na muundo wa Kiingereza.

Ili kuthibitisha kwamba Waswahili walipinga mtindo huu mpya wa
Kiswahili na othografia yake, mwandishi wa "Kiswahili cha Kisasa"
aliambatisha makala kutoka gazeti la 'Al-lslah' la Mombasa. Makala hiyo
ilikuwa ya Juni 20, 1932 ambayo mwandishi aliishambulia othografia
mpya ya Kiswhili. Othografia iliyokubaliwa kama tulivyoeleza haikuwa
na baadhi ya herufi kama vile kh inayopatikana tu katika maneno
yaliyoazimwa kutoka kwa Kiarabu. Othografia iliyokubaliwa ingekuwa
na h badala ya kh na hii ni mojawapo ya sababu zilizomfanya mwandishi
wa makala ya Al-lslah alalamike. Makala hiyo inasema hivi:

"Ni madhara makubwa tupatayo kwa Kiswahili hiki kilichoharibiwa
ni Wazungu. Kiswahili ni lugha ya watu wa Pwani, nacho hakiwi safi
ella kitanganyikapo na Kiarabu. Tangu kufika Wazungu, wame-
kigeuza na kukiharibu kwa wapendavyo wao; wamepunguza baadhi

36

ya harufu ambazo ni lazima ziwemo katika baadhi ya maneno, na
pengine hubadilika maana kwa kukosekana harufu hizo. Wameitungia
vitabu vya nahau, na pengine hao watungao vitabu hivyo ni
Wazungu wageni hawajui sana lugha hii, na ambao wavitowa
makosa ni Wazungu wa bara, wasiojuwa Kiswahili. Na wakiambiwa
ni mtu wa Pwani kuwa ni makosa, hawakubali ella kile kile chao ..."
(I.L.C. Bulletin Na. 7, 1934: 8).

Mwandishi wa "Kiswahili cha Kisasa" anaendelea kutilia nguvu mambo
aliyoyataja kwa kusema kwamba baadhi ya vitabu vilivyochapishwa hivi
karibuni vilikuwa tafsiri ya neno kwa neno ya vitabu vya Kiingereza.
Anasema kwamba matumizi ya kanuni za sarufi yalikuwa yakihimishwa
sana jambo ambalo lilifanya vitabu vilivyochapishwa kuwa sahihi kisarufi,
lakini vilikuwa mbali sana na Kiswahili halisi kwa kuwa sarufi peke yake
haiundi lugha. Anataja upungufu mkubwa wa Kiswahili "kipya". Upungu-
fu huo ni, tafsiri ya neno kwa neno, kuzingatia matumizi ya kanuni za
sarufi bila ya kujali methali na semi pamoja na kutojali tabia ya kishairi ya
Kiswahili. Mwishowe anatoa mifano ya sentensi ambazo zina upungufu
kutokana na vitabu vilivyoandikwa kwa Kiswahili sanifu vilivyokuwa
vikitumika shuleni wakati huo.

Katika jarida hilo hilo la Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki,
kufuatia makala hiyo ya "Kiswahili cha Kisasa" kuna jibu lake lililo-
andikwa na Kasisi Canon Broomfield mwandishi wa kitabu kijulikanacho
kama Sarufi ya Kiswahili, ambaye kwa wakati huo alikuwa mhariri
kutoka Zanzibar. Canon Broomfield alikuwa ameombwa na katibu wa
Kamati kumjibu mwandishi wa "Kiswahili cha Kisasa" kwa manufaa ya
wasomaji wa jarida.

Katika jibu lake Canon Broomfield anaonelea kwamba mwandishi wa
"Kiswahili cha Kisasa" ametia chumvi suala la kugeuka kwa Kiswahili
kuwa lugha mpya. Anasema kwamba marekebisho yaliyokuwa yakitokea
yalikuwa hayana budi kuwepo kwa kuwa lahaja moja ndiyo ilichaguliwa
kuwa msingi wa kusanifisha Kiswahili. Kwa hiyo marekebisho yalifanywa
ili kusaidia kutumiwa kwa lahaja hiyo kama lugha ya mawasiliano kote.
Usanifishaji ulihitaji kusomesha Kiswahili hicho ambacho chaonekana
kuwa kipwa. Anaeleza zaidi kwamba Kiswahili sanifu chaonekana kuwa
lugha mpya zaidi katika lahaja zinazotofautiana sana na Kiunguja,
ambacho ndicho msingi wa usanifishaji.

Kuhusu athari za Kiingereza katika Kiswahili, Broomfield anaeleza
kwamba hilo ni jambo lisiloweza kuepukika kwa sababu lugha mbili
zinapotumika katika eneo moja hazina budi kuathiriana na haziwezi
kubaki kuwa safi, pia matokeo ya kuazima huenda yakatajirisha lugha

37

inayoazima. Anatoa mifano ya semi za Kiebrania zilizoingia katika
Kiingereza kupitia tafsiri ya Biblia. Sasa semi hizo zimekuwa Kiingereza.
Anatetea kile kinachoonekana kama tafsiri za neno kwa neno au tafsiri za
semi za Kiingereza kwa kusema kwamba Kiingereza kinaathiri Kiswahili
cha mazungumzo cha Waafrika wanaozijua lugha zote mbili. Anasema
kwamba mabadiliko kama hayo ni ya kawaida kwa kuwa lugha hubadilika
kila mara na kwamba Kiswahili cha wakati huo hakikuwa sawa na
Kiswahili cha wakati wa Krapf. Haoni kama Kiswahili kinaweza kujiepu-
sha na kuazima kwa istilahi za ufundi na teknolojia. Broomfield anaandika
hivi:

"Maendeleo yoyote ya kielimu huhitaji kuwa na mabadiliko na
maendeleo ya lugha itakayotumika kueleza elimu hiyo. Tupende
tusipende, Kiswahili kitabadilika na kuendelea kwa haraka, kwa
sababu hizi. Katika wakati huu kuna maandishi machache sana na
tunaanza kusanifisha lugha hii, pia Waafrika wanaojua kusoma na
kaundika ni wachache sana. Tena Afrika inawasiliana na ustaarabu
wa Uropa; elimu mpya na utaalamu mpya wa kila aina unawafikia
Waafrika. Kiswahili cha miaka ishirini tu iliyopita hakifai siku hizi.
Ni lazima lugha ibadilike na itabadilika, tupende tusipende..."
(Broomfield I.L.C. Bulletin Na 7, 1934: 4).

Njia za kukuza lugha zitakuwa ni pamoja na kuazima maneno kutoka
lugha za kigeni hasa Kiingereza na kuunda maneno mapya. Broomfield
anaonya kwamba lazima watu wajifunze maneno hayo na vile yanavyo-
tumika. Anatoa mfano wa maneno kumi na tisa (19) yaliyoundwa
kutokana na neno vote aliloliazima kutoka kwa Kiingereza, ambayo
anasema, kwamba yanaweza kueleweka vizuri baada ya kujifunza maana
ya neno vote.

Broomfield anasema kwamba mwandishi wa kumbukumbu hakuzi-
shughulikia lahaja tofauti za Kiswahili ambazo zatofautiana kimsamiati,
kimatamshi, sarufi na semi ambazo zaifanya kazi ya wahariri wa Kamati
ya Kiswahili ya Afrika Mashariki kuwa ngumu. Anasema kwamba
wahariri hawatarajiwi kuandika upya miswada wanayopelekewa. Anaeleza
kwamba, Kiunguja kinapotumiwa kama msingi wa usanifishaji jitihada
zinafanywa kuzihusisha lahaja zingine kwa kuwa lahaja zote kubwa
zitakichangia Kiswahili katika siku za baadaye.

Broomfield anakanusha madai ya mwandishi wa kumbukumbu kwamba
kuna chochote katika kazi za Meinhof, Werner, Madan, Torrend,
Domet, Stigand na kadhalika ambacho chaweza kufaa shuleni.

"Yako wapi maandishi hayo; je, twapata chochote kinachoweza
kutumika kama vitabu vya shule vya jiografia, historia, hesabu,

38

afya, elimu ya viumbe, kilimo au uraia? Mbali na uchunguzi wa
kiisimu unaokusudiwa kusomwa na Wazungu, maandishi mengine
mengi, zaidi ni mkusanyiko wa mila, ngano na hadithi. Nyingi kati
ya hizi ni za lugha isiyo na adabu na nyingi hazina umuhimu wowote
wa kielimu." (Broomfield, I.L.C. Bulletin Na. 7, 1934: 19).

Anakiri kwamba uandishi wa vitabu umefanywa kwa haraka na
kwamba baadhi ya vitabu hivyo havikosi upungufu lakini kuchaguliwa
kwa Kiswahili na kule kupenda kwa nchi zote za Afrika Mashariki
kutumia Kiswahili wastani kumesabibisha hali kuwa hivyo. Wale walio-
andika vitabu walifanya hivyo kwa sababu hapo awali hakukuwa na
vitabu kama hivyo na ni juu ya wale wanaotoa lawama kuandika vitabu
bora zaidi.

Mwisho kabisa Broomfield anataja kwamba kusanifisha na kuunganisha
lugha ni kazi ngumu sana na kwamba wale wanaoishughulikia hawata-
pendwa. Makala iliyoandikwa katika gazeti la Al-Islah imeandikwa kwa
Kimvita na wale ambao hawatumii lahaja hiyo hawataisifu kamwe. Pia
Broomfield anasema kwamba, katibu wa Kamati ya Kiswahili ya Afrika
Mashariki alijibu makala ya Al-Islah lakini gazeti hilo halikuichapisha.

Huko kuonekana kwa Kiswahili kuwa ni lugha ngeni kwa sababu ya
kutafsiri wakati wa usanifishaji, kwa maoni yangu, hakungeepukika. Hiyo
ilikuwa deni ambayo ilibidi Kiswahili kilipe kwa maendeleo yake ya
haraka. Kiswahili ambacho hapo awali kilikuwa tu lugha ya biashara,
kilianza kutumika kwa haraka kama lugha ya elimu siyo tu Uswahilini bali
kote katika Afrika Mashariki. Kwa hivyo Kiswahili hakikuwa tena lugha
ya Waswahili tu kama vile mwandishi wa "Kiswahili cha Kisasa"
alivyosema bali kilikuwa lugha ya halaiki kubwa ya watu wa Afrika
Mashariki nzima. Ili kukiwezesha Kiswahili kiumudu wadhifa huo, ilibidi
vitabu vitayarishwe kwa muda mfupi. Siku hizo hakukuwa na Waafrika
wa kutosha ambao wangeweza ama kuandika vitabu vilivyohitajika au
kutafsiri vya Kiingereza kwa Kiswahili.

Maoni kwamba Kiswahili kilikuwa kikichafuliwa kwa kusanifishwa na
kwa kutumiwa kwa kuandikia na kutafsiria vitabu vya shule hayakuwa
Kenya pekee. Nchini Zanzibar, kilikotoka Kiunguja, kulikuwa na hofu
kwamba lahaja ya Kiunguja itachafuliwa na jitihada za usanifishaji.
Akitoa ripoti yake kuhusu vitabu vya shule ya mwaka 1927, Mkaguzi wa
Shule wa Zanzibar, Bwana G. B. Johnson alieleza masikitiko yake
kwamba ni sharti vitabu vinavyotumiwa Zanzibar vikubalike huko
Tanganyika. Alisema kwamba ni sharti vitabu hivyo viwe vya "Kiswahili
kilichorekebishwa kuambatana na maagizo ya Kamati ya Uchapishaji ya
Tanganyika". Ilibidi vitabu vya Zanzibar vikubalike Tanganyika kwa

39

sababu Zanzibar ilikuwa ikihitaji vitabu vichache sana na gharama ya
kuchapisha vitabu vya shule za Zanzibar pekee ilikuwa kubwa.

Zanzibar ilifurahia uamuzi wa kutumiwa kwa Kiunguja kuwa msingi wa
kusanifisha Kiswahili. Lakini kulikuwa na hofu kwamba ingewabidi
Wazanzibari kutumia maneno na miundo kutoka Tanganyika. Jambo hili
liliwakera sana kama inavyodhihirishwa na maneno ya Johnson.

"Yaonekana wazi kwamba hatimaye Zanzibar italazimika kutumia
vitabu vya shule vilivyoandikwa kwa lugha yao iliyochafuliwa. Hili
ni jambo la kusikitisha hata ingawa yaonekana haliepukiki. Hii ni
gharama kubwa ya kulipa dhidi ya usanifishaji wa Kiswahili. Watu
wa Zanzibar wanaojiona kwamba wanakitumia Kiswahili safi
wanachukizwa na kutumiwa kwa Kiswahili cha bara ambacho kwao
wanakiona kwamba ni lugha iliyoharibiwa. Kuhakikisha kwamba
shule zetu zinatumia Kiswahili sanifu kutakuwa kazi ngumu isiyo-
pendeza na itachukua muda kabla matumizi ya bara hayajakuba-
lika." 21*

Kutumiwa kwa Kiswahili kama lugha ya vitabu vya shule kulikuwa ni
matumizi mapya ya lugha hiyo. Lugha ya vitabu vya shule ni tofauti na
lugha ya mazungumzo. Katika Kiswahili, tofauti hiyo ilionekana kuwa
kubwa sana kwa sababu ya maendeleo ya haraka yaliyochukua muda
mfupi na kwa kuwa Waafrika hawakutumiwa kuyatekeleza maendeleo
hayo. Jambo muhimu lililosababisha masikitiko ni kule kutumika shuleni
kwa vitabu vilivyotafsiriwa vibaya vikiwa na ithibati ya Kamati ya
Kiswahili ya Afrika Mashariki. Matumizi ya semi na miundo ya Kiingereza
katika vitabu hivyo vilivyotafsiriwa neno kwa neno hayakukanushwa na
Broomfield kama nilivyotaja. Baadhi ya wanakamati pia waliyapigia
makelele matumizi hayo.

Alipokuwa akiandika kuhusu siku hizo za mwanzo wa usanifishaji wa
Kiswahili, Snoxall anatukumbusha kwamba kulikuwa na vitabu vichache
sana na kwamba kamati ilitegemea sana tafsiri za Kiingereza zilizokuwa
zikitafsiriwa na wanakamati wenyewe. Vitabu vya waandishi kama vile
Rivers-Smith, Mkurugenzi wa Elimu Tanganyika, vilifaa sana. Snoxall
anasema kwamba baadhi ya tafsiri hizo zilikuwa za neno kwa neno na
anashangaa iwapo wanafunzi walizielewa. (Snoxall 1982: 3) 22*.

--
21* Zanzibar Protectorate Administrative Reports for the Year 1927 - Iliyochapishwa 1928.
Sehemu iliyonakiliwa inagusia mkutano wa Mombasa wa 1928.
22* Mfano mmoja ambao Snoxall anaukumbuka sana kutoka kitabu cha Uraia ambacho
kilikuwa tafsiri ya A Manual of Citizenship na Rivers-Smith ni: "Watu wa Taifa hilo
wamekwisha panda kipawa kingine katika ngazi ya ustaarabu". Wanafunzi walitaka kujua ni
nini "Ngazi ya ustaarabu" na ilikuwa wapi?

40

Sura ya Tatu

3.0 Miaka ya mwanzo ya usanifishaji

3.1 Kabla ya vita

Kipindi cha kuanzia 1930 hadi 1938 kilikuwa muhimu sana kwa historia
ya usanifishaji wa Kiswahili.

Katika kipindi hicho, msingi imara sana uliwekwa na kukaanzishwa
kiwango cha juu cha kufanya kazi. Kamati ya Kiswahili ya Afrika
Mashariki ilihitaji msingi imara hivyo ili kuiwezesha kufanya kazi wakati
wa vita. Sifa nyingi za mafanikio ya Kamati zatokana na kazi nyingi na ya
kuchosha iliyofanywa na Frederick Johnson aliyekuwa katibu wa kwanza
wa Kamati hiyo. Mbali na kutafsiri vitabu vingi, Johnson alifanya kazi
nyingi ya kutunga kamusi za Kiswahili-Kiswahili, Kiswahili-Kiingereza na
Kiingereza-Kiswahili.

Nitaanza sehemu hii kwa kujadili hali nzuri ya wakati huo iliyoisadia
kamati kufanikiwa. Hasa sera ya lugha ya nchi za Afrika Mashariki wakati
huo, iliwataka maafisa waliozifanyia kazi nchi hizo, wapite mitihani ya
lazima ya Kiswahili. Kisha tutaijadili kazi yenyewe ambayo Kamati
ilikuwa ikifanya.

Serikali zote za Afrika Mashariki, Kenya, Uganda, Tanganyika na
Zanzibar ziliunga mkono Kamati kwa kuwa zote ziliwakilishwa katika
Kamati. Sera ya lugha za nchi zote zilikisaidia Kiswahili kama tutakavyo-
endelea kufafanua. Wafanyakazi Wazungu wa nchi hizi zote ilibidi
wajifunze Kiswahili na waipite mitihani. Walioshindwa kufauli mitihani
hiyo walibaki kuwa wafanyakazi wa muda wala si wa kudumu. Kwa hivyo
iliwabidi maafisa wa serikali Wazungu wajifunze Kiswahili. lli kupandi-
shwa cheo kazini iliwabidi wapite mitihani ya juu ya Kiswahili. Sera hii
ilikipa Kiswahili hadhi. Mitihani hiyo ya Kiswahili ilisababisha mahitaji
ya kuchapisha vitabu vitakavyowasaidia maafisa hao kujitayarisha kufanya
mitihani hiyo. Pia vitabu hivyo vilinunuliwa kwa wingi kwa kuwa maafisa
hao walitamani kupita mitihani ili wazihifadhi kazi zao. Kwa hivyo
mitihani hiyo ilisaidia kukuza na kueneza Kiswahili pamoja na kuongeza
idadi ya vitabu vilivyochapishwa wakati huo. Sasa tutajadili vile sera ya
lugha ilivyokuwa katika kila nchi. 23*

--
23* Maagizo haya yapatikana katika kitabu cha Ratcliffe na Elphinstone kiitwacho Modern
Swahili 1932: 295-310.

41

Nchini Kenya, kulingana na barua ya Katibu Mkuu namba 40 ya Juni, 1,
1931, mbali na mitihani ya Wazungu waliokuwa wafanyakazi wa Jeshi la
King's African Rifles ambayo ilikuwa na maagizo yake tofauti, maafisa
wengine wote Wazungu waliokuwa wakifanya kazi katika Koloni iliwabidi
wafanye mitihani ifuatayo ambayo ilikuwa ya lazima.

Mtihani uliotangulia ulikuwa, mtihani wa kwanza wa mahojiano kwa
Kiswahili ambao ilibidi ufanywe kabla ya mwaka mmoja kwisha tangu
kuajiriwa kwa kazi isiyokuwa ya kibarua. Iwapo afisa aliyehusika
hangepita mtihani huo ilimaanisha kwamba hangepata nyongeza ya
mshahara ya kila mwaka na pia ingesababisha kushushwa cheo na kuwa
mfanyakazi wa kibarua. Kiwango cha Kiswahili kilichohitajika ni cha
kumwezesha afisa huyo kufanya kazi kwa kutumia Kiswahili pasipo
mahitaji ya mkalimani.

Mtihani wa pili ulikuwa wa Kiswahili sanifu kiwango cha chini. Mtihani
huu ulitahiniwa baada ya mwaka mmoja kwisha na kabla ya miaka miwili
na nusu kwisha tangu afisa aajiriwe. Wale ambao hawakupita mtihani huo
walichukuliwa hatua sawa na wale ambao hawakupita mtihani wa
kwanza. Ili mtu aweze kupita mtihani huo ilibidi awe amefikia kiwango
cha kuelewa na kuzungumza Kiswahili kwa ufasaha na ujasiri.

Mtihani wa Kiswahili sanifu kiwango cha juu ndio uliokuwa wa tatu na
wa juu sana kati ya hiyo mitihani ya lazima. Mtihani huo ulikuwa wa
mahojiano pamoja na wa kuandika. Ulikuwa wa Wazungu wenye vyeo
vikubwa na ulifanywa baada ya miaka mitatu na kabla miaka kumi
haijakwisha tangu waajiriwe. Kukosa kupita mtihani huo kwa muda
uliowekwa kuliathiri cheo cha afisa aliyehusika na kumaanisha kwamba
hangeendelea kupewa nyongeza za mshahara. Ili mtu aweze kupita
mtihani huo ilibidi aijue vizuri sarufi ya Kiswahili na aweze kuzungumza
Kiswahili kwa ufasaha.

Maagizo yaliyoihusu Uganda yapatikana katika tangazo la barua
namba 40 ya Disemba 29, 1928 kutoka afisini mwa Katibu Mkuu.
Maagizo hayo ni sawa na ya Kenya isipokuwa kwamba kuna tofauti
chache nitakazoeleza. Kuhusu mtihani wa kiwango cha kwanza wa
mahojiano, maafisa waliokuwa wakifanya kazi Buganda, waliruhusiwa
kufanya mtihani wa Kiluganda kwa kiwango hicho, lakini maafisa
waliokuwa wakifanya kazi katika sehemu zingine za Uganda ilibidi
wafanye mtihani wa Kiswahili.

Maafisa waliokuwa wakifanya kazi katika tawala za mikoa na wa Idara
ya Elimu ilibidi wapite mtihani wa Kiswahili sanifu, kiwango cha chini
kabla hawajathibitishwa kazini. Maafisa wengine wote wangethibitishwa
kabla hawajapita mtihani huo, lakini baada ya kufanya kazi kwa muda wa
miaka minne hawangepata tena nyongeza ya mshahara mpaka kwanza

42

wapite mtihani huo.

Mtihani wa Kiswahili sanifu, kiwango cha juu nchini Uganda ulikuwa
ukifanywa na maafisa wa tawala za mikoa, na idara za elimu, kilimo,
mifugo, misitu na polisi. Maafisa wote wa idara hizi ilibidi wapite mtihani
huo, la sivyo, mshahara wao haungezidi pauni 720. Nchini Uganda,
maafisa wa serikali wangefanya mitihani ya kiwango cha chini na cha juu
ya lugaha zingine za Uganda badala ya Kiswahili.

Nchini Zanzibar, dondoo kutoka maagizo ya serikali ya Zanzibar
yanaeleza kwamba ni lazima maafisa wote wa Kizungu wapite mtihani wa
Kiswahili sanifu, kiwango cha chini kabla mwaka mmoja haujakwisha
tangu waingie nchini. Wale ambao hawangepita mtihani huo ama
hawangeendelea kuwa waajiriwa wa kudumu au hawangepata nyongeza
ya mshahara ya kila mwaka. Wauguzi ambao hawangepita mtihani huo,
ingebidi wasimamishwe kazi.

Wale waliokuwa wakifanya mtihani wa Kiswahili sanifu kiwango cha
juu walikuwa maafisa Wazungu ambao walikuwa wafanyakazi wa
kudumu. Baada ya kupita mtihani huo walipewa kiinua mgongo cha pauni
hamsini (50). Mbali ya huu mtihani wa Kiswahili kiwango cha juu
maafisa Wazungu wa Zanzibar walikuwa huru kufanya mtihani wa
Kiarabu au Kigujerati wa kiwango hicho. Watahiniwa wa mtihani wa
kiwango cha juu wa Kiswahili, Kiarabu au Kigujerati ilibidi waweke
amana ya rupia arobaini na tano (45), pesa ambazo wangerudishwa
wapitapo mtihani.

Maagizo yaliyoihusu Tanganyika yapatikana katika 'Maagizo kwa
watu wote kutoka Afisi ya Katibu Mkuu, Dar es Salaam, Juni 15, 1931'.
Kulingana na Maagizo hayo ilibidi maafisa wa Kizungu wapite mtihani wa
Kiswahili sanifu, kiwango cha chini kabla mwaka mmoja haujakwisha
tangu waajiriwe nchini. Wale ambao hawangepita mtihani huo hawa-
ngeendelea kuwa waajiriwa wa kudumu.

Mtihani wa Kiswahili sanifu, kiwango cha juu ulikuwa ukitahini ujuzi
kamili wa Kiswahili, sarufi na muundo wa lugha kwa jumla. Watahiniwa
waliofaulu walitakikana waweze kueleza maagizo, sheria na kanuni za
serikali vizuri kwa Kiswahili. Pia walitakikana waweze kutafsiri kwa
ufasaha maandishi ya Kiswahili kwa Kiingereza na ya Kiingereza kwa
Kiswahili.

Maagizo haya yote yaonyesha wazi kwamba sera ya lugha katika Afrika
Mashariki wakati wa ukoloni ilikiunga Kiswahili mkono hasa wakati huo
wa siku za mwanzo za Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki. Sera hiyo
ilikusudiwa kuwawezesha Wazungu kuwaelewa Waafrika wanapofanya
kazi zao. Sera hii iliwaridhisha wanakamati ambao walijivunia kazi zao
kwa kuona kwamba zilitambuliwa na serikali. Juhudi za Kamati ya

43

Kiswahili ya Afrika Mashariki hazikuzinufaisha shule tu, bali ziliwafaidi
maafisa wa Kizungu ambao ilibidi wajitayarishe kufanya mitihani hiyo ya
lazima. Ufafanuzi huu unatusaidia kuelewa ni sababu gani iliyowafanya
wanakamati wawe na moyo thabiti wa kufanya kazi nyingi ngumu ya
kusanifisha Kiswahili kwa kujitolea.

Sasa tutaigeukia "warsha" ili tuone machache kati ya mambo muhimu
yaliyokuwa yakifanywa na Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki
kabla ya vita vya pili vya dunia.

Kwa kifupi kazi nyingi na ngumu ilifanywa na maafisa wa serikali na
misheni kutoka Kenya, Uganda, Tanganyika na Zanzibar waliojitolea
kusanifisha Kiswahili. Hawakuwa na vitabu vya kutosha vya Kiswahili
ambavyo wangetegemea kuwasaidia katika kazi zao. Mjadala mfupi
unaofuata watokana na Jarida la Kamati - ILC Bulletin Na. 1 ya 1930.
Waonyesha baadhi ya matatizo yaliyoikumba Kamati.

Kabla ya kufikia uamuzi kuhusu msamiati sanifu, orodha za maneno
zilipelekewa wahariri wa Kamati pamoja na kuchapishwa kwenye Jarida
la ILC Bulletin ili kuwapa wahariri pamoja na raia nafasi ya kuyajadili.
Maoni na mapendekezo tofauti yalijadiliwa na Kamati kabla orodha
iliyokubaliwa haijachapishwa kama msamiati sanifu. Maoni na mapende-
kezo yaliyotolewa na wahariri kabla uamuzi haujafikiwa yalitofautiana
sana kama inavyodhihirishwa hapa chini.

Kasisi B. J. Ratcliffe, mhariri wa Kenya, anapendekeza kwamba 'irabu' na
'herufi' zitumiwe badala ya kuazima 'vokali' na 'konsonanti' kutoka Kiingere-
za. 'Herufi' ilipendekezwa badala ya 'harufu' ambalo lilikuwa likitumiwa
kwa wingi na Waswahili wa Mombasa ili kulitofautisha na neno harufu la
kawaida.

Naye katibu wa Kamati, Frederick Johnson anashuku iwapo neno irabu
latumiwa na watu wengi au latumiwa na Waswahili wachache wanaoandika
kwa kutumia hati za Kiarabu. Kwa maoni ya Johnson neno herufi au
harufu lilimaanisha hati yoyote ya maandishi iwe vokali au konsonanti.
Kisha anafikia uamuzi kwamba neno lenye kumaanisha konsonanti
lilikuwa lahitajika. Hivyo ndivyo neno konsonanti lilivyoazimwa.

Mengi kati ya maneno tunayoyaona kuwa ya kawaida siku hizi, ilibidi
yatolewe uamuzi. Mfano mmoja ni neno shule. Kasisi A. B. Hellier,
mhariri wa Tanganyika alipendekeza neno shule lililoazimwa kutoka
Kijerumani badala ya neno skuli lililoazimwa kutoka lugha ya Kiingereza.
Naye Canon Broomfield alikuwa na maoni kwamba maneno yote mawili
yangetumiwa kumaanisha vituo tofauti vya elimu. Broomfield aliyekuwa
mhariri wa Zanzibar alipendekeza neno skuli litumiwe kumaanisha vituo
na vyuo vya kufunzia walimu nalo neno shule limaanishe shule za vijijini
tu.

44

Maoni yalitofautiana sana hivi kwamba inashangaza iliwezekanaje
kamati ikaweza kutimiza mambo mengi hivyo. Tukitazama mifano ya
maneno lindi na kina, twaona kwamba wahariri wote wanne walikuwa na
maoni tofauti.

Bwana Morris, mhariri wa Uganda alipendekeza kwamba neno lindi
litumiwe badala ya kina. Kasisi Ratcliffe wa Kenya alisema kwamba neno
sahihi ingekuwa kwina wala si kina. Canon Broomfield kutoka Zanzibar
alisema kwamba neno kimo lilitumiwa kumaanisha urefu wa kwenda juu
na wa kwenda chini, na kwamba neno kina lilikuwa halijulikani Zanzibar.
Naye Kasisi Hellier alijaribu kutoa suluhisho kwa kusema kwamba
"tukitumia kimo kumaanisha kwenda juu na kina kumaanisha kwenda
chini tutakuwa tumepiga hatua mbele" (ILC Bulletin Na. 1 1930: 5).

Baada ya kusoma aya za hapo juu mtu anaweza kushawishiwa kushuku
ujuzi wa kamati na wahariri wake. Maoni kama hayo yangekuwa ya
haraka na yasiyo ya kweli kwa sababu watu hao walikuwa wakishughulikia
karibu kila kitu, kuanzia maneno ya kawaida ya kila siku ambayo
yalihitajika hadi sarufi ya Kiswahili. Wewe unayesoma kitabu hiki, jihisi u
mmoja kati ya wanakamati, naye Kasisi A. B. Hillier anakufahamisha
kama alivyoifahamisha Kamati kwamba:

"Sarafu za senti hamsini, senti kumi, na senti tano kwa sasa hazina
majina. Ni muhimu zipewe majina ya kutumiwa shuleni na ya
kutumiwa na umma." (ILC Bulletin Na. 1, 1930: 10).

Je, kama mwanakamati ungetoa mapendekezo gani, hasa unapojua
kwamba baadhi ya wasemaji wa Kiswahili walikuwa wakitumia maneno
mengi kama vile "peni la senti kumi" na "peni la senti tano"? Maneno nusu
shilingi kumaanisha senti hamsini, peni kumaanisha senti kumi na nusu
peni kumaanisha senti tano yalikuwa ni afadhali kuliko deka na pente
kutoka Kigiriki na ashara na hamsa kutoka Kiarabu ambayo yalipendeke-
zwa kumaanisha senti kumi na senti tano.

Maelezo ya hapo juu yanaonyesha baadhi ya shida zilizowakumba
wasanifishaji wa Kiswahili mapema katika shughuli za usanifishaji.
Kufanikiwa kwao kulitokana na jitihada za pamoja za misheni wa
madhehebu mbalimbali pamoja na msaada na ushirikiano wa serikali za
kikoloni za Kenya, Uganda, Tanganyika na Zanzibar.

Mashauriano mengine mengi kama hayo yaliyojadiliwa hapo juu
yalifanywa na matokeo yake yalikuwa ni kusanifishwa kwa maneno mengi
ya Kiswahili. Kamati ilitoa orodha za maneno ya Kiswahili, ikayajadili,
kisha ikachapisha yale yaliyokubaliwa kama Kiswahili sanifu. Katika
jarida la ILC Bulletin Na. 9 la Oktoba 1935, Kamati inajadili orodha ya
maneno ya Kiswahili yenye asili ya Kibantu na kutoa maelezo ya chanzo

45

chake. Orodha hiyo inayo maneno kama vile kanzu, shamba na kizibao.
Katika Jarida hilo Johnson pia anajadili chanzo cha baadhi ya maneno
naye Kasisi Hellier anayo orodha ya msamiati anaoupendekeza wa vipimo
na mizani.

Katika Jarida la mwaka uliofuata, I.L.C. Bulletin Na. 10 ya 1936
kumbukumbu tatu za J. W. T. Allen, Broomfield na F. Johnson
zimechapishwa. Kumbukumbu hizo ni maoni ya Kamati kumjibu Clement
M. Doke aliyetoa mapendekezo kuhusu jinsi ya kugawanya maneno
katika kitabu cha Bantu Linguistic Terminology. Mapendekezo ya Doke
yangesababisha kuwe na maandishi ya maneno kama vile waSwahili,
muIngereza, mUngu, waDaudi na kwamtu badala ya Waswahili, Mwi-
ngereza, Mungu, wa Daudi na kwa mtu. Kamati ilikataa mapendekezo ya
Doke katika makala hayo na mengine yaliyochapishwa katika jarida
la 1937.

Masuala ya kisarufi pia yalijadiliwa na kuchapishwa katika jarida la
Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki. Kwa mfano matumizi ya KA
na KI yalijadiliwa na A. B. Hellier katika jarida la 1931 naye F. Johnson
alijadili kinyume cha kiambishi "kuto-" katika jarida la 1933. Katika
makala yake, Johnson anatoa rai kwamba neno kutoenda latokana na
maneno kutoa na kwenda. Naye mwanakamati Ronald Snoxall anapinga
maelezo ya Johnson na kumsahihisha kwa kueleza kwamba to katika neno
kutoenda ndicho kiungo cha kinyume.

Masuala mengine kuhusu kusanifishwa kwa Kiswahili yalishughulikiwa
na Kamati pia, na matokeo yake yakachapishwa kwenye jarida. Masuala
hayo yalikuwa ni pamoja na kutoa sababu za kutumiwa kwa irabu
zikifuatana kulikoelezwa na Broomfield mnamo 1931; kuhesabu katika
Kiswahili na A. B. Hellier 1932; alfabeti za Kiswahili na A. B. Hellier
1934; mjadala kuhusu alama za kuwakifisha; pamoja na kukadiriwa kwa
vitabu vya shule vya wakati huo, kulikofanywa na Kamati ya Kiswahili ya
Afrika Mashariki.

Mnamo mwaka 1934 ilibidi Kamati ipime kazi yake. Jambo hili
lilisababishwa na kumbukumbu "Kiswahili cha Kisasa" iliyoandikwa na
afisa mmoja wa Idara ya Elimu, Kenya. Baada ya kuipokea kumbukumbu
hiyo, katibu alimuomba Broomfield aijibu. Kumbukumbu hiyo, majibu
yake, pamoja na dondoo la gazeti Al-Islah la Mombasa zilizochapishwa
katika Jarida, ILC Bulletin la 1934 tayari zimejadiliwa katika sura ya pili.

Baadhi ya makala zilirudiwa katika matoleo ya Jarida ya hapo mwanzo.
Kwa mfano, makala ya Snoxall kuhusu kitendo kutoa, ilichapishwa
katika Jarida namba 6 la 1933 na kurudiwa tena katika Jarida namba 8
la 1935.

Makala iliyojadilia suala la a mbili katika maandishi ya Kiswahili katika

46

Jarida namba 2 la 1931, ilichapishwa tena katika jarida Bulletin namba 6,
la 1933. Kuna sababu mbili za kuchapisha upya makala hayo. Sababu ya
kwanza ni kuwa ILC Bulletin lilikuwa jarida changa lililokuwa likitoa
nakala chache, na lilikuwa na wasomaji wachache na waandishi wa
makala za kuchapishwa hawakuwa wengi pia. 24* Inawezekana kwamba
watu ambao wangeandika makala ya kuchapishwa kwenye jarida walikuwa
na kazi nyingi ya kuandika na kutafsiri vitabu vya Kiswahili ili kutosheleza
mahitaji ya vitabu hivyo. Sababu ya pili ni kwamba matolea machache ya
kwanza hayakuchapishwa kama vitabu bali yalipigwa taipu na kutolewa
nakala. Jarida la kwanza lililochapishwa kama kitabu lilikuwa toleo
namba 6 la Oktoba 1933. Kupigwa chapa huko kulipoanza, ndipo baadhi
ya makala zilipoanza kuchapishwa upya ili ziweze kuwafikia wasomaji
wengi zaidi.

Yale yaliyojadiliwa hapo juu ni baadhi ya mambo muhimu ya kupanga
lugha kitaaluma, ambayo hujulikana pia kama "uhandisi wa lugha",
uliofanywa na Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki. Jarida hali-
kuchapishwa katika mwaka 1937 kutokana na kifo cha Frederic Johnson
aliyekuwa katibu wa kwanza wa Kamati. Johnson alifariki akiwa Aden
mnamo mwezi Machi, 1937.

3.2 Wakati wa vita

Wazungu wengi, baadhi yao wakiwa misheni waliondoka Afrika
Mashariki kwenda nchi zao mbalimbali za Ulaya kujiunga najeshi wakati
wa vita vya pili vya dunia. Kwa sababu hizo hizo na kwa kuwa ilikuwa
hatari kusafiri wakati wa vita, Wazungu wengi waliotarajiwa kujiunga na
misheni kadha hawakuwasili. Kulikuwa na ukosefu wa pesa kwa sababu
ya kugharamia vita. Wanafunzi wa Afrika Mashariki waliopevuka
pamoja na wengi wa walimu wao walijiunga na jeshi lililokuwa likilinda
Afrika Mashariki. Kwa sababu hiyo shuguli zote za kielimu zilififia kama
inavyodhihirishwa na maelezo yafuatayo ya Mkurugenzi wa Elimu,
Kenya mnamo 1942.

"Mahitaji ya viongozi wa jeshi, ya Waafrika ambao walijua kusoma na
kuandika, yalikuwa mengi kama yalivyokuwa katika miaka ya vita
iliyotangulia. Idadi ya vijana walioacha shule za misheni na za
serikali kabla hawajamaliza masomo yao ilikuwa kubwa. Mshahara
mkubwa unaolipwa na jeshi pia umesababisha walimu wa Kiafrika
wengi wa shule za msingi kuacha kazi za kufundisha." 25*

--
24* Hapo mwanzo bila shaka nakala zilikuwa chache sana. Kufikia 1953 nakala zilizokuwa
zikichapishwa zilikuwa kati ya 500 na 600.
25* Kenya Education Department Annual Report 1942, Government Printer - Nairobi, (pia
tazama Lugumba na Ssekamwa 1973: 19).

47

Hali katika nchi zingine za Afrika Mashariki ilikuwa mbaya pia. Nchini
Uganda, kwa mfano, vijana wa kiskauti wa shule walitumiwa kusaidia
askari polisi katika kulinda mji mkuu Kampala. Baadhi ya shule, kama
vile shule ya kilimo ya Gulu ilibidi ifungwe baada ya Mzungu aliyekuwa
akiisimamia kuambiwa arudi kwao Ulaya. (Lugumba na Ssekamwa
1973: 65).

Kuhusu Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki Whiteley 1969,
anadai kwamba hakukuwa na kazi nyingi iliyofanywa na Kamati. Hata
hivyo maoni ya Whiteley yanapingwa vikali na mafanikio ya Kamati ya
wakati huo.

Jarida la Kamati ILC Bulletin lilichapishwa kila mwaka wakati wa vita,
vitabu vingi vilichapishwa, miswada ilipokewa na kushughulikiwa, ku-
likuwa na mashindano ya uandishi wa Kiswahili na vitabu kadha
vilitafsiriwa. Pia jitihada zilifanywa kukisanifisha Kiswahili cha Zaire ili
kiwe sawa na Kiswahili cha Afrika Mashariki. Baadhi ya mikutano ya
Kamati haikuweza kuitishwa wakati wa vita na bila shaka kama haku-
ngekuwa na vita Kamati ingefanikiwa zaidi kati ya 1939 na 1945. Maelezo
yafuatayo yanaonyesha kwamba hatuwezi kudunisha mafanikio ya Kamati
katika miaka hiyo ya hatari.

Jarida la lLC Bulletin Na. 13 la 1959 linatoa orodha ya maneno na
mapendekezo ya matumizi yake ili wasomaji wa jarida watoe maoni yao.
Ni muhimu kutaja kwamba kamati inapendekeza majina kama vile kabila,
chupa na jumba yatumiwe katika ngeli za 9/10 (Ngeli ya N, kwa mfano:
Kabila hii badala ya kabila hili). Kamati ilifikiria kwamba, endapo majina
hayo yangetumiwa kama majina ya ngeli za 5/6 JI-MA), yangevuja sifa ya
maana kwa kuleta hisia mbaya hivi kwamba neno makabila lingeleta
maana ya ushenzi, hali neno majumba lingeonyesha maana ya nyumba
kubwa zisizo na umbo zuri lililolingana.

Katika maelezo hayo kamati ilitilia maanani sana uwezo wa ngeli za 5/6
wa kuleta hisia mbaya ya jina ambalo si muhimu likilinganishwa na maana
ya kuonyesha ukubwa wa jina. Maoni haya ya kamati kuhusu sarufi ya
Kiswahili yalipingwa. Bwana E. B. Huddon aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa
Mashariki nchini Uganda, katika I.L.C. Bulletin Na. 14 ya 1940 anata-
hadharisha kwamba, Wazungu wanaweza kupendekeza kutumia kwa
kabila hii (ngeli ya 9) badala ya kabila hili (ngeli ya 6), Dachi-Madachi
badala ya Dachi-Wadachi nk. lakini itachukua muda kujua ni matumizi
gani yatakayoshika. Anatoa mfano wa vile mabibi na mabwana yanavyo-
tumiwa kama wingi wa bibi na bwana na wala maneno ambayo tungetarajia,
ambayo ni, wabibi na wabwana hayatumiki kamwe. Pia tamko wake zake
ni matumizi sahihi hata ingawa hayafuati kanuni za viambishi vya ngeli.

Majadiliano haya pamoja na ya matumizi ya viambishi m-wa kuonyesha

48

wingi yanaendelea katika matoleo kadha yajarida la I.L.C. Bulletin. Kasisi
Canon A. B. Hellier katika jarida la 1941 kwa mfano, anasisitiza kwamba
kamati inao wajibu wa kukomesha matumizi yasiyokuwa sanifu katika
shule licha ya matumizi ya watu. "Ikiwa baadhi ya watu wataamua kusema
Mataliana badala ya Waitaliano inasikitisha, lakini hatuwezi kuwazuia;
lakini tunaweza kuzuia matumizi kama hayo yasiingie katika vitabu vya
shule". Vile vile Hellier anasema kwamba, Kamati haitashawishiwa
kuandika Waingereza na Waitaliano kama Wengereza na Wetaliano ati
kwa sababu baadhi ya ai huwa e. 26*

Hellier anasema kwamba maneno kama vile rafiki adui na mke ni
baadhi ya maneno ambayo hayafuati kanuni za viambisho vya ngeli katika
hali ya wingi. Anajadili neno mbona kwa kirefu na kudai kwamba ni sawa
na tamko 'kwa nini?'. Hakubaliani na maelezo ya Bull na Snoxall ya hapo
awali kwamba neno mbona, chanzo chake ni navona. Anasema kwamba
nivona ni chanzo kinachofaa zaidi na kwamba ndilo neno lililotangulia
mbona.

Katika jarida namba 14 mapendekezo ya maneno ya Kiswahili ya
msamiati uliochapishwa katika jarida namba 13 yanatolewa; kisha
maneno yaliyokubaliwa ambayo yamesanifishwa yamechapishwa katika
jarida I.L.C. Bulletin Na. 14 la 1941. Ningependa kutaja kwamba Kamati
iliona ni muhimu maneno mlangobahari na pembemraba yaandikwe
hivyo badala ya kuyagawa pembe mraba na mlango bahari.

Kamati pia ilipendekeza maneno ya lugha zingine za Kiafrika yatumiwe
walipokosa maneno ya Kiswahili yanayofaa. Kwa mfano, neno lililo-
sanifishwa la ugonjwa wa ngombe 'ndigano' latokana na neno la Kimasai
'oldikana'. Pia neno ugonjwa mwingine wa ngombe 'kimeta' ni la Kihehe
kinachozungumzwa katika Wilaya ya Malangani, Tanzania. Labda neno
la homa mbaya ya matumbo lililosanifishwa 'entereki' ni la Kimasai pia.

Jarida la I.L.C. Bulletin Na. 16 la 1942 lilichapisha matokeo ya
uchunguzi pamoja na mapendekezo ya Kamati kuhusu mambo kadha ya
sarufi, matumizi na msamiati. Jarida namba 17 la 1943 pia lilichapisha
matokeo ya uchunguzi wa sarufi, matumizi, msamiati na othografia. 27*
Jarida namba 18 la 1944 lilimkumbuka Dkt. Ludwig Krapf na kumsifu
kwa kazi zake za uchunguzi wa Kiswahili na uandishi wake aliouanza
miaka mia moja iliyopita. Mwaka 1944 uliadhimisha miaka 100 tangu
Krapf afike Afrika Mashariki. Mbali na orodha za maneno ya Kiswahili na
Kiingereza, maana, na matumizi yake, makala fupi pia zilichapishwa.
Mwisho kabisa Kamati inawashukuru wanafunzi wa Chuo cha Serekali

--
26* Tazama sehemu ya othografia, sura ya pili.
27* Ili kupata mengi kuhusu othografia soma sura ya pili.

49

cha Uchapishaji cha Dar es Salaam pamoja na mwalimu wao kwa
kuchapisha Jarida la I.L.C. Bulletin kwa miaka mingi.

Makao makuu ya Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki yalihami-
shwa kutoka Dar es Salaam kuenda Nairobi mnamo mwaka 1942.
Wasomaji wa Jarida walijulishwa anwani mpya ya Kamati katika toleo
namba 16 la mwaka huo. Katika jarida namba 17 la 1943 katibu wa
Kamati anawashukuru wasomaji wa jarida kwa kutoa maoni na mape-
ndekezo yao kwa wingi kuhusu Kiswahili. Alisema kwamba maoni na
mapendekezo hayo yalikuwa mengi sana hivi kwamba hayangechapishwa
yote au kujibiwa moja moja. Yaonekana kwamba labda vita viliwafanya
wananchi wa Afrika Mashariki watambue kwamba walikuwa ni jamii
moja na kwamba Kiswahili ndicho kingewaunganisha na kuwawezesha
kujitambua.

Inaripotiwa kwamba katika mwaka uliotangulia (1942), Kamati iliende-
lea kuwasiliana na idara za utangazaji za Kenya na Tanganyika pamoja na
jeshi kuhusu uchapishaji wa vitabu pamoja na mafunzo ya Kiswahili kwa
wanajeshi. Katibu aliendelea kuwasiliana na nchi zingine kwa kuandikiana
barua kwa kuwa vizuizi vya wakati wa vita havikumruhusu kusafiri.
Anarekodi mwamko mpya wa kukipenda Kiswahili uliothibitishwa na
barua nyingi alizozipokea kutoka kote katika Afrika Mashariki. Katibu
Ratcliffe anaandika hivi:

"Usafiri wa wanajeshi na kuongezeka kwa njia za usafiri kumeongeza
sana mahitaji ya othografia sanifu." (I.L.C. Bulletin Na.17 la 1943: 14).

Moja kati ya shughuli kubwa sana za Kamati ya Kiswahili ya Afrika
Mashariki ilikuwa ni kuhakikisha kwamba wanajeshi wamefunzwa
Kiswahili. Jeshi liliwaendea Kamati, nayo Kamati iliwashauri vilivyo.
Sera ilinuia kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya wanajeshi kote katika
Afrika Mashariki. Baadhi ya maafisa vijana wa Kiingereza ilisemekana
hawakupenda kujifunza Kiswahili kwa kuwa hawakuona umuhimu wa
lugha hiyo baada ya vita (Snoxall: mahojiano na mwandishi). Waafrika
wote waliojiunga na jeshi ilibidi wajifunze Kiswahili, ili waweze kuwasiliana
na wanajeshi wenzao waliokuwa wakitumia lugha tofauti. Kwa hivyo,
Kiswahili kikawa lugha ya wanajeshi. Shule zilizokuwa zikisomesha
watoto wa wanajeshi pia zilitumia Kiswahili. (Kwa maelezo zaidi, tazama
Sura ya Tano).

Kimoja kati ya vitabu vilivyotumika sana ni Upcountry Swahili
Exercises kilichoandikwa na Breton. Lakini kitabu kilichotayarishwa na
kuchapishwa na sehemu ya Elimu ya Jeshi la Afrika Mashariki ili
kusomesha wanajeshi Kiswahili kiliitwa A Kiswahili Instruction Book for
the East African Command.

50

Kiswahili walichofunzwa wanajeshi kilikuwa cha mwanzo tu. Hata
baadhi ya wanajeshi waliokijua Kiswahili vizuri hawakukifikiria kuwa ni
Kiswahili safi. Mmoja wao ni C. A. R. Savage aliyekuwa mwanajeshi huko
Jinja, Uganda. Bwana Savage aliyekijua Kijaluo, Kiacholi na Kiswahili
vizuri alikuwa mwanakamati wa Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki
kutoka Uganda. Siku moja mabwana Savage na Snoxall wakiwa safarini
kwenda Nairobi kwa gari la moshi kuhudhuria mkutano wa Kamati,
Bwana Savage alitunga ubeti ufuatao wa Kiingereza kukieleza Kiswahili
cha bara kama kile walichofunzwa wanajeshi:

"Natives who speak Swahili here
Have never heard of Bishop Steere
Their primitive upcountry speech
No rules of Grammar serves to teach
Sometimes really zealous learner
Some concords may pick up from Werner
But "Safi" stuff is heard alone
When Ratcliffe talks to Elphinstone." 28*

Tafsiri:

Wenyeji wanaoongea Kiswahili huku
Hawajamsikia Askofu Steere
Lugha yao ya bara isiyostaarabika
Haifuati kanuni za sarufi
Mara nyingine mwanafunzi mwenye bidii
Hujifunza viambisho vitabuni vya Werner
Lakini lugha iliyo safi husikika tu
Ratcliffe azungumzapo na Elphinstone.

Kamati ilianzisha ushirikiano na Belgian Congo (Zaire) katika shughuli
za kuleta pamoja maendeleo ya Kingwana na ya Kiswahili sanifu (tazama
Sura ya Pili).

Vitabu vinane vipya vilichapishwa mnamo 1942. Vitabu vingi vilipigwa
chapa na misheni za Afrika Mashariki. Pia miswada ishirini na tano
ilipelekwa Kamati, ikiwa ni ya masomo mbalimbali kama vile kilimo,
mazoezi ya viungo na mbinu za kusomeshea. Baadhi ya miswada ilipelekewa
Kamati ili kamati iikague na ithibitishe kwamba othografia ilikuwa sanifu,
nayo miswada mingine ilipelekewa Kamati ili Kamati iisanifishe na
kuichapisha ikiamua kufanya hivyo. Kwa sababu ya vita, katibu anaeleza
kwamba kulikuwa na upungufu wa karatasi na kwamba ilichukua muda

--
28* Snoxall, mahojiano na mwandishi, Februari 10, 1984. Sehemu moja ya ubeti huo pia
yapatikana katika Whiteley, 1969: 79).

51

mrefu kutuma miswada Uingereza ili ichapishwe.

Kama vile nilivyotaja katika mwanzo wa sehemu hii, mashindano ya
uandishi wa Kiswahili yaliiendelea wakati wa vita. Zawadi mbili za
kwanza za uandishi wa insha ya kuelekezwa zilishindwa na Wakenya
wawili kutoka shule za wavulana za Alliance na Mangu. Zawadi ya tatu
ilishindwa na mtu mmoja kutoka Masasi, Tanganyika. Katika shindano la
uandishi wa insha ambapo mwandishi hakuelekezwa, zawadi ya kwanza
na ya tatu zilishindwa na waandishi kutoka Makerere, Uganda, nayo
zawadi ya pili ilishindwa na mwandishi kutoka Dar es Salaam, Tanganyika.
Mashindano mengine yalikuwa ni mashindano ya uandishi na mashindano
ya insha ya wanafunzi wa shule za Wazungu. Akizungumzia ufasaha wa
lugha mhariri wa jarida anasema kwamba Kiswahili kilichotumiwa
chaonyesha kwamba waandishi walikuwa wanaimudu lugha, na walijieleza
vizuri. (I.L.C. Bulletin Na. 17, 1943: 16).

Katika jarida, I.L.C. Bulletin Na. 18 la 1944, ripoti ya mwaka
uliotangulia inaonyesha kwamba mnamo 1943 kulikuwa na mawasiliano
na makundi ya Afrika Mashariki na ya kimataifa ambayo yangesaidia
katika utoaji wa vitabu vya fasihi ya Kiswahili. Katibu alitembelea mikoa
ya Mashariki, Kati na Kaskazini ya Tanganyika kukadiria mahitaji ya
vitabu vya Kiswahili katika shule na vituo vingine vya elimu. Vitabu kumi
vya Kiswahili vilichapishwa na kamati ilipokea miswada ishirini na nane
kuichunguza. Kamati yenyewe iliongezea orodha hii kwa kutafsiri vitabu
vinne.

Mnamo 1943 Waafrika walioshiriki kwenye mashindano ya uandishi wa
Kiswahili, wakiwa ni pamoja na askari jeshi walikuwa 215, lakini
hakukuwa na yeyote aliyeshiriki kutoka shule za serikali za watoto wa
Kizungu. Kitengo cha Kamati kilichokagua mashindano hayo kiliridhika
kwamba mashindano hayo yalisaidia katika kueneza ujuzi wa kusoma na
kuandika. Miswada iliyopokelewa ilionyesha kukua kwa vipawa vya
uandishi ambao ulihitajika sana kwa kuwa kulikuwa na upungufu wa
fasihi ya Kiswahili iliyoandikwa na Waafrika.

Kati ya wale walioshinda zawadi katika mashindano ya 1943 wali-
kuwemo Maurice Otunga wa Holy Ghost College, Mangu, Kenya na
Josiah Muli wa Alliance High School, Kikuyu, Kenya. Katika mashindano
ya 1944, Robert Matano wa Alliance High School, Kikuyu, na Moses
Kinyanjui wa Holy Ghost College, Mangu, pia walishinda zawadi.

Ripoti ya 1944 ilichapishwa katika I.L.C. Bulletin Na. 19 ya 1945.
Ripoti hiyo inataja kwamba Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki
ilikumbwa na matatizo. Hata hivyo jarida halikueleza aina ya matatizo
hayo. Labda kamati ilikuwa na wasiwasi kuhusu pendekezo la Waku-
rugenzi wa Elimu wa Serikali za Afrika Mashariki kwamba Kamati

52

iunganishwe na halmashauri ya uchapishaji - East African Literature
Bureau - iliyonuiwa kuanzishwa. Miswada iliyoendelea kupokewa na
Kamati iliwapa ofisi ya katibu pamoja na wahariri wa Kamati kazi za
kutosha za kufanya mwaka huo. Wahariri hao walipongezwa kwa
kufanya kazi kwa bidii, licha ya upungufu wa wafanyakazi wakati wa vita.
Vitabu kumi vipya vilichapishwa mnamo 1944 na miswada kumi na tisa
ilipokelewa. Kwa upande wake kamati ilitafsiri vitabu kumi na vinne.

Kazi iliyofanywa na Kamati wakati huu wa vita, kulipokuwa na
upungufu wa pesa na wafanyakazi ilikuwa nyingi na ya kushangaza. Kati
ya 1942 na 1944, kipindi kifupi cha miaka mitatu Kamati iliripoti kwamba
ilichapisha jumla ya vitabu ishirini na vinane (28). Ilikuwa imetafsiri
vitabu kumi na vinane (18), pamoja na kushughulikia miswada sabini na
miwili (72).

Vita havikupunguza usomaji wa vitabu, bali vitabu viliuzwa kwa wingi
zaidi. Ratcliffe anaandika kwamba "ingawaje ni wakati wa vita, vitabu vya
Kiswahili havijawahi kununuliwa kwa wingi jinsi hii". (Ratcliffe I.L.C.
Bulletin Na. 18, 1944: 4). Mnamo 1943 pekee, Ratcliffe anaripoti kwamba
zaidi ya vitabu 330,000 vya Kiswahili vilivyochapishwa huko Uingereza
viliuzwa katika Afrika Mashariki, mbali na nakala 70,000 za vitabu
vilivyochapishwa Afrika Mashariki. Kamati inapendekeza Kiswahili kitu-
miwe katika kuelimisha watu kwa wingi badala ya kutumia lugha za
kwanza zilizokuwa zikipendekezwa, ambazo zilitumiwa na idadi ndogo ya
watu wa kabila moja moja.

Jarida la I.L.C. Na. 19 la 1945, lilichapishwa mwezi Novemba wa
mwaka ambao vita vya pili vya dunia vilimalizika. Jarida linashangilia
kukomeshwa kwa uhasama huko Ulaya. Kumalizika kwa vita kulileta
mabadiliko mengi. Yasemakana kwamba Kamati ya Kiswahili ya Afrika
Mashariki ilipewa miradi mipya na kwamba mambo yaliyokuwa yakitiliwa
mkazo kuliko hapo awali yalikuwa ni kusoma na kuandika pamoja na
ukuzaji wa lugha za kwanza. Mhariri wa Jarida anasema hivi - "Mengi
yamesemwa na yangali yanasemwa kuhusu kuhitajika kwa Kiingereza
kama lugha ya kusomesha masomo mengine, lakini itachukua muda
mrefu kabla Kiingereza hakijakuwa tiba ya Waafrika ya kutojua kusoma
na kuandika". (I.L.C. Bulletin Na. 19, 1945: makala ya mhariri).

Kutiliwa mkazo huku kwa Kiingereza na lugha za kwanza mara tu
baada ya vita, kulikuwa ndiyo mwanzo wa kudhoofika kwa shughuli za
Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki. Usanifishaji wa Kiswahili
ulikuwa umeanza kushuka kutoka upeo wake. Kamati ilitambua hivyo na
ikajaribu kuonyensha kwamba Kiingereza hakingeweza kutumiwa ku-
pigana na hali ya kutojua kusoma na kuandika. Ilibidi lugha za Kiafrika
zitumiwe. Kwa kuwa ingekuwa ghali sana kukuza lugha nyingi za kwanza,

53

ingekuwa bora Kiswahili kitumiwe. Kiswahili kilikuwa kimejitambulisha
kama lugha sanifu iliyotumika kote katika Afrika Mashariki. Kilikuwa na
maandishi mengi yaliyokuwa yakiongezeka kwa wingi, na hiyo ndiyo
sababu Kamati ikaonelea kwamba Kiswahili pekee ndicho kinachofaa
kwa elimu ya watu wengi.

Afisi ya Kikoloni haikufuata mapendekezo ya Kamati. Kwao lilikuwa
suala la kisiasa. Ilibidi Wakoloni watumie mbinu mpya kuwatawala
Waafrika ambao walikuwa wamepevuka kisiasa baada ya kushiriki katika
vita. Waafrika walikuwa wameutambua udhaifu wa Wazungu wakati wa
vita. Ilikuwa wazi kwao kwamba iwapo wangeshirikiana wangeweza
kupinga utawala wa kikoloni.

Watawala wa kikoloni walikuwa na hamu ya kutumia mgawanyiko wa
lugha za kwanza ili kuwatenganisha Waafrika. Kuendelea kutumiwa kwa
lugha moja ya Kiswahili kungeleta matokeo yaliyo kinyume cha yale
yaliyotarajiwa, kwa kuwa kungewaunganisha Waafrika. Kiingereza haki-
ngekuwa na matokeo kama hayo kwa kuwa kingewaunganisha Waafrika
wachache walioelimika, ambao hawangekuwa tisho kubwa kwa serikali ya
kikoloni. Sera hii mpya ya kupunguza mkazo wa Kiswahili ilijitokeza na
kuiudhi Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki na bila shaka ndiyo
Jarida linayoigusia linapotaja kwamba Kamati ilikumbwa na matatizo
fulani.

54

Sura ya Nne

4.0 Kamati baada ya vita

4.1 Kipindi cha Nairobi (1946-1952)

Tayari tumetaja kwamba kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki
(I.T.L.C.) ilihamisha makao yake makuu kutoka Dar es Salaam hadi
Nairobi mnamo mwaka wa 1942. Sehemu hii inahusu maisha ya kamati
jijini Nairobi baada ya vita vikuu vya pili vya dunia kuanzia mwaka 1946
hadi 1952. Baada ya kukaa Nairobi, makao makuu ya kamati yalihamishwa
hadi Kampala.

Jarida la I.L.C Bulletin halikuchapishwa mnamo mwaka wa 1946.
Mkutano wa kwanza wa Kamati yote, tangu vita vianze mwaka 1939,
ulikuwa mjini Nairobi tarehe 4 na 5 Machi mwaka 1946. Kama ilivyo-
jadiliwa katika Sura ya Tatu hakukuwa na mikutano ya kamati yote
wakati wa vita. Mikutano iliyokubaliwa ilikuwa ni ile kitengo cha kamati
ambacho kilihudhuriwa na wasomaji, mwenyekiti na katibu. Kitengo
kilifanya uchunguzi wa lugha na kazi zingine kama vile ukaguzi wa
mashindano ya uandishi.

Kama ilivyotarajiwa mabadiliko kadha yalikuwepo hasa kuhusu
uanachama wa kamati baada ya vita. Kamati ilipokutana mwaka 1942
Wakurugenzi wote wa Elimu kutoka Tanganyika, Uganda, Kenya na
Zanzibar walikuwa wapya. Kwa hivyo walikuwa wakihudhuria kikao cha
kamati kwa mara yao ya kwanza. Wasaidizi wa wahariri wa Kiafrika
kutoka nchi zote nne, pia walihudhuria kikao cha Kamati kwa mara yao
ya kwanza. Mbali na mabadiliko haya, pia kulikuwa na mabadiliko katika
ajenda ya mkutano ambayo ilihusu zaidi masuala ya lugha zingine za
Kiafrika kuliko Kiswahili. Kama itakavyojadiliwa kwa kirefu katika Sura
ya Tano, Kipindi hiki cha Kamati, baada ya vita kilikuwa na mabadiliko
mengi kuhusu sera ya lugha ambapo Kiingereza na lugha kadha za
Kiafrika zilianza kutiliwa mkazo badala ya Kiswahili.

Jarida la I.L.C. Bulletin Na. 20 lilichapishwa mwaka 1947. Kama
ilivyokuwa kawaida, jarida lilikuwa na maoni mengi kuhusu lugha kutoka
kwa wasomaji. Mwandishi mmoja ambaye makala yake yametokea katika
majarida ni A. N. Tucker kutoka School of Oriental and African Studies,
Chuo Kikuu cha London. Katika maandishi yake yanayohusu mtindo wa
kuandika lugha, anasema kwamba lugha zingine za Kibantu zatakikana
zitumie mtindo wa kuandika Kiswahili kama kielekezo. Hata hivyo

55

anatahadharisha kuhusu miundo tofauti ya baadhi ya lugha za Kibantu
kama vile kuwepo na irabu saba badala ya tano za Kiswahili na hali ya
kuwa na irabu mbili zilizofuata katika neno moja (ambapo irabu hizo
zinasababisha neno liwe na maana tofauti). Tucker anatahadharisha
kwamba tofauti kama hizo zitiliwe maanani wakati wa kuunda mtindo wa
kuziandika lugha za Kibantu.

Katika mwaka wa 1946 uliotangulia, jumla ya miswada ishirini na mbili
ilikabidhiwa Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ili iishughulikie.
Vitabu kumi na moja vya Kiswahili vilichapishwa na vitabu vingine vitano
vikatafsiriwa na wafanyakazi wa afisi ya katibu mtendaji. Mashindano ya
uandishi wa Kiswahili yaliendelea kuwavutia washiriki wengi kutoka
shule za Kiafrika hata ingawa hakukuwa na walioshiriki kutoka shule za
Wazungu.

Jarida la I.L.C. Bulletin halikuchapishwa katika miaka ya 1948, 1949 na
1950 ambapo mabadiliko kadha yalikuwa yakitendeka. Licha ya hivyo,
jumla ya vitabu vipya ishirini na sita vya Kiswahili vilichapishwa wakati
huo. Pia wahariri wa Kamati pamoja na katibu walikabidhiwa miswada
156 (mia moja hamsini na sita) kuishughulikia.

Mnamo mwezi wa Disemba mwaka wa 1949 Rev. B. J. Ratcliffe katibu
wa Kamati alistaafu. Rev. Ratcliffe alifika Afrika ya Mashariki kwa mara
ya kwanza mwaka 1899 alipoanza kazi za kidini katika wilaya ya Tana
River nchini Kenya. Uhusiano wake na Kamati ya Kiswahili ya Afrika
Mashariki ulianza hapo mwaka 1930 alipochaguliwa kuwa mhariri
kuwakilisha Kenya. Alishikilia wadhifa huo hadi mwaka 1937 alipo-
ajiriwa kuwa katibu baada ya kifo cha Frederick Johnson aliyekuwa
katibu wa kwanza wa Kamati.

Shughuli kubwa aliyoifanya Ratcliffe kama katibu ilikuwa ni kuha-
kikisha kwamba kamusi mbili Standard Swahili-English na English-
Swahili zimechapishwa. Kamusi hizo zilikuwa zimehaririwa na Frederick
Johnson kutegemea msingi uliowekwa katika kamusi za Madan. Ratcliffe
aliweza kutetea vilivyo, matumizi ya msamiati wa lahaja tofauti za
Kiswahili. Kufuatia juhudi zake, msamiati wa lahaja za Kenya, hasa
Kimvita uliweza kuingizwa kwenye kamusi - jambo ambalo halinge-
dhaniwa kwamba lawezekana mwaka 1928.

Baada ya Ratcliffe kustaafu, mkurugenzi wa East African Literature
Bureau, Bwana C. G. Richards alishikilia wadhifa wa katibu kwa muda.
Baada ya Richards, Bwana H. E. Lambert alichaguliwa kuwa kaimu wa
katibu hadi mwezi wa Agosti 1952 wakati W. H. Whiteley alipouchukua
uwadhifa wa katibu.

Wakati jarida la I.L.C. Bulletin la mwaka wa 1951 lilipochapishwa,
tayari Kamati ilikuwa imeundwa upya. Kamati ilibadilisha jina kutoka

56

lnter-Territorial Languages (Swahili) committee (I.L.C.), likawa East
African Inter-Territorial Language (Swahili) Committee (E.A.I.L.C.).
Tangu Kamati hii ya Kiswahili ya Afrika Mashariki iundwe mwaka 1930,
ilikuwa chini ya (mamlaka ya ) halmashauri ya Magavana wa Afrika ya
Mashariki. Kwanzia Januari moja mwaka 1948 Kamati ilianza kuwa chini
ya tume ya East African High Commission.

Katika mwaka wa 1950 kulikuwa na mkutano uliohudhuriwa na
maafisa wakuu wa Kamati kutoka nchi zote za Afrika ya Mashariki
pamoja na Bwana C. G. Richards aliyewakilisha halmashauri ya uchapi-
shaji wa vitabu - East African Literature Bureau. Mwenyekiti wa
mkutano huo alikuwa ni afisa tawala wa East African High Commission.
Mkutano huo uliitishwa kujadili kazi za Kamati tangu kuanzishwa kwa
East African Literature Bureau. Ilikubaliwa kwamba Kamati ingeendelea
kuwepo kama chombo cha lugha ambacho ni tofauti na East African
Literature Bureau. Ilikubaliwa kwamba Kamati ingeendelea kujihusisha
zaidi na uchunguzi wa lugha na somo la Kiswahili. Kamati pia ingebakia
kuwa mamlaka ya juu kuhusu uandishi na uchapishaji wa vitabu vya
Kiswahili.

Nayo halmashauri ya East African Literature Bureau ilipewa mamlaka
ya utoaji na uchapishaji wa vitabu. Kazi hiyo hapo awali ilikuwa ikifanywa
na Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki. Pia kazi ya upangaji wa
mashindano ya uandishi wa Kiswahili ilikabidhiwa East African Literature
Bureau hata ingawa usomaji na utoaji uamuzi wa maandishi hayo ulikuwa
ukifanywa na Kamati. Kwa sababu ya ushirikiano huu wa kufanya kazi
kati ya Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki na halmashauri ya
uchapishaji, naonelea ni bora nieleze machache kuhusu East African
Literature Bureau.

East African Literature Bureau iliundwa mwezi Januari, 1948 kama
mojawapo ya huduma zilizotolewa na East African High Commission.
Iliundwa baada ya kufanywa uchunguzi ulioagizwa na mkutano wa
Magavana wa Afrika Mashariki. Uchunguzi huo ulifanywa kuanzia Julai
1945 hadi 1947. Kwa maoni ya J. W. Chege (1978: 128) East African
Literature Bureau ilirithi kampuni ya uchapishaji ya C.M.S. iliyojulikana
kama Ndia Kuu Press (Highway Press). Meneja wa kampuni hiyo C. G.
Richards, pia ndiye aliyechaguliwa kuwa mkurugenzi wa kwanza wa East
African Literature Bureau. Kazi za uchapishaji za Ndia Kuu Press
zilichukuliwa na East African Literature Bureau.

Makao makuu ya East African Literature Bureau yalikuwa mjini
Nairobi, lakini pia kulikuwa na matawi madogo huko Kampala na Dar es
Salaam. Tawi la Kampala lilikuwa likihudumia Uganda nalo tawi la
Dar es Salaam lilihudumia Tanganyika na Zanzibar. Pia halmashauri hii

57

ilitoa huduma za maktaba kwa kutumia magari yaliyozitembelea shule na
miji ya Afrika Mashariki. Huduma hii ya maktaba pia ilitolewa kupitia
njia ya posta.

East African Literature Bureau ilianzishwa ili kutosheleza mahitaji ya
vitabu yaliyokuwa yakiongezeka kwa haraka kati ya Waafrika walio-
elimika. Kwa hivyo ilitarajiwa kuchapisha na kutawanya "vitabu vya
fasihi kwa watu wa kawaida, vitabu vya lazima vya shule, vitabu vya kilimo
na ufundi vya watu wazima, magazeti au majarida, kuwasaidia waandishi
wa Kiafrika na kutoa huduma za maktaba. Mahitaji ya Waafrika
yangehudumiwa kwanza, lakini pia, halmashauri hiyo ilitakikana ichapishe
vitabu vya fasihi kwa Wahindi". 29*

Kazi ya uandishi wa vitabu vya lazima vya shule uligawanywa katika
sehemu nne.

(i) Kuandika na kuhariri miswada ya vitabu vya walimu na
wanafunzi ili kutosheleza mahitaji ya ratiba za Idara za Elimu.
(ii) Kufanya vivyo hivyo kwa vitabu vya ziada.
(iii) Kutafsiri au kukagua tafsiri za Kiswahili, Kiluganda, Kijaluo
na Kikikuyu na kufanya mpango wa tafsiri kama hizo nje ya
halmashauri kwa lugha zingine zinazohitajika katika elimu.
(iv) Kushughulikia miswada ya vitabu vya lazima na maswali
kutoka kwa wachapishaji.

Sehemu ya uchapishaji wa magazeti ya East African Literature Bureau
ilichapisha gazeti la kila wiki lijulikanalo kama Tazama. Gazeti hilo
lilikuwa likitolewa zaidi ya nakala 17,000. Tazama lilianza kuchapishwa
na East African Standard mwaka 1956. Tafsiri ya Tazama kwa Kiluganda
ilikuwa ikichapisha nakala chache sana.

J. W. Chege (1978: 30) anayo maoni kwamba vitabu vya East African
Literature Bureau vilinuiwa kutosheleza "mahitaji ya kikoloni ya kuko-
mesha kutoridhika na ukoloni na kwamba vilichapishwa kufuatia mashauri
na kibali cha Baraza la Ushauri". Ushirikiano wa East African Literature
Bureau na mashirika ya uchapishaji ya Uingereza kama vile MacMillan,
Longman na Thomas Nelson n.k, kwa maoni ya Chege ilikuwa ni hila ya
wakoloni ya kumiliki biashara za uchapishaji. Anatoa mifano na tarakimu
kuthibitisha dai lake kwamba vitabu vilivyokuwa vikinunulika kwa wingi
zaidi vilipewa wachapishaji hao baada ya East African Literature Bureau
kuhakikisha kwamba vingenunuliwa kwa wingi katika matoleo ya kwanza.
'Mkurugenzi mkoloni' (C. G. Richards) alifaulu sana kwa hila hii hivi
kwamba wakati wa kustaafu 'alipendekeza kwamba East African Literature

--
29* East African Literature Bureau, Annual Report for 1950: 2.

58

Bureau ivunjiliwe mbali kwa kuwa ilikuwa tayari imetimiza kazi zake na
kwamba makampuni yaliyomiliki uchapishaji yalikuwa na uwezo wa
uchapishaji'. (Chege 1978: 131).

Kamati iliyoundwa upya ilikuwa na watu tisa, wawili kutoka kila nchi
pamoja na katibu. Idadi hii ilikuwa ndogo sana ikilinganishwa na
wanakamati kumi na saba - wanne kutoka kila nchi na katibu. Snoxall
hufikiria kwamba kupunguzwa kwa wanakamati ilikuwa ni hatua ya
maendeleo. "Ni maendeleo mazuri kwamba uwanachama wa kamati
umepunguzwa kuwa kundi dogo la wataalamu wenye bidii na kwamba
mashindano ya uandishi na kazi za uchapishaji wa vitabu vya shule
zimechukuliwa na East African Literature Bureau" (Snoxall E.A.I.L.C.
Bulletin Na. 22, 1952:3).

Orodha mpya ya shughuli za Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki
iliyoundwa upya ilikubaliwa katika kikao cha kumi na tatu (13) cha
kamati. Shughuli hizo zilizoorodheshwa hapa chini zilitilia mkazo
uchunguzi katika maeneo kama vile fasihi ya Kiswahili na lahaja.
Shughuli zifuatazo za Kamati zilikubaliwa:

a) Kuandaa vifaa vya kutosha vya kusomesha Kiswahili.
b) Kurekebisha na kuchapisha upya makamusi ya Kiswahili
kutegemea matokeo ya utafiti.
c) Kushirikiana na mabaraza ya lugha kuhusu mitihani.
d) Kuwajulisha watu wa Afrika Mashariki mambo yanayohusu
hadhi, umuhimu na maendeleo ya Kiswahili kupitia vyombo
vya kutawanya habari.
e) Kufanya uchunguzi juu ya historia ya Waswahili, lugha,
lahaja, uhifadhi na ufafanuzi wa fasihi ya jadi ya Waswahili.
f) Kuendelea kuwa na mawasiliano kati ya nchi zinazotumia
Kiswahili - Tanganyika, Zanzibar, Kenya, Uganda, Rhodesia
ya Kaskazini (Zambia), Nyasaland (Malawi), Somaliland
(Somalia), Kongo ya Ubelgiji (Zaire) na Visiwa vya Komoro.
g) Kuendelea kuwa na mawasiliano kati ya kamati na mashirika
ya kielimu, vyuo, na vyuo vikuu vinavyoshughulikia Kiswahili
kama vile Chuo Kikuu cha London, Chuo Kikuu cha Afrika ya
Kusini, Leyden, Lourain na Berlin, pamoja na kuvihimiza
vyuo vikuu vingine vianzishe somo la Kiswahili.
h) Kuhimiza kuanzishwa kwa somo la Kiswahili katika shule za
Wazungu na za Wahindi katika Afrika Mashariki ili kuwe na
ushirikiano wa kijamii; na ili kuwezesha kupata wanaisimu
watakaoweza kufanya uchunguzi wa somo hili katika siku za
baadaye.

59

i) Kudondoa makala muhimu kuhusu somo la Kiswahili kutoka
kwenye majarida ya vyuo na mashirika yanayohusika na
Kiswahili.
j) Kuongoza au kukagua usomeshaji wa Kiswahili katika vituo
vilivyokubaliwa ili kurekebisha mitindo isiyofaa ya kufunza
somo la Kiswahili.
k) Kufanya kazi za ukatibu wa kamati za lugha zisizo za Serikali.

Orodha ya shughuli za Kamati inayo mambo mengi sana. Kama katibu
Whiteley alivyokiri baadaye "Kamati ingeweza kutekeleza michache kati
ya miradi iliyoorodheshwa, zaidi kwa kuwa, katibu atakuwa na kazi
zingine mbali na ukatibu". (E.A.I.L.C. Bulletin Na. 23, 1953: 7).

Taarifa ya mhariri ya Bulletin Na. 21 inatangaza kuajiriwa kwa
Bi. D. V. Perrott wa U.M.C.A. ambaye pia ni mwandishi wa kitabu
kiitwacho Teach Yourself Swahili, kuwa mhariri wa Kamati ya Kiswahili
ya Afrika Mashariki huko London. Kazi hii mpya ingemwezesha muajiriwa
kuiwakilisha Kamati huko London, hasa katika kuisoma miswada
inayochapishwa huko Uingereza. Hapo awali miswada hiyo ilikuwa
ikitumwa katika ofisi ya katibu kusomwa. Kuwa na mhariri huko London
kulinuiwa kupunguza gharama za kutuma miswada kati ya London na
Afrika Mashariki.

Toleo la E.A.I.L.C. Bulletin Na. 22 la 1952 lilikuwa na makala muhimu
ya somo la Kiswahili. Makala hayo ni pamoja na jinsi ya kusomesha
Kiswahili kama lugha ya kigeni iliyoandikwa na Ali Ahmed Jahadhmy,
viambishi KA na U iliyoandikwa na J. Williamson pamoja na makala ya
H. E. Lambert kuhusu vile tafsiri inavyoathiri Kiswahili.

Katika mkutano wa kumi na nne (14) wa kila mwaka uliokuwepo
Nairobi Oktoba 17, 1951, Kamati ilijadili mambo kadha kuhusu lugha na
katiba pia. Pamoja na hayo kamati ilijadiliana kuhusu uwezekano wa
kuyapeleka makao makuu yake huko Kampala katika Chuo cha Makerere.
Pendekezo la kuishirikisha Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki na
Makerere liliwasilishwa kwa mkuu wa Chuo cha Makerere na afisa tawala
wa East African High Commission mwezi Januari 1952. Baraza la Chuo
lilijadili pendekezo hilo na kulipitisha mwezi Aprili mwaka huo huo.
Mapatano hayakuchukua muda mrefu kufikiwa kwa sababu Taasisi ya
Ucunguzi wa Shughuli za Jamii ya Afrika Mashariki ya huko Chuoni
tayari ilikuwa imeanzisha uchunguzi wa lugha.

Katibu mpya Bwana Wilfred Howard Whiteley alikuwa tayari ameajiri-
wa kama mchunguzi mwandamizi wa isimu na lugha za Kibantu na
Taasisi ya Uchunguzi wa Shughuli za Jamii. Whiteley alijifunza Kiswahili
katika School of Oriental and African Studies, Chuo Kikuu cha London

60

kwa miaka miwili. Pia alikuwa amefanya kazi kwa muda wa karibu miaka
mitatu kama afisa wa shughuli za jamii huko Tanganyika. Akiwa huko
Makerere, Whiteley angeendelea na uchunguzi wake kwa lugha kadha za
Kibantu huko Tanganyika mbali na kazi zake za kutoa mihadhara.

Mwezi Septemba 1952 katibu mpya, W. H. Whiteley, alishika usukani
kutoka kwa katibu wa muda, H. E. Lambert mjini Nairobi. Whiteley
aliyahamisha makao makuu ya Kamati hadi Chuo cha Makerere Kampala
ambapo kamati iliambatanishwa na chuo hicho mwaka huo huo wa 1952.
Whiteley aliposhika usukani kazi nyingi za Kamati zilihusu kutoa idhini
ya kuchapishwa kwa miswada baada ya kuisoma na kuirekebisha vilivyo.
Mradi mwingine uliokuwa shughuli kubwa ya Kamati, hasa katibu, ni ule
wa kuchapisha jarida la E.A.I.L.C. Bulletin ambalo lilikuwa jukwaa la
kujadili masuala muhimu yanayohusu Kiswahili.

Akiwa Makerere, Whiteley alijikuta na shida ya kufanya kazi zote za
ukatibu kwa kuwa, kama tulivyotaja, alikuwa na kazi za uchunguzi na
kusomesha pia. Ilikuwa vigumu kwake kufanya kazi hizi zote pamoja na
kusoma miswada ipatayo minne kila mwezi ambayo ilipelekewa kamati
kuishughulikia. Kwa hivyo Whiteley aliwaajiri wahariri watatu wa muda,
kumsaidia. Mmoja alitoka Makerere na wawili walitoka Dar es Salaam.
Afisa tawala wa muda pia aliajiriwa ili kuvipanga vizuri vitabu vya
maktaba ya Kamati na kufanya mambo mengine kama vile kupanga vizuri
faili za Kamati.

Shughuli za uchapishaji wa vitabu hazikuwa tena mikononi mwa
Kamati, kama tulivyoeleza. Kwa hivyo, kufikia mwaka 1953 waandishi
wengi walikuwa wakiipeleka miswada yao moja kwa moja kwa East
African Literature Bureau bila ya kupata ithibati ya Kamati. Isipokuwa
miswada hiyo iwe ni ya vitabu vya shule, East African Literature Bureau
haikutakikana isisitize kuwepo kwa kibali cha Kamati kabla ya kuvichapi-
sha vitabu. Kwa hivyo Kamati ililifikiria jambo hili na kuamua kutoa
idhini kwa vitabu vichache vilivyochaguliwa kama vile, vitabu vya sarufi
na vitabu vya lazima vya kutumiwa shuleni. Kusomwa na Kamati kwa
miswada mingine kulikomeshwa. Uamuzi huu uliipatia afisi ya katibu
nafasi ya kupumua kwa kuwa uliiondolea kazi ya kuchosha ya kuisoma
miswada mingi ambayo baadhi yake haikuambatana na shughuli za
kamati mbali na kuwa imeandikwa kwa Kiswahili.

Mwaka uliofuata, 30* Whiteley, alijaribu kutoa sababu za msimamo wake
mpya kuhusu ithibati kwa kusema kwamba, kusisitiza Kiswahili kiwe na
umbo maalum kulisababisha lugha ionekane kama iliyobuniwa kwa
kukosa uhalisi wake.

--
30* Tazama E.A.I.L.C. Bulletin Na. 23 ya 1953.

61

4.2 Kipindi cha Makerere (1952-1960)

Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ilikuwa na makao yake
makuu Makerere, Kampala kuanzia mwaka 1952 hadi mwaka 1962.
Katika sehemu hii nitajadili shughuli za kamati kufikia mwaka 1960 kwa
kuwa shughuli za kati ya mwaka 1960 na 1962 zinahusu zaidi sura ya sita
inayojadili kubadilika kwa kamati kuwa Taasisi ya Uchunguzi wa
Kiswahili.

Jarida la E.A.I.L.C. Bulletin Na. 23 la 1953 linayo makala ya kurasa
ishirini iliyoandikwa na H. E. Lambert kuhusu lahaja ya Kivumba cha
kisiwa cha Wasini na jimbo karibu na Vanga katika kusini mwa pwani ya
Kenya. Lambert pia anajadili utenzi wa kutekwa kwa mji wa Tumbe na
Waswahili (Wavumba) kutoka Vanga pamoja na shairi la kumsifu Mwana
Mnga. Maandishi haya yalikuwa ni matokeo ya uchunguzi uliofanywa na
Lambert huko Vanga ambacho ni kijiji cha Waswahili cha kusini zaidi
nchini Kenya. Shairi hilo la mwisho lasemekana kwamba lilitungwa na
mshairi mashuhuri Muyaka, lakini kama Lambert anavyoeleza, hakuna
ushahidi wa kutosha kuthibitisha au kukanusha dai hili.

Kufikia wakati huu, Kamati ilikuwa tayari imeanza kuchunguza zaidi
lahaja za Kiswahili. Makala ya Lambert yalikuwa ni mfano tu wa matokeo
ya uchunguzi huo. Baadhi ya matokeo ya uchunguzi huo wa lahaja
yalichapishwa katika Jarida la E.A.I.L.C. Bulletin lakini mengine yali-
chapishwa kama vitabu kama tutakavyoendelea kujadili.

Mnamo mwaka wa 1954 jarida lilibadilishwa jina kutoka Bulletin hadi
Journal. Pia jina la Kamati lilibadilishwa kutoka jina refu la East African
Inter-Territorial Language (Swahili) Committee, hadi East African Swahili
Committee. Katika makala ya mhariri jarida la EASC Journal Na. 24 la
1954, Whiteley anaeleza kwamba hapo awali jarida lilikuwa likichapisha
taarifa rasmi fupi za habari kwa raia ambayo ni maana halisi ya neno
Bulletin. Anasema kwamba neno Journal linafaa zaidi kwa jarida jipya
litakalokuwa kubwa kuliko Bulletin na litakalochapisha makala ndefu
zaidi zenye kuamsha msisimko wa wasomi ili kuwafanya watoe mchango
wao kwa kuandika makala. Kuanzia na toleo la 1954 Whiteley alitarajia
matoleo yote ya jarida yawe kielelezo katika makala yote yanayochapishwa.

Toleo la 1954 ni mfano bora wa aina ya jarida alilolitaka Whiteley.
Lilikuwa na makala ndefu kuhusu vimiliki katika Kiswahili sanifu
iliyoandikwa na O. B. Kopoka. Baada ya kupata makala ya Kopoka,
katibu ambaye pia ni mhariri wa jarida, alimwuliza H. E. Lambert aandike
kuhusu vimiliki katika lahaja huku akitoa mifano kutoka lahaja kadha za
Kiswahili. Mwishowe anaongeza makala inayojadili vimiliki katika
Kidigo kutokana na maandishi ya Z.M.S. Zani ili kulinganisha na

62

Kiswahili na kukamilisha mjadala huu wa vimiliki. Mbali na vimiliki,
jarida hili linayo makala kadha ya uchambuzi wa vitabu.

Katika jarida hili la 1954 pia tunafahamishwa kwamba tayari Kamati
imeanzisha uchunguzi wa lahaja za Kiswahili pamoja na uchambuzi wa
matumizi ya Kiswahili katika magazeti.

Katika mkutano wa kumi na saba (17) wa Kamati ya Kiswahili ya
Afrika Mashariki uliokuwepo kati ya Februari 10 na 12 1954 ilikubaliwa
kwamba nakala zote za Jarida la EASC Journal zitakuwa zikiuzwa
kuanzia wakati huo. Kabla ya hapo nakala za E.A.I.L.C. Bulletin zilikuwa
zikitolewa bure.

Jarida la EASC Journal Na. 25 la 1955 limechapisha makala nyingi
kuhusu Kiswahili. Makala hizo ni pamoja na ya W. H. Whiteley kuhusu
lahaja ya Kimvita, makala ya O. B. Kopoka inayohusu maneno yanayoishia
kwa irabu yenye kuonyesha nia inayotazamia na vile yanavyotumiwa
katika mashairi ya zamani ya Kiswahili. E. B. Haddon pia anaijadili hiyo
nia ya kutazamia katika makala yake. Kurasa zilizobaki za jarida zinazo
makala za uhakiki au uchambuzi wa vitabu pamoja na barua za wasomaji.

Kujadiliwa kwa undani kwa nia inayotazamia kunatokana na utaratibu
mpya wa jarida ulioanzishwa na Whiteley wa kuandika makala ya
kitaaluma ya Kiswahili. Matoleo mengine ya jarida yaliyochapishwa
wakati Whiteley akiwa katibu wa Kamati yalifanana na hayo yaliyojadiliwa
hapo juu. Yaelekea hakukuwa na kiwango kilichowekwa cha urefu wa
makala zilizochapishwa. Kati ya zile ndefu sana ni Habari za Wakilindi
makala (kitabu) yenye karibu kurasa 50 iliyoandikwa na Abdallah bin
Hamed bin Ali Liajjemi na kuchapishwa na EASC Journal Na. 27 1957.
Orodha za istilahi au msamiati wa kitaaluma zimechapishwa katika
matoleo kadha ya jarida. Kwa mfano, istilahi za uchaguzi zimechapishwa
katika EASC Journal Na. 27 la 1957 na istilahi za ujenzi zimechapishwa
katika EASC Journal Na. 28/1 la 1958.

Katika mwaka wa 1956, mbali na kuchapisha jarida kamati ilianza
kutayarisha vitabu vya ziada ambavyo vingechapishwa kama nyongeza
kwa jarida. Karibu vitabu hivyo vyote vilikuwa tenzi. Utenzi wa Vita vya
Wadachi kilichohaririwa na J. W. T. Allen kilikuwa tayari kimechapishwa
katika mwaka 1955 kama kitabu cha ziada ya EASC Journal Na. 25.
Miaka miwili baadaye Utenzi wa Vita vya Majimaji kilichoandikwa na
Abdul Karim bin Jamaliddini kilichohaririwa na W. H. Whiteley kili-
chapishwa kama kitabu cha ziada ya EASC Journal Na. 27 la 1957. Vitabu
vingine vya ziada vilichapishwa mwaka wa 1958. Vitabu hivyo ni Maisha
ya Siti Binti Saad cha Shaaban Robert EASC Journal Na. 28/1 na
Maisha ya Hemed bin Mohammed, Yaani Tippu Tip Kwa Maneno Yake
Mwenyewe kilichoandikwa utangulizi wa kihistoria na kufasiriwa na Bi

63

Alison Smith. Kitabu hiki kilikuwa cha ziada ya Jarida la EASC Journal
Na. 28/2 la 1958.

Nyongeza ya kamusi ambayo ilitarajiwa kuchapishwa kama kijitabu
ilichapishwa katika jarida la EASC Na. 26 la 1956. Wazo la kuchapisha
nyongeza ya kamusi lilijadiliwa katika mikutano kadha ambayo ni pamoja
na mkutano wa kumi na tisa (19) wa kila mwaka wa Kamati wa Desemba
1955. Maneno yaliyokusudiwa kuchapishwa katika nyongeza hiyo ya
kamusi yalichapishwa katika matoleo kadha ya jarida.

Wazo la kuchapisha nyongeza ya kamusi ya Kiswahili-Kiingereza na
Kiingereza-Kiswahili yaonekana lilikuwa limetupiliwa mbali kufikia
mwaka 1959 ambapo katibu aliulizwa atafute njia za kupata pesa za
kuchapisha kamusi timilifu ya Kiswahili-Kiingereza. Wazo la kamusi
mpya lilizuka baada ya kulinganisha kamusi sanifu ya Kiswahili-Kiingereza
na kamusi kubwa zaidi za lugha "ndogo" kuliko Kiswahili. Kamati
ilionelea kwamba ikiwa ushirikiano wa watawala wa Kibelgiji huko
Kongo ungepatikana, kamusi za Kiswahili-Kiingereza na Kiswahili-
Kifaransa zingechapishwa wakati mmoja. Kwa kufanya hivyo gharama
ingepunguzwa na pengo kati ya Kiswahili sanifu na lahaja ya Kingwana
ingepunguzwa. 3l*

Makala kubwa za jarida la EASC Journal la 1956 zilikuwa ni pamoja na
mchangio wa Wajerumani katika somo la Kiswahili katika miongo ya hivi
karibuni iliyoandikwa na Prof. E. Dammann na utafiti wa istilahi za ukoo
wa Waswahili iliyoandikwa na A. H. J. Prinns. Pia jarida hilo lilichapisha
makala fupi iliyoitwa "Halmashauri ya Kiswahili ya Afrika Mashariki"
iliyoandikwa na Shaaban Robert wa Tanganyika. Mwandishi anasema
kwamba Kiswahili kiliondolewa katika vyuo vya Uganda. Pia anatoa hoja
kwamba Wakenya walikuwa wakisomesha Kilatini badala ya Kiswahili
katika vyuo vyao. Ni wazi, hata ingawa Shaaban Robert hakuthibitisha
hoja yake, kwamba watawala wa kikoloni walikuwa tayari wameanza
kupunguza matumizi ya Kiswahili katika vituo vya elimu.

Kwa mara ya kwanza, tunafahamishwa kwamba kamati ilikuwa
ikikadiria mitihani ya Kiswahili ya watahini wa Chuo Kikuu cha
Cambridge. Kamati ilikuwa ikiwashauri kuhusu muundo na kupendekeza
vitabu vya lazima.

Katika Jarida, EASC Journal Na. 27 la 1957, katibu, W. H. Whiteley,
anaalika maoni na mchangio kwa nyongeza ya kamusi ya Kiswahili sanifu.
Yaonekana hamu ya wanakamati kuendelea na shughuli zao ilikuwa
imeanza kufifia kwa kuwa tawala za kikoloni za Afrika Mashariki

--
31* Mabadiliko ya sera ya lugha yaliyojadiliwa katika sura ya nne hayakuiwezesha Kamati
kutimiza lengo hili.

64

hazikuonyesha shukrani bali ziliipuuza Kamati. Alipokuwa akiwapa
moyo na kuwahimiza waandike kamusi, Whiteley aliongeza kusema
yafuatayo:

"Hata ingawa kazi ya kutayarisha kamusi ya Kiswahili-Kiingereza
imekaribia kwisha idadi ya maoni tuliyoyapata ni ndogo kuliko
ilivyotumainiwa. Je, yawezekana wazungumzaji wa Kiswahili wakose
mapenzi kwa lugha yao kiasi cha kwamba kazi muhimu kama hii
inapita bila wao kujali? Ama ni wanakamati - ambao Kamati yote
hutegemea - ambao wamekosa hamu ambayo wanatarajiwa kuo-
nyesha?

Yeyote mwenye ulegevu huu wa kutojali asijiliwaze kwa kuamini
kwamba hii ni kazi ya kitaaluma tu ambayo haina umuhimu wa
kufaa. Mahitaji ya kuwasiliana vya kutosha tayari yamedhihirishwa
kwa ukatili nchini Kenya kwa muda wa miaka minne iliyopita, na ni
ujinga kudhania kwamba Kiswahili hakina matatizo kama hayo." 32*
(EASC Journal Na. 27, 1957: 6).

Tabia ya kutojali Kiswahili ya serikali za kikoloni za Afrika Mashariki
na ulegevu wa wanakamati ulianza kudhuru moyo wa kufanya kazi wa
maafisa wa Kamati. Pia katika jarida hilo hilo la 1957, mchunguzi msaidizi
Bwana O. B. Kopoka anaripotiwa kuwa amehuzunishwa sana kwa kuwa
wanakamati hawaonyeshi kupendezwa na kazi yake kuhusu sarufi ya
Kiswahili. Kutokana na uchunguzi wa Bwana Kopoka tayari vitabu viwili
vya sarufi - Miao na Matendo vilikuwa vimechapishwa. Baadaye,
mwaka 1959 Bwana Kopoka alijiuzulu kazi ya mchunguzi msaidizi na
akaanza kufanya kazi na Kampuni ya Shell. Baada ya kujiuzulu huko,
Kamati ilisimamisha kazi za uchunguzi wa sarufi. Pia, katika jarida la
Kamati Na. 30 la 1959, tunajulishwa kwamba kamati imesikitishwa kwa
kufahamishwa kwamba serikali ya Tanganyika haihitaji tena sarufi na
kwamba haitaki kazi aliyoifanya Bwana Kopoka (uk. 19).

Katika mwaka 1958, kamati ilieleza kusikitishwa kwake na idadi ndogo
ya Waafrika waliokuwa wakinunua jarida. Huku kukiwa na wanunuzi
kutoka sehemu kadha za Ulaya, hakukuwa hata na mtu mmoja aliye-
linunua kutoka Zanzibar. Ingawa hivyo, kwa jumla, idadi ya wanunuzi
ilikuwa ikiongezeka kutoka 350 mwaka 1952, kufikia 600 mwaka 1958.
Kuanzia mwaka 1958 ilikatwa shauri kuchapisha jarida mara mbili kwa
mwaka kwa sababu ya kuongezeka kwa makala za kuchapishwa.

Suala la ununuzi wa majarida lilizuka tena mwaka mmoja baadaye.

--
32* Ni dhahiri kwamba sentensi ya mwisho inazungumzia juu ya hali ya hatari nchini Kenya.
Serikali ya kikoloni ya Kenya iliona wazi kwamba haikuwa na ujuzi wa lugha wa kutosha
kupenya njama za Mau Mau kwa kutumia Kikikuyu, Kimeru au Kiembu.

65

Katika maoni ya mwandishi wa Jarida la Kamati - EASC Journal
Na. 29/1 la 1959, Whiteley alitaja kwamba hakukuwa na Mhindi au
Mwafrika yeyote aliyekuwa akilinunua hata ingawa makala kadha katika
kila toleo pamoja na vitabu vyote vya ziada vilikuwa vikitarajiwa
kusomwa na Waafrika. Whiteley analaumu ukosefu wa njia bora za
usambazaji majarida. Ni wazi pia kwamba, tatizo hili pia lilisababishwa na
kutotangazwa vyema kwa shughuli za Kamati na Kamati yenyewe haiwezi
kujiepusha na lawama hii. Katika kurasa zingine za jarida hilo imetajwa
kwamba, wakiwa katika shughuli za kufanya uchunguzi wa Kihadimu,
Kitumbatu na Kipemba huko Zanzibar na Pemba, Kamati ilisikitika
kuona kwamba watu wa Zanzibar na Pemba hawakujua kuwepo kwa
Kamati hii.

Katika mkutano wa kila mwaka wa 1957, Kamati ilionyesha wasiwasi na
masikitiko yake kuhusu kiwango cha chini cha Kiswahili kilichokuwa
kikitumika katika vipindi vya idhaa mpya ya Kiswahili ya B.B.C.

Jarida la 1958 - EASC Journal Na. 28 limechapisha makala ya
mfululizo wa mihadhara mitano ya kila mwezi iliyotolewa Tanga kwa
kudhaminiwa na "Jumuia ya Taaluma ya Kiswahili" ya Tanga. Sehemu ya
pili ya makala ya Prinns kuhusu istilahi za ukoo wa Waswahili pamoja na
majina ya Kiswahili ya samaki wa baharini pia yamechapishwa katika
toleo hilo.

Kwenye mkutano wa kila mwaka wa Septemba 1958, wazo la kuanzishwa
kwa kamati ya ukusanyaji, uhariri na uchapishaji wa makala za kihistoria
ulijadiliwa. Iliripotiwa katika mkutano huo kwamba Liwali wa Pwani,
Kenya, Sheikh Mbarak Ali El Hinawy angekuwa radhi kuwa mwenyekiti wa
kamati hiyo. Hata hivyo Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ilikuwa
na wasiwasi. Whiteley anatahadharisha kwamba "bila shaka familia
nyingi zinashuku kwamba Wazungu wataitumia miswada yao kwa njia
mbaya".

Hofu za Waswahili zilikuwa na msingi kwa sababu hata ingawa
Wazungu walihifadhi miswada hiyo, wengine, kama vile Jan Knappert,
wameichapisha baadhi ya miswada hiyo kuwa vitabu ghali sana huko
Ulaya. Vitabu hivyo havipatikani Afrika Mashariki na hata vikipatikana
ni ghali sana hivi kwamba wenye miswada hawawezi kupata pesa za
kuvinunua licha ya kuwa baadhi yao walilipwa pesa kidogo na wengine
hawakulipwa chochote kwa miswada yao. 33*

--
33* Mifano ya vitabu vya Jan Knappert ambavyo Mswahili wa kawaida hawezi kuvigharamia
ni pamoja na vitabu vya mashairi ya kiislamu Swahili Islamic Poetry vilivyochapishwa na E.
J. Brill, huko Leiden, Netherlands mwaka 1971, na kitabu chenye tenzi za karne nne: Four
Centuries of Swahili Verse: A Literary History and Anthology chenye kurasa 323 kilicho-
chapishwa London na Heinemann mwaka 1979.

66

Mpango ungefanywa ili miswada kama hiyo ichapishwe na Kamati ya
Kiswahili ya Afrika Mashariki. Pesa ambazo zingepatikana kutokana na
kuuzwa kwa vitabu vilivyochapisha zingewekwa kwenye wakfu ambao
ungetumiwa kuwanufaisha Waswahili kwa njia kama vile kugharamia
masomo ya juu ya watoto wao, kugharamia uchunguzi zaidi, au kwa
huduma za jamii. Kamati ilijua wazi kwamba Waswahili hawakuwa tayari
kupeana miswada yao, na hiyo ndiyo sababu walihitaji msaada wa watu
mashuhuri wa pwani kama vile Liwali Sheikh Mbarak Ali el Hinawy.

Kamati ya kihistoria iliundwa. Ilikutana kwa mara ya kwanza tarehe 27
Juni 1959. Wafuatao walihudhuria:
1) Sheikh Mbarak Ali El Hinawy.
2) Bwana J. S. Kirkman wa Mombasa.
3) Bwana J. W. T. Allen - Katibu mtendaji wa Kamati ya
Kiswahili ya Afrika Mashariki.
4) Bwana Shihabuddin Chiraghdin - wa Mombasa.
5) Sheikh Hyder Mohammed El Kindy - wa Mombasa ambaye
alikuwa katibu wa hii kamati ndogo.

Wanachama wafuatao wa hiyo kamati waliomba radhi kwa kutoweza
kuhudhuria.
1) Sir John Grey wa Zanzibar.
2) Sir Said bin Ali Mugheiry wa Pemba.
3) Dkt. G. S. P. Freeman-Grenville wa Mafia.
4) Sheikh Muhammad Kassim Mazrui wa Malindi.
5) Sheikh Mohammed bin Ali bin Hamed Buhry wa Tanga.

Kamati hiyo ilipewa jukumu la kukusanya miswada mingi ya kihistoria
iwezekanavyo. Ilikubaliwa kwamba makala na miswada yote itakayo-
kusanywa atapelekewa katibu katika chuo cha Makerere. Katibu ali-
takikana kuiorodhesha na kuipa nambari miswada hiyo na ikiwezekana
angeinakili na kuipeleka nakala moja kwa mwenyekiti na nyingine kwa
mwenye mswada kama shukrani kwa ushirikiano wake - (Tazama:
EASC Journal Na. 30, 1959: 13). Yaonekana kwamba suala la mwenye
haki za kunakili na kuchapisha miswada na makala hayo halikushughu-
likiwa.

Zaidi ya hayo, Kamati iliamua kuchunguza uwezekano wa kupiga picha
ndogo (microfilm) maandishi ya kale yaliyokuwa katika hifadhi za
Makerere na Mombasa. Katibu aliombwa kutafuta msaada wa pesa
kutoka kwa mashirika ya kutoa misaada ili kuwezesha ukusanyaji wa
miswada. Kiasi fulani cha pesa kilitumiwa kununua miswada kutoka kwa
watu ambao hawakuwa tayari kuitoa bure.

Ripoti ya mkutano wa 21 wa kila mwaka uliokuwepo kati ya tarehe 10
na 13 Septemba 1958 huko Tanga, Tanganyika, imechapishwa katika

67

jarida Na. 28/1 la 1958. Kamati ilijadili hali ya baadaye ya Kamati kwa vile
kushirikishwa kwake kwenye Taasisi ya Uchunguzi wa Shughuli za Jamii
ya Afrika Mashariki katika Chuo cha Makerere kwa kipindi cha miaka
mitano kungemalizika mwisho wa mwaka wa masomo wa 1959/60.
Wakati huo Taasisi ilikuwa ikigharamia nusu ya mshahara wa katibu na
hakukuwa na uhakika ikiwa pesa zingepatikana na kuigharamia kamati
baada ya hapo. Wanachama wa Kamati walikubaliana kuonyesha
umuhimu wa Kamati kwa serikali zao ili kuiwezesha Kamati kupata pesa
baada ya kwisha kwa muda wa kuwa kwenye Taasisi. Makisio mapya ya
kuigharamia kamati yalipelekewa serikali (zote) ili kufikiriwa.

Kufikia wakati wa mkutano uliofuata wa kila mwaka kati ya tarehe 9 na
11 Septemba huko Mombasa, serikali za Afrika Mashariki zilikuwa bado
hazijajibu ombi la Kamati. Kwa hivyo Kamati haikuwa na uhakika iwapo
wangepata pesa ambazo walikuwa wameomba. Ilionekana kwamba
Kamati zaidi ilikuwa chombo cha uchunguzi ambacho kingegharamiwa
na serikali mpaka kitakapojiunga vizuri na Chuo Kikuu.

Katika ripoti ya kila mwaka ya 1958 - 1959 iliyochapishwa kwenye
EASC Journal Na. 30 la 1959, katibu mpya J. W. T. Allen anaeleza
kwamba Kamati ilipata shida kubwa za kiidara kwa sababu ya kuondoka
kwa katibu W. H. Whiteley, msaidizi wake Bi. Fawler na Bwana O. B.
Kopoka. Pia anaripoti kwamba hakukuwa na matumaini ya kupata pesa
zingine kutoka kwa serikali. Ilibidi Kamati ipunguze gharama zake kwa
kuajiri makarani wa muda inapowezekana na kwa kuhamisha ofisi za
Kamati hadi University Hall ambapo Allen alikuwa akifanya kazi ya
mlinzi. Ilibidi maktaba ya Kamati iwekwe amana katika maktaba ya Chuo
Kikuu cha Makerere kwa sababu ya kukosa chumba kulikosababishwa na
ukosefu wa pesa.

Uamuzi wa kupunguza matumizi zaidi. ulifikiwa katika mkutano wa kila
mwaka uliokuwepo kati va tarehe 4 na 5 Septemba 1959. Katika mkutano
huo, Kamati ilikata shauri kutochapisha vitabu vya ziada tena kwa sababu
ya gharama kubwa ya uchapishaji. Kwa bahati nzuri Kamati ilikuwa na
ushirikiano bora na East African Literature Bureau na mkurugenzi wake,
C. G. Richards, alikuwa amehudhuria mkutano huo. Badala ya vitabu
hivyo vya ziada ya majarida, East African Literature Bureau ilikubali
kuanza kuchapisha mfululizo wa vitabu wenye kujulikana kama Johari za
Kiswahili. Wangeanza kuchapisha vitabu viwili viwili kila mwaka.
Ilikubaliwa pia kwamba vitabu vya kwanza vya Johari za Kiswahili
ambavyo vingechapishwa na Kamati kama vitabu vya ziada ya majarida
vitakuwa:
1) Utenzi wa Vita vya Wadachi.
2) Utenzi wa Abdirrahmani na Sufiyani.

68

3) Utenzi wa Uhud.
4) Utenzi wa Seyyida Hussein bin Ali. 34*

Mkurugenzi wa East African Literature Bureau pia alikubali kuchapisha
toleo jipya la kitabu kilichosahihishwa cha Tippu Tip.

Kufikia mwaka 1959 vitabu vifuatavyo vya uchunguzi wa lahaja za
Kiswahili vilikuwa tayari vimechapishwa na Kamati ya Kiswahili ya
Afrika Mashariki:
1) Ki-Mtang'ata - A Dialect of Mrima Coast na W. H. Whiteley,
1956.
2) Ki- Vumba - A Dialect of the Southern Kenya Coast na H. E.
Lambert, 1957.
3) Chi-Jomvu and Ki-Ngare - Sub dialects of the Mombasa
Area na H. E. Lambert, 1958.
4) The Dialects and Verse of Pemba - An Introduction na W. H.
Whiteley 1958.
5) Chi-Chifundi - A Dialect of The Southern Kenya Coast na
H. E. Lambert 1958.

Kwa sababu ya matatizo ya kipesa ya Kamati, Allen aliandika maoni ya
mhariri ya EASC Journal Na. 30 la 1959 na kutishia kwamba Kamati ya
Kiswahili ya Afrika Mashariki haingeweza kuendelea kufanya kazi yake
kikatiba. "Ni lazima ipanuke, iwe kitu kikubwa au ikomeshe jitihada za
kuendelea", akaandika. Anailaumu nia mbaya ya kikoloni ya kupuuza na
kutojali Kiswahili kwa kusababisha mashaka hayo ya Kamati. 35*

Allen anaeleza kwamba Kamati ni kama mji uliozingirwa. Ikikoma
kujitahidi itapoteza kile kilichochukua miaka mingi ya kazi ngumu
kukipata. Lingine la kufanya ni kwa kamati kuvumilia kuendelea na
kutumaini kwamba watapata mwokozi. Kamati ilikuwa katika hali ya
kukata tamaa, na Allen alijitahidi juu chini kutafuta msaada wa pesa
kutoka kwa mashirika ya kutoa misaada.

Kwenye mkutano wa Kamati wa kila mwaka uliokuwepo mwezi
Septemba 1959 Kamati ilijulishwa kwamba Chuo Kikuu cha Makerere
kilikuwa kimependekeza kuundwa kwa kamati ya chuo ya kushughulikia
somo la Kiswahili. Kamati hiyo ingetoa mapendekezo yake kwa Kamati
ya Kiswahili ya Afrika Mashariki.

Baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo, Kamati ilikubali pendekezo la
kamati ya chuo kikuu la kuanzishwa kwa Taasisi ya Uchunguzi wa
Kiswahili. Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ilikubali pendekezo
hilo hata ingawa ilielewa wazi kwamba kuendelea kwa "Kamati kungeishia

--
34* Majina kamili, pamoja na watunzi au waandishi na wahariri yapatikana katika bibliografia.
35* Tazama sehemu ya kubadili sera dhidi ya Kiswahili katika sura ya Tano ambapo Allen
amenukuliwa kwa kireru.

69

kwenye mwanzo wa kipindi kipya cha miaka mitano (au mapema zaidi)".
Kamati vilevile ilipendekeza kwamba, kamati ya chuo ihakikishe kwamba
washauri wenye ujuzi wa isimu, elimu jamii na historia wanashirikishwa
katika kuanzishwa kwa taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili. Kamati vile
vile ilitaraji kwamba, serikali za Kenya, Uganda, Tanganyika na Zanzibar
zitaendelea kuisaidia Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili kifedha ikiwa
Makerere au ikihamia katika chuo kikuu kingine.

Makala kuu zilizochapishwa mwakawa 1960 (EASC Journal Na. 31) ni
pamoja na sehemu ya pili ya makala ya Sir John Gray kuhusu historia ya
Zanzibar, sehemu ya pili ya makala ya W. H. Whiteley kuhusu lahaja ya
Zanzibar mashambani na makala ya Mwidani bin Mwidadi iliyohaririwa
na Lyndon Harries kuhusu kuanzishwa kwa mji wa Rabai. (Sehemu za
kwanza za makala ya Sir John Gray na W. H. Whiteley zilichapishwa
katika EASC Journal Na. 30 la 1959.) Mjadala wa matumizi ya Kiswahili
nchini Zaire, Rwanda na Burundi ulioandikwa na Hamis Kitumboy na
makala ya B. Lecoste kuhusu sarufi ya Kiswahili cha Kongo ya Ubelgiji
(Zaire) yalichapishwa pia katika jarida hilo la 1960.

Mnamo tarehe 23 Mei 1961 ilitangazwa huko Makerere kwamba Wakfu
wa Calouste Gulbenkian ya Lisbon umetoa msaada wa pauni elfu tisa
(?9000) na kwamba kiasi kama hicho kitatolewa na Hazina ya Maendeleo
ya Makoloni. Pesa hizo zilitolewa kugharamia mchunguzi mmoja na
wasaidizi wake kwa miaka mitatu pamoja na usafiri na gharama zingine ili
kukiwezesha Chuo Kikuu cha Makerere kianzishe Taasisi ya Uchunguzi
wa Kiswahili.

Ripoti hiyo iliyotolewa kwa magazeti pia inaeleza kwamba Afrika
Mashariki pamoja na Kongo (Zaire), wana lugha moja kuu ya mawasiliano
ambayo hueleweka kwa urahisi na Waafrika wa eneo hilo, kwa sababu
imefanana sana na lugha zao. Inapendekezwa kwamba chuo au taasisi ya
uchunguzi wa Kiswahili ianzishwe kwa kupanua kazi za Kamati ya
Kiswahili ya Afrika Mashariki ili kukuza uchunguzi katika lugha ya
Kiswahili. Pia inaelezwa kwamba serikali za Afrika Mashariki zingeendelea
kugharamia shughuli za kiidara ili pesa zilizotolewa zitumike zaidi katika
shughuli za uchunguzi.

70

Sura ya Tano

5.0 Kiswahili na sera ya lugha

5.1 Kiswahili na sera ya lugha nchini Uganda

Historia ya maendeleo na usanifishaji wa Kiswahili pamoja na shughuli
za Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki hugusia zaidi vile hali
ilivyokuwa Tanzania na Kenya kuliko Uganda. Labda sababu yake ni
kwamba Kiswahili hakikupewa nafasi ya kuenea huko kama kilivyoenea
Kenya na Tanzania. Wabaganda walipinga kusomeshwa kwa Kiswahili
katika shule zao wakati ambapo serikali ya kikoloni ilikuwa tayari kukuza
Kiswahili. Wakati sera ya lugha ilipobadilika dhidi ya Kiswahili kote
katika Afrika Mashariki kuanzia muongo wa 1950 Kiswahili kiliondolewa
shuleni kwa kuwa hakikuwa tena lugha iliyotambulika kusomeshwa
nchini Uganda. Kabla sijayajadili mabadiliko ya sera ya lugha dhidi ya
Kiswahili, kwanza nitaijadili sera ya lugha nchini Uganda, na vile
ilivyokuwa ikibadilikabadilika, kufikia wakati Kiswahili kilipoondolewa
shuleni.

Kuanzia mwaka wa 1925 suala la ni lugha zipi za Kiafrika zitakazo-
tumika kusomesha katika madarasa ya mwanzo ya shule za msingi kote
nchini Uganda, lilijadiliwa na serikali ya kikoloni. Kwanza uamuzi
ulitolewa kwamba Kiluganda itumike katika eneo lote lililokuwa likitumia
lugha za Kibantu. Kisha kamati ikaundwa kuchagua lugha muafaka ya
kutumia katika eneo la Kinailoti la Mikoa ya Kaskazini na Mashariki.
Kamati hiyo pia ilitakikana kutayarisha tafsiri ya vitabu vya shule katika
lugha zilizochaguliwa. Kiingereza kingetumika kuanzia madarasa ya juu
ya shule za msingi na kuendelea.

Mwaka 1926 Idara ya Elimu iliamua kutumia lugha tatu za Kiafrika
katika shule za msingi.

Lugha hizo ni:
1) Kiluganda - iliyotumiwa Buganda na sehemu ya kaskazini ya
Mkoa wa Mashariki.
2) Kiacholi - iliyotumiwa katika Mkoa wa Kaskazini.
3) Kiateso - lugha iliyotumiwa katika shule za eneo la kati la
Mkoa wa Kati.

Lugha zingine zote za Kiafrika zilitambuliwa kuwa "lahaja ndogo"
ambazo hazingetumiwa ila katika shule za malezi. Kiwango hicho cha

71

elimu kilisemekana kwamba hakikuhitaji vitabu na kwamba wanafunzi
wengi hawakuendelea na masomo huko kwa kuwa walijiunga na shule za
msingi ambako wangetumia moja kati ya lugha tatu zilizochaguliwa. 36*

Kufikia 1927 vitabu kadha vilikuwa vimeandikwa kwa Kiluganda
lakini kulikuwa na matatizo katika zile lugha zingine mbili. Gavana
aliandika kumbukumbu kuhusu jambo hili, nalo baraza la kutoa mashauri
kuhusu elimu ya Waafrika likaijadili kwa kirefu. Matokeo yake ni
kwamba ilionekana muafaka Kiacholi na Kiateso zitumiwe kama lugha za
kusomesha katika shule za msingi zilizokuwa katika maeneo hayo tu (ya
Acholi na Teso). Ilikubaliwa kwamba Kiswahili kisomeshwe kama somo
katika shule za msingi na kwamba vitabu vya masomo kama vile afya,
jiografia na kilimo viandikwe kwa Kiswahili. 37*

Uamuzi wa kusomesha Kiswahili ulifikiwa kwa sababu ya matatizo
ambayo hayakuweza kutatuliwa wakati huo ya kutafsiri vitabu kwa lugha
za Kiateso na Kiacholi. Sababu nyingine kubwa pia ni ile athari
iliyotokana na kutumiwa kwa Kiswahili katika nchi jirani za Kenya,
Tanganyika na Zanzibar. Ripoti ya Idara ya Elimu ya Mwaka wa 1927
inaongeza kwamba "Aidha lugha hizi mbili si lugha za kwanza za watu
wengi walioko katika maeneo hayo, na kwao Kiswahili hakitakuwa shida
kukielewa kuliko Kiateso na Kiacholi" (uk. 10).

Kwa hivyo sera ya lugha iliruhusu kutumiwa kwa lugha za kwanza
kusomesha wanafunzi wote katika miaka miwili ya kwanza ya masomo
kiwango ambacho vitabu havikuhitajika sana. Baada ya kiwango hicho,
wanafunzi walianza kujifunza Kiswahili, lugha ambayo iliwawezesha
kusoma idadi kubwa ya vitabu ambavyo vilikuwa vikiongezeka kwa
wingi. Kiswahili kilitambuliwa kuwa lugha ya pekee ambayo ingerahisisha
mawasiliano katika nchi za Afrika Mashariki. Kilitambuliwa kuwa lugha
ya watu wengi ambayo ingetumiwa katika kuvichapisha vitabu vingi vya
shule na vya fasihi. Gavana Gowers aliyekuwa Gavana wa Uganda wakati
huo alikiunga mkono Kiswahili. Katika mwaka 1928 alipendekeza
Kiswahili kitumiwe badala ya Kiluganda kama lugha ya elimu na utawala
nchini Uganda (Ladefoged et. al. 1971: 88).

Sera hii ya kufunza lugha za kwanza zikifuatiwa na Kiswahili ilifuatwa
katika mikoa yote ya Uganda isipokuwa mkoa wa Buganda. Hapo
mwanzoni Kiswahili kilipingwa katika Mkoa wa Mashariki, lakini
baadaye kilikubalika kuliko Kiluganda ambayo ingetumiwa ikiwa
Kiswahili hakingetumika. Katika Mikoa ya Kaskazini na Magharibi
mabadiliko ya kuanza kutumia Kiswahili yalitajwa kuwa "yalipendwa

--
36* Education Department, Annual Report ya 1926 uk. 11.
37* Education Department, Annual Report ya 1927 uk. 10.

72

sana na watu wote". 38* Kwa sababu ya sera hii mpya ya lugha, vitabu vya
shule vilivyokuwa vikitumiwa Tanganyika vilianza kutumika katika shule
za Uganda kuanzia mwaka 1928. Pia Mkurugenzi wa Elimu nchini Uganda
alipendekeza kuanzishwa kwa shirika la kutafsiri vitabu vya Kiswahili ili
kuhudumia nchi za Kenya, Uganda, Tanganyika na Zanzibar.

Mwaka 1928 Ronald Snoxall alihamishwa kutoka Tanganyika kwenda
Uganda kama Msimamizi wa Elimu ya Msingi. Snoxall alikuwa na ujuzi
wa nchi ambayo ilikuwa ikitumia Kiswahili kama lugha ya kufunza katika
shule za msingi. Idara ya Elimu ya Uganda ilihitaji msaada wake katika
jaribio la kufuata sera ya lugha ya Tanganyika. 39* Vituo vya elimu
vilivyokuwa vikihudumia nchi nzima yaonekana viliunga mkono kwa
dhati sera mpya kuhusu Kiswahili. Shule ya Ufundi ya Kampala, kwa
mfano, iliamua kutofundisha Kiingereza. Badala ya Kiingereza, Kiswahili
kilifundishwa kwa kuwa ndicho lugha ya mawasiliano kote Afrika
Mashariki. Kama alivyosema mkuu wa shule hiyo, Bwana Savile, shule
hiyo ilikuwa ikihudumia nchi nzima pamoja na watu wenye kuzungumza
lugha zisizo za Kibantu ambao hawangeielewa Kiluganda.

Mwezi Januari 1928 chuo cha serikali cha kufunza walimu wa shule za
msingi kilianzishwa. Katika chuo hiki, Kiswahili kilitumiwa kama lugha
ya kusomeshea.

Katika ripoti yake ya 1928 mkuu wa chuo hicho, Kampala Normal
School, A. J. Lush, alisema kwamba mitihani ya Kiswahili ilionyesha
maendeleo ya kuridhisha katika mazungumzo na maandishi. Mwalimu wa
Kiswahili, Sheikh Abdul Rahman Mahomet, aliajiriwa kutoka Zanzibar
mwaka huo wa 1928. Mwezi Februari 1929 mkuu wa chuo pamoja na
wanafunzi wake sita walitembelea Mombasa ambako walijifunza Kiswahili
kwa muda wa miezi mitatu.

Matumizi ya Kiswahili yalikuwa yakienea vizuri kote nchini Uganda
mwaka 1929 isipokuwa Buganda. Wanafunzi wa Uganda kutoka shule za
serikali na za misheni walipelekwa Mombasa, Kabaa na Zanzibar ili
kupewa mafunzo ya Kiswahili. Vilevile Kiswahili kilifunzwa kwa mafanikio
katika chuo cha walimu cha misheni ya C.M.S. Mukono na chuo cha
walimu cha misheni ya White Fathers, Bikira. Katika vyuo kadha
Kiswahili kilifunzwa badala ya Kiingereza.

Urahisi wa Mwafrika kujifunza lugha nyingine ya Kiafrika badala ya
Kiingereza ulitambuliwa. Kiswahili kilionekana kwamba kinafaa kuliko
lugha zingine za Kiafrika kwa sababu kulikuwa na vitabu vingi vilivyo-
andikwa kwa Kiswahili. Haingewezekana kuchapisha vitabu vyote

--
38* Education Department, Annual Report 1928 uk. 9.
39* Education Department, Annual Report ya 1928 uk. 6.

73

vinavyohitajika shuleni katika lugha nyingi za Kiafrika kwa sababu ya
gharama ya kuchapisha nakala chache kwa kila lugha. Vitabu vya
Kiswahili viliuzwa kwa wingi nchini Uganda. Kuanzishwa kwa kamati ya
Kiswahili ya Afrika Mashariki kulikuwa kunangojewa kwa hamu nchini
Uganda kwa kuwa kungesaidia kuchapishwa kwa vitabu vingi vya
Kiswahili.

Ripoti ya maendeleo ya misheni ya C.M.S. ya Elgon inaonyesha
kwamba walianza kufunza Kiswahili kwa mara ya kwanza mwaka 1929.
Baadhi ya walimu na wanafunzi wa chuo cha walimu cha misheni hiyo
walipelekwa Mombasa kufunzwa Kiswahili ili wasaidie katika kuanzishwa
kwa somo la Kiswahili. 40* Wakati huo huo, Katibu wa Elimu wa shule za
misheni Katoliki ya Mataliani, W. Gotta alitoa ripoti kwamba hata
ingawa Kiswahili kilikuwa somo jipya, kilipokelewa vizuri katika madarasa
ya shule za msingi na vyuo vya walimu katika eneo la Gulu. Baadhi ya
shule za msingi za Gulu, Kitgum, Moyo, Ama na Ngal zilikuwa na
matatizo ya kusomesha Kiswahili. Lakini iliripotiwa kwamba masista
wote waliokuwa wakiongoza shule hizo walikuwa tayari wamekwenda
Dar es Salaam ili kujifunza Kiswahili.

Ripoti ya Koloni ya Uganda ya mwaka 1929 inasema yafuatayo kuhusu
maendeleo ya Kiswahili:

"Ufunzaji wa Kiswahili tayari umeanzishwa katika Mkoa wa Masha-
riki na maendeleo mazuri yamepatikana. Lugha hii itasomeshwa
kote katika vyuo vya kufunza walimu wa shule za vijijini isipokuwa
Buganda. Vitabu vilivyoko, ambavyo vimekusudiwa kutumiwa na
makabila ya Afrika Mashariki yanayojua Kiswahili havifai kwa
makabila ya bara ambao wanaanza kujifunza lugha hiyo; utayarishaji
wa vitabu vinavyofaa zaidi yafaa iwe kazi ya kwanza ya Kamati
mpya ya Kiswahili ya Afrika Mashariki." 41*

Juhudi za kueneza ufunzaji wa Kiswahili nchini Uganda zilivuma
mwaka 1930 wakati mradi mahsusi wa kufunza walimu wa vijijini kwa
miaka miwili ulipoanzisha vituo 29 kote katika Mikoa ya Mashariki,
Kaskazini na Magharibi. Masomo yaliyokuwa yakifunzwa ni dini, kilimo,
mbinu za kufunza, afya na Kiswahili. Ufunzaji wa Kiswahili ulinuiwa
kuhakikisha kwamba walimu wa gredi C watakaofaulu watakuwa wame-
jiandaa vya kutosha kusitawisha ufunzaji wa Kiswahili katika shule zao.
Wawakilishi wawili wa serikali na wengine wawili wa misheni waliwakilisha
Uganda kwenye mkutano wa kwanza wa kamati ya Kiswahili ya Afrika
Mashariki uliokuwepo Nairobi mwezi Aprili 1930.

--
40* Education Department, Annual Report ya 1929 uk. 31.
41* Uganda Annual Colonial Reports: Annual Report 1929, uk. 31, London, 1930.

74

Sera hii ya kueneza Kiswahili iliendelezwa na misheni mwaka wa 1930.
Misheni ya C.M.S. iliripoti kuenea kwa matumizi ya Kiswahili bora.
Misheni ya White Fathers iliwafunza Kiswahili walimu wa zamani kumi
na watatu ili wahitimu kuwa walimu wa kudumu. Katibu wa Elimu wa
misheni ya White Fathers, C. Robbiard alisema kwamba ni rahisi sana
kwa Mwafrika kujifunza lugha nyingine ya Kiafrika hivi kwamba baadhi
ya walimu wao walijifunza wenyewe. 42*

Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki ilikutana Makerere Uganda
mwezi Aprili 1931 kwa mara ya kwanza. Katika mkutano huo kazi
muhimu ilikamilishwa kuhusu usanifishaji wa uandikaji wa maneno ya
Kiswahili yaliyoazimwa kutoka lugha za kigeni.

Mwezi Juni 1931 Baraza la Kutoa Mashauri Kuhusu Elimu ya Waafrika
lilikutana na kutoa maoni kwamba Kiluganda iendelee kuwa lugha ya
kusomesha masomo mengine katika Mkoa wa Buganda na kwamba
Wabaganda wakipenda wanaweza kuanzisha somo la Kiswahili. Pia
shauri ilikatwa kwamba walimu wa vyuo vya walimu vya serikali
wafunzwe ili kusomesha Kiswahili katika shule ya King's African Rifles
(KAR), shule za polisi, na shule zingine za msingi zilizoko kwenye maeneo
yenye lugha tofauti. Baraza hilo la kutoa mashauri pia lilisema kwamba:

"Vyuo vya walimu vya misheni vinavyopata ruzuku vya Nabumali,
Ngora, Arua, na Gulu lazima vifunze Kiswahili kwa wanafunzi
wanaosomea huko. Kwamba katika maeneo yenye mchanganyiko
wa lugha, Kiswahili kisomeshwe kama somo la shule za msingi mara
tu walimu wanapopatikana kutoka vyuo hivyo, lakini lugha za
kwanza za maeneo hayo ziendelee kuwa lugha za kufundishia.
Kwamba, Kiswahili kisomeshwe katika chuo cha ufundi cha serikali
ambacho kitasomesha vijana kutoka kote nchini." 43*

Pingamizi ya kwanza kubwa dhidi ya Kiswahili ilianza mwezi Septemba
1931 wakati maaskofu wa misheni nne za Church Missionary Societies,
pamoja na Kabaka wa wakati huo, Sir Daudi Chwa, walipomkabidhi
Waziri wa Nchi anayesimamia Makoloni (ya Uingereza) kumbukumbu
kulalamika dhidi ya kutumiwa kwa Kiswahili kama lugha ya pekee ya
kusomesha masomo mengine katika shule za msingi. Nilipomhoji Ronald
Snoxall alikiri kwamba karibu wahubiri wote wa Church Missionary
Society (C.M.S.) walikuwa Wabaganda waliotaka kueneza lugha yao ya
Kiluganda. Walitoa madai ya uwongo kwamba watu wote nchini Uganda
walifahamu Kiluganda. Katika kumbukumbu yao, maaskofu pamoja na
Kabaka walidai kwamba watu walikuwa wakilazimishwa kujifunza

--
42* Uganda Annual Colonial Reports. Annual Report ya 1929 uk. 31, London, 1930.
43* Education Department, Annual Report ya 1931, uk. 6.

75

Kiswahili kinyume cha kupenda kwao. Dai hili halikuwa la kweli. Sera ya
lugha ya Gavana Sir William Gowers ilihimiza Kiswahili katika maeneo
yenye mchanganyiko wa lugha yaliyokuwa nje ya Buganda. Kwa sababu
ya pingamizi hii dhidi ya Kiswahili wamisheni wengi walikosa hamu ya
kujifunza lugha hii.

Jibu la Idara ya Elimu lilisema kwamba kumbukumbu hiyo ilitokana na
kutoielewa sera ya serikali ya kutumiwa kwa lugha za kwanza katika
madarasa mawili ya kwanza ya shule za msingi na kutumiwa kwa lugha
hizo za kwanza pamoja na Kiswahili kama lugha za kusomesha masomo
mengine katika madarasa mawili yafuatiayo. Kumbukumbu haikutaka
Uganda itumie Kiswahili kama lugha ya mawasiliano kama nchi zingine za
Afrika Mashariki kwa kuwa walitaka lugha ya Uganda (bila shaka -
Kiluganda), iwe lugha ya mawasiliano nchini Uganda. Waganda, na zaidi
Wabaganda, waliogopa na kwa hivyo hawakutaka kuanzishwa kwa
shirikisho la Afrika Mashariki (Tazama Ladefoged et al 1971: 89).

Mwaka 1932 suala la lugha ya kusomesha masomo mengine lilitatuliwa
na serikali iipoamua kwamba masomo yote isipokuwa hesabu (hisabati)
yasomeshwe kwa kutumia lugha za kwanza za maeneo mbalimbali. Somo
la hesabu lilisomeshwa kwa Kiswahili, lugha ambayo wakati huo ilikuwa
ikisomeshwa kama somo katika shule zote za msingi nje ya eneo la ufalme
wa Buganda na Wilaya ya Busoga. Ripoti ya mwaka ya Koloni, ya 1931,
ilionyesha kwamba Kiswahili kilikuwa kikianzishwa kwa utaratibu kama
lugha ya kusomesha masomo mengine katika madarasa mawili ya mwisho
ya shule za msingi katika wilaya zinazotumia lugha za Kinailoti. Katika
Wilaya za Kibantu, Kiswahili kilikuwa kikisomeshwa kama somo isipo-
kuwa katika Mkoa wa Buganda na Wilayani Busoga ambapo Kiluganda
ilikuwa ikitumiwa katika madarasa yote ya shule za msingi. Ripoti za
koloni za kila mwaka zilirudia habari hizi kati ya 1931 na 1936. Katika
mwaka 1937 Ripoti ya Mwaka ya Koloni ilitaja kwamba Kiswahili
kilisomeshwa kama somo katika madarasa mawili ya mwisho ya shule za
msingi. Haya yalikuwa mabadiliko, lakini mradi Kiswahili kiliendelea
kuwa katika ratiba ya masomo ni hakikisho kwamba kilikuwa kikienea
kama lugha ya mawasiliano nchini Uganda.

Ubora wa Kiswahili kikilinganishwa na Kiingereza ulitiliwa mkazo tena
na Bwana E. G. Morris, Mkurugenzi wa Elimu, katika Ripoti ya Mwaka
1932. Morris aliandika yafuatayo:

"Huku inapomchukua kijana hodari Mwafrika muda wa miezi sita tu
kujifunza lugha ili aweze kukisoma kitabu cha Kiswahili na kukielewa
barabara, ingemchukua angalau miaka sita ya kujifunza Kiingereza
kwa makini ili aweze kukielewa kitabu cha Kiingereza cha kiwango
sawa. Ni vigumu kuelewa vile watetezi wa Kiingereza wanavyotaraji

76

kusitawisha elimu ya Waafrika kwa kutumia lugha ya Ulaya kama
lugha ya kusomesha masomo mengine." 44*

(Inasikitisha kwamba baada ya zaidi ya nusu ya karne moja tangu
maneno hayo yaandikwe vile hali ilivyo siyo tu kwamba lugha hiyo ya
Ulaya ndiyo inasomesha bali Kiswahili kilichokuwa kikitetewa hata
hakisomeshwi kama somo katika shule za msingi nchini Uganda).

Katika "shule za kati" (shule ambazo zilitoa mafunzo ya kazi) lugha ya
kusomesha ilikuwa ama Kiluganda katika eneo la kifalme la Buganda na
Wilaya ya Busoga au Kiswahili katika sehemu zingine za Uganda.

Lugha ya kusomesha katika vyuo vya walimu vya serikali ilikuwa ni
Kiswahili. Ili kuonyesha vile ilivyokuwa rahisi kwa Waafrika kujifunza
Kiswahili E. G. Morris anatoa mfano wa Mwalimu Omwami Y. Kakoza
aliyeanza kujifunza mwezi Januari 1932 na ilipofika Septemba mwaka
huo alifaulu mtihani wa Lower Government Standard Examination kwa
kupata alama za juu zaidi - asilimia 89 1/2.

Mwaka 1934 Kamati Kuu ya Church Missionary Society ya Diocese ya
Elgon iliamua kwamba kuanzia wakati huo, masomo yote katika Chuo
cha Kidini na cha Walimu cha Bawalasi yatasomeshwa kwa Kiswahili. Pia
Kamati Kuu iliamua kutumia Kiswahili katika shule za msingi za misheni
zilizokuwa katika maeneo ya mchanganyiko wa lugha.

Mwaka 1935 mabadiliko yalifanywa kuhusu majina ya viwango tofauti
vya elimu. Badala ya shule za malezi, shule za msingi, shule za kati ya chini,
kati ya juu na sekondari ya chini, zote zilijulikana kama shule za msingi au
shule za sekondari. Kila kiwango kilikuwa cha miaka sita. Mkaguzi
wa shule za msingi katika mwaka huo wa 1935 alilalamika kwamba
kulikuwa na uhaba wa vitabu vya shule vilivyoandikwa kwa lugha za
kwanza zilizokuwa zikitumiwa kusomesha. Wakati huo huo kulikuwa na
ongezeko la vitabu vya Kiswahili, lugha ya mawasiliano nje ya Mkoa wa
Baganda na Wilaya ya Busoga. Serikali ilionyesha wasiwasi kuhusu
kushuka kwa kiwango cha Kiingereza mashuleni kwa sababu walimu
waliotarajiwa kukifundisha walikosa mazoezi baada ya kupelekwa kufanya
kazi vijijini. 45*

Mkutano wa kila mwaka wa Wakurugenzi wa Elimu wa Kenya,
Uganda, Tanganyika na Zanzibar ulikuwa Makerere katika Februari na
Machi 1936. Kati ya mambo waliyoafikiana ni kwamba kulikuwa na
umuhimu wa kuongeza vitabu vya Kiswahili. Hali ya Kiswahili nchini
Uganda ilitiliwa nguvu na mkutano wa kila mwaka wa Kamati ya
Kiswahili ya Afrika Mashariki uliokuwepo Makerere mwezi Februari

--
44* Education Department, Annual Report ya 1932 uk. 5.
45* Education Department, Annual Report ya 1935 uk. 43.

77

1936. Lugha ya kusomesha katika "shule za kati" zilizokuwa zikifunza
taaluma mbalimbali, zilizokuwa zikipewa ruzuku ya serikali, ilikuwa
Kiswahili, isipokuwa Buganda na Busoga. Katika kiwango hicho cha
shule, walimu Waganda wapatao 50 walikuwa wakifundisha zaidi ya
wanafunzi Waganda 700, kwa kutumia Kiswahili mwaka huo wa 1936.

Kulikuwa na washiriki 14 wa mashindano ya uandishi wa Kiswahili
kutoka Uganda. Saba kati yao walipata zawadi. Wanne kati ya wale
waliopewa zawadi walikuwa Wabaganda. 46*

Ripoti ya Koloni ya mwaka 1938 yaonyesha kwamba Kiswahili
kiliendelea kusomeshwa katika miaka miwili ya mwisho wa shule za
msingi katika Wilaya za Kinailoti. Pia Kiswahili kiliendelea kuwa somo
katika shule za Wilaya ya Kibantu isipokuwa katika Mkoa wa Buganda na
Wilaya ya Busoga.

Katika miaka ya vita, 1939-1945 shule zilitumiwa kutawanya taarifa za
vita zilizoandikwa katika lugha nne, ambazo ni Kiingereza, Kiswahili,
Kiluganda na Kigujerati. Habari hizo zilikusudiwa kubatilisha uvumi na
propaganda. Mwaka 1942 Halmashauri ya Elimu ya Wanajeshi ya Afrika
Mashariki (East African Army Education Corps) ilianzishwa. Moja kati
ya madhumuni yake ilikuwa ni kupunguza matatizo ya mawasiliano kwa
kufunza wanajeshi Waafrika Kiingereza na kuwafunza wanajeshi Wazungu
ama Kiswahili, Chinyanja au Kisomali.

Mkutano uliitishwa Makerere mwezi Oktoba 1944 kujadili kumbu-
kumbu ya lugha katika shule za kuelimisha Waafrika iliyotolewa na
Kamati ya Kutoa Mashauri ya Elimu Katika Makoloni. Maoni ya
mkutano huo yalikuwa kwamba "Kiingereza pekee ndicho kilistahili
kutambuliwa kuwa lugha ya baadaye ya mawasiliano". 47* Hata hivyo
mkutano huo haukutetea kutumiwa kwa Kiingereza katika shule za
Buganda. Ulipendekeza kwamba muda wa kusomesha Kiingereza uonge-
zwe na kwamba lugha za kwanza zilistahili kusomeshwa kwa makini zaidi
kote katika vyuo na vituo mbalimbali. Lugha zilizochaguliwa kusomeshwa
hivyo, zilikuwa Kiluganda, Kirunyoro-Rutooro, Kiacholi (Kijaluo cha
Kaskazini), Kiateso na Kilugbara. Haya yalikuwa mabadiliko makubwa
ya sera. Kufikia mwaka 1944 sera ya lugha ilikuwa ikihimiza Kiswahili na
lugha za kwanza. Sera mpya ilihimiza Kiingereza na lugha za kwanza.
Haikutoa nafasi ya kusomeshwa kwa Kiswahili katika elimu ya Uganda. 48*

--
46* Education Department, Annual Report ya 1937 uk. 6.
47* Education Department, Annual Report ya 1944, uk. 7.
48* Uganda iliendelea kuwakilishwa katika Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki katika
miaka yake yote 1930-1964. Kati ya 1945 na 1946 Wakurugenzi wa Elimu wa Afrika
Mashariki walikuwa na mikutano ya kujadili suala la kuanzishwa kwa kampuni ya uchapishaji
wa vitabu katika chuo kikuu cha Halmashauri ya Fasihi na Lugha ya Afrika Mashariki
ambayo baadaye ilikuwa East African Literature Bureau.

78

Kutiliwa mkazo kwa lugha za kwanza katika shule za msingi haku-
kufurahiwa hasa huko Buganda. Afisa wa Elimu wa Mkoa alisema
kwamba:

"Labda jambo lililozusha ubishi mwingi sana kati ya walimu na shule
za msingi lilikuwa ni kuondolewa kwa Kiingereza kuwa lugha ya
kusomesha masomo mengine katika shule za msingi na kutahiniwa
kwa mitihani yote ya mwisho wa mwaka kwa lugha za kwanza.
Mabadiliko haya hayajatekelezwa vizuri." 49*

Mwaka 1946 Kiswahili kiliendelea kusomeshwa katika shule za msingi
za maeneo ambayo yalitaka kisomeshwe. 50* Ripoti ya mwaka 1948
inaonyesha kwamba lugha sita za Kiafrika zilikuwa zimekubaliwa kuwa
lugha za kusomesha katika shule za msingi. Lugha hizo sita ni Kiluganda,
Kirunyoro-Rutooro, Kijaluo cha Kaskazini, Kiateso, Kilugbara na
Kiswahili (Ladefoged et. al. 1971: 91).

Mwaka 1949 Kiswahili kilikuwa kikitumiwa kama lugha ya kusomesha
masomo mengine katika shule mbili tu (za pekee) za serikali, za watoto wa
askari polisi na askari wa magereza. Hii ni kwa sababu Kiswahili
kiliendelea kuwa lugha ya mawasiliano ya majeshi. Katika shule zingine
zote, watoto walisomeshwa kwa lugha zao za kwanza kufikia darasa la
nne. Lugha zingine tano za Kiafrika zilizotambuliwa zilibaki Kiluganda,
Kirunyoro-Rutooro, Kiacholi au Kijaluo cha Kaskazini, Kiateso na
Kilugbara. Lugha zingine za kwanza zingetumika katika madarasa mawili
ya kwanza ya shule za msingi.

Kiingereza hakikutumiwa kama lugha ya kusomesha masomo mengine
katika shule za msingi isipokuwa katika sehemu chache baada ya kibali
maalum. Hata hivyo kilikuwa kikisomeshwa kama somo katika madarasa
ya tano na sita na kingesomeshwa mapema zaidi mradi tu kisitatize
kusomeshwa kwa masomo mengine. Shule za watu binafsi zilisomesha
Kiingereza katika madarasa ya chini na kwa hivyo ziliwavutia wanafunzi
wengi. 51*

Vyuo vya kuwafunza walimu wa lugha za kwanza ambavyo viliwafunza
walimu wa kusomesha madarasa ya kwanza hadi ya nne vilinuiwa
kusomesha kwa lugha za kwanza tu pamoja na kusomesha somo la
Kiingereza.

Katika shule za Magoa lugha ya kusomesha ilikuwa ni Kiingereza
kuanzia mapema katika muongo wa 1950. Katika shule zingine za
Wahindi, Kihindi na Kigujerati zilitumiwa kusomesha masomo mengine.

--
49* Education Department, Annual Report ya 1945 na 1946 uk. 9.
50* Uganda Annual Colonial Report ya 1946 uk. 51.
51* Education Department, Annual Report ya 1949 uk. 8.

79

Katika shule chache za msingi za Kiafrika ambapo somo la Kiingereza
lilianzishwa mapema, ilionekana kwamba hakikuathiri masomo mengine.
Kufuatia pendekezo la kundi la Binns na Kamati ya de Bunsen ya 1952,
ilikatwa shauri somo la Kiingereza lianzishwe katika madarasa ya chini ya
shule za msingi. Kabla ya hapo, somo la Kiingereza halikupendekezwa
katika madarasa manne ya kwanza katika shule za msingi. Ingechukua
muda kabla walimu wa kutosha hawajafundishwa ili matokeo ya taratibu
hii yapatikane.

Pigo kubwa zaidi la Kiswahili nchini Uganda lilikuwa tangazo la 1952
kwamba Kiswahili hakitambuliwi tena kama somo katika shule za
Uganda. 52* Shule ambazo hazikuhusika ni za polisi na watoto wao. Lugha
tano za Kiafrika ambazo tumezitaja ziliendelea kuwa lugha za pekee za
Kiafrika zilizotambuliwa katika elimu. Lugha zingine za Kiafrika zinge-
tumika tu katika madarasa mawili ya kwanza kama tulivyotaja. Lugha za
kusomesha masomo yote katika miaka yote sita ya shule za msingi zilibaki
hizo lugha tano za Kiafrika, nacho Kiingereza hakikusomeshwa sana
kabla ya darasa la tano. Lakini shule zilihimizwa zianze kukisomesha
katika madarasa ya chini.

Ripoti ya Idara ya Elimu ya mwaka 1953 inatambua kwamba hata
ingawa msimamo wa elimu ni kwamba mtoto hujifunza vizuri anapotumia
lugha ya mama yake, lugha za Kiafrika zinazotumiwa katika shule za
Uganda si lugha za mama za watoto wengi nchini Uganda. Hii ni kwa
sababu ni lugha tano tu zinazotumiwa kielimu katika nchi yenye lugha
nyingi. Serikali haikuwa tayari kutumia lugha zote za Uganda mashuleni
kwa sababu ya gharama kubwa. Kulikuwa na maoni kwamba ikiwa
Kiingereza kingesomeshwa vizuri katika madarasa ya mwanzo ya shule za
msingi, watoto wangeanza kukitumia kama lugha ya kusomesha masomo
mengine badala ya kubadilisha kutoka lugha ya mama hadi lugha nyingine
ya Kiafrika iliyotambulikana (moja kati ya zile lugha tano).

Ili kuwafunza walimu wa kusomesha Kiingereza katika madarasa ya
mwanzo ya shule za msingi, masomo maalum ya kuwafunza Kiingereza
yalitayarishwa mwaka 1954. Mwaka huo huo mafunzo ya kuwafunza
walimu wa kusomesha kwa kutumia lugha za kwanza yalikwisha. Baadhi
ya vyuo vilivyokuwa vikifunza walimu hao vilifungwa, na vingine
vilipanuliwa na kufanywa kuwa vyuo vikubwa. Kuanzia 1958 serikali
ilihakikisha kwamba Kiingereza kilisomeshwa kama somo muhimu
kuanzia darasa la tatu. Kiingereza kilitiliwa mkazo zaidi mwaka 1960

--
52* Education Department, Annual Report ya 1952 uk. 8. Tangazo lasema hivi: "Kiswahili si
lugha inayotambulika tena katika shule za Uganda, kwa sasa, kinatumika tu katika shule za
polisi na watoto wao kwa kuwa kingali lugha rasmi ya jeshi la polisi".

80

baada ya kuunganishwa kwa shule ambazo hapo awali zilikuwa zimega-
wanywa katika shule za Waafrika, Magoa, na Wazungu.

Kama tulivyojadili katika sehemu hii, kutumiwa kwa Kiswahili katika
elimu nchini Uganda kulianza vizuri kukiwa na msaada kamili wa serikali.
Kiswahili hakikuungwa mkono na baadhi ya Waganda - hasa Waba-
ganda. Kufuata mabadiliko ya siasa katika Afrika Mashariki, Kiswahili
kiliondolewa katika shule za Uganda mwaka 1952. Hata baada ya uamuzi
huo mkali Uganda iliendelea kuwa mwanachama na kutoa pesa za
kuigrarimia Kamati ya Kiswahili ya Afrika Mashariki hadi 1964.

Upinzani dhidi ya Kiswahili uliofanywa na Wabaganda wakati wa
ukoloni labda ulitarajiwa kwa vile walivyokuwa na nafasi maalum katika
nchi ya Uganda. Hali haiko hivyo tena katika Uganda huru. Uganda, sawa
na majirani zake wa Afrika Mashariki na kati, inahitaji Kiswahili katika
kujenga umoja wa taifa na kwa mawasiliano ya kimataifa. Kwa muda wa
karibu karne moja Kiingereza kimeshindwa kuyatatua matatizo ya lugha
ya Uganda. Si lugha ya mwananchi wa kawaida na kingechukua zaidi ya
karne nyingine kuwa hivyo. Kiswahili chastahili kupewa nafasi ya kuwa-
unganisha wananchi wa Uganda. Hatua ya kwanza ni kuanza kukisomesha
katika shule nchini Uganda.



Mzee alipotolewa nje alikuwa kama mtu mwenye wazimu.
Alikuwa akitetemeka kwa woga. Alitembea kwa haraka
kutoka nje. Moyo wangu ulivurugika kwa mchanganyiko
wa hasira na huzuni nilipoona mzee akikimbia Serikali
yake. Mzee alipokuwa akitoka nje sikuona kitu kingine
isipokuwa kwamba wazee walikuwa wakitukimbia. Uhusiano
kati yao nasi ulikuwa ukikatika. Niliona wazazi wakiwakimbia
watoto wao ambao sasa walikuwa kama simba. Kwa kuwa
mzee huyu alikuwa amevaa shati ambalo lilikuwa limepasuka
mgongoni niliweza kuona mgongo wake vizuri sana. Kweli
niliona wazee wakitupa migongo. Mgongo wa mzee huyu sasa
ulikuwa kama ukurasa ambao haukuandikwa maneno; ulikuwa
kama ubao mweusi uliofutwa upande mmoja.

Maneno yaliyokuwa yameandikwa upande mwingine
sikuweza kuyasoma. Mawazo haya yalikuwa bado yakinizu-
nguka ndani ya bongo na damu yangu mata tu niliposikia
Mkuu wa Wilaya akipiga kelele: "Mwingine aingie!"

Yule msichana aliingia. Alipoingia tu Mkuu wa Wilaya
alisikika akisema: "Aa! Pili karibu!" Mlango ulifungwa.

Mwanzoni walikuwa wakizungumza kwa sauti ya chini,
lakini baadaye walijisahau. Walianza kuzungumza kwa

7

sauti ya juu. Hata sisi tuliokuwa nje tuliweza kusikia
maneno yaliyokuwa yakisemwa.

"Pili, mpango huu unauonaje?"
"Hata mimi nimechoka na sinema. Kila Jumapili
sinema. Afadhali Jumapili hii twende Serengeti tukawaone
wanyama."

"Basi kama ni Serengeti inafaa twende Jumamosi ili
tulale huko siku mbili maana ni mbali kidogo."

"Haya, vizuri. Lakini mimi leo nimechoka sana; utakuja
kunichukua jioni twende sinema?"

"Tutakuja kama saa mbili hivi. Utamwambia shemeji
pia twende naye."

Waliendelea kuzungumza kwa muda mrefu. Mambo
waliyosema yalikuwa mengi. Mara kucheka, mara "Mimi
sitaki", na mara "Huniamini". Nilisikia mlio wa kiti
kikibururwa chini. Nafikiri Mkuu wa Wilaya alikuwa akiinuka.

"Lete kitambaa changu! Hakika mimi siwezi kutoka nje
bila kitambaa kichwani!".

Kwa muda mfupi uliofuata walizungumza tena kwa sauti
ya chini. Ilikuwa baada ya muda huu msichana alipotoka
nje. Nilipokuwa nikiingia ndani nilisikia watu nje wakimgunia.

Kweli nilipoingia ndani sikuweza kuamini kwamba
aliyekuwa mbele yangu ndiye alikuwa Mkuu wa Wilaya.
Alikuwa kijana mwenye umri wa miaka thelathini hivi. Mara
tu nilipoingia na kutazamana uso kwa uso kila mmoja aliweka
matuta usoni, kwani tulifahamiana tangu zamani.

"Habari ya asubuhi," nilimsabahi.

"Asante, keti kitini."

"Mimi nilikuwa na shida kidogo."

"Ndiyo kusema sasa huna."

"Nina shida," nilijisahihisha ili kumpendeza. "Natafuta

8

kazi ya muda. Miezi mitatu hivi."

"Wewe nani?"

Nilikasirika kidogo, lakini hasira yangu niliimeza kwa
kuuma meno. "Mimi Kazimoto, mwanafunzi wa Chuo
Kikuu - Dar es Salaam."

"Huko ndiko mnakofunzwa jinsi ya kuwasabahi wakubwa
namna hiyo."

"Mimi ninatafuta kazi."

"Hata mimi nilipokuwa Makerere nilikuwa nikiwaheshimu
watu. Au labda kwa kuwa umesoma Chuo Kikuu unafikiri
u mtu tofauti."

"Kusoma Chuo Kikuu siyo dhambi," nilimjibu. "Lakini
mimi hayo hayakunileta hapa. Mimi ninatafuta kazi."

"Huna adabu! Kaa nje kwanza, unanichelewesha kazi
bure. Utaingia humu mtu wa mwisho."

Nilisimama. Kwa muda nilimtazama machoni.

"Unasikia! T-o-k-a nn-nje!"

Nilitoka.

Msichana aliyekuwa akinifuata aliingia ndani. Kwa kuwa
nilikuwa nimekwisha sikia kwamba kulikuwa na kazi nilikaa
pale kwa muda; zaidi ya hayo watu walikuwa wamebaki
wachache.

Yule msichana hakukawia sana mle ndani. Alipotoka nje
nilimwona anatembea kuelekea kwangu. Nilifikiri kwamba
labda alikuwa ametumwa na Mkuu wa Wilaya kuja
kuniambia jambo fulani.

"Mwalimu, siku hizi uko wapi?"

"Bado ninaendelea na masomo."

Ingawa nilimjibu, nilikuwa sikumbuki mahali nilipopata
kumfundisha. Nilikuwa nimekwisha fundisha shule nyingi
kwa muda. Shule zingine sikumaliza hata miezi miwili.
Niliona haya kidogo kuona kwamba kwa muda wote ule

9

nilikuwa nikijitahidi kugusa kiuno cha mwanafunzi wangu.

"Kwa muda wote huu ulikuwa bado hujanitambua. Mimi
nilipokuona tu nilikukumbuka mara moja."

"Samahani, nimesahau jina lako."

"Salima."

"Siku hizi uko wapi? Habari za Jangwani?"

"Jangwani nilimaliza mwaka jana. Siku hizi ninafanya
kazi."

"Kazi gani?"

"Ninafundisha, lakini ninatarajia kuacha kazi hivi hivi
karibuni."

"Kwa nini?"

"Kazi ngumu, pesa kidogo. Haya kwa heri."

"Kwa heri, asante."

Alipokuwa amekwenda nilikumbuka wazi kwamba Salima
alikuwa mmoja kati ya wasichana waliokuwa wakisoma shule
ya wasichana ya Jangwani huko Dar es Salaam. Ingawa
wakati huo alionyesha mapenzi kwangu, mimi sikutaka, kwa
kuogopa kwamba wanafunzi wengine wangetambua wange-
fanya fujo na ingekuwa vigumu kuendesha darasa. Zaidi ya
hayo ufundishaji wakati huo ulikuwa ni mtihani na mkaguzi
alikuwa akikaa darasani. Salima alinifanya sasa nikumbuke
tena wale wasichana waliokuwa wakikaa mbele. Wasichana
hao, kwa vile walivyokuwa wamezoea kukaa walinifanya
nifundishe nikitazama juu ya vichwa vya wanafunzi.
Hili ndilo kosa ambalo mkaguzi alinikumbusha karibu kila
siku.

Wakati nilipokuwa nikifikiria mambo haya niliona mtu
wa mwisho anaingia ofisini. Sura ya Mkuu wa Wilaya
ilinijia tena kichwani. Nilijongea karibu ili nipate kuingia
tena. Ilikuwa wakati huu nilipovumbua kwamba nilikuwa
nimesahau kufunga kifungo kimoja cha suruali yangu.

10

Jambo hili lilinuidhi sana. Nilianza kufikiri mabarabara
yote ya mjini niliyokuwa nimepita nikiwa katika hali hiyo;
pia watu wote niliowaona. Lakini mara mlango ulifungu-
liwa. Yule mtu alitoka. Niliingia.

"Naam, Bwana mkubwa sana, nafikiri sasa kiburi
kimekwisha. "

"Mimi sina kiburi. Shida yangu kazi."

"Keti."

Nilikaa mbele yake, tukawa tunatazamana. Nilipotupa
macho juu ya meza niliona visusu viwili. Kimoja
kimeandikwa In kingine Out. Ilikuwa ndani ya kile
kijikapu cha In nilimoona picha za wasichana watatu
ambao sasa niliweza kuwafahamu - Vumilia, Pili na Salima.
Ndani ya kijikapu cha Out niliona bahasha za kiserikali.
Juu ya meza niliona barua ambayo ilikuwa bado kwisha
kuandikwa. Niliweza kuona maneno machache: "Salima
natumaini kwamba hutakasirika sana; wale wasichana sina
uhusiano nao..."

Haya yote niliyaona kwa haraka Mkuu wa Wilaya
alipokuwa anafunga kabati, kwani nilipoketi tu juu ya kiti
yeye aliinuka. Alipomaliza kufunga kabati nilimwona
anachukua funguo zingine mfukoni mwake. Nafikiri zilikuwa
funguo za gari lake.

"Samahani, ninataka kufunga ofisi. Saa nane na nusu sasa.
Utarudi kesho."

Nilimtazama machoni kwa mshangao.

"Kazimoto, fika kesho asubuhi." Mimi niliendelea kumkazia
macho.

"Bwana Manase," nilimwita.

"Ndiyo, unanifahamu; lakini sasa nimo kazini."

"Sasa umo kazini."

"Ndiyo."

11

"Manase," nilimwita tena.

"Kazimoto," aliniita.

Nilisimama pale nikamtazama dakika chache, kisha nikatoka
nje kwenda kutafuta chakula; njaa ilikuwa inaniuma.


Naam, Mkuu wa Wilaya, Bwana Manase, tulikuwa tukiishi
kijiji kimoja. Ukweli ni kwamba tulikuwa majirani. Tangu
utoto tulikuwa tumezoeana. Manase alipokuwa bado mtoto
mdogo tulikuwa tukimwita "Popo" kwa vile masikio yake
yalivyokuwa makubwa. Kati ya wanafunzi tuliokuwa tukisoma
darasa la kwanza Manase ndiye alikuwa akifikiriwa kuwa
mjinga wa mwisho. Ninakumbuka kwamba siku moja Manase
alilia sana darasani bila kupigwa. Sababu yenyewe ilikuwa
kwamba mwalimu alimwekea zero kubwa yenye macho
mawili na meno yakimcheka. Kwa kuwa alikuwa jirani yangu,
mara nyingi alikuwa akishinda nyumbani kwetu na nikimsaidia
katika hesabu.

Uadui kati yangu na yeye ulianza tulipokuwa darasa la
nne. Siku moja, pale shuleni nilichimba shimo dogo na fupi.
Ndani ya shimo hili niliweka maji. Niliwaita wanafunzi kama
kumi hivi. Walipojongea niliwaambia, "Shimo hili ni refu
sana huwezi ukagusa mwisho wake."

"Labda kuna nyoka?" wengine waliuliza.

"Hapana," nilijibu.

Manase alijitokeza. "Mimi ninaweza kugusa mwisho
wake," alisema.

"Haya jaribu," nilimwambia.

Manase alitumbukiza mkono. "Mbona fupi," alisema.

"Umegusa chini?" nilimwuliza.

"Ndiyo."

"Ebu tuzolee mchanga wa chini," nilimwambia.

Manase alipotoa mkono, alikuwa amejaza mbolea ya
ng'ombe mkononi mwake. Wanafunzi walimzomea, akalia.

12

Tangu siku hiyo Manase alinichukia na nyumbani kwetu
hakufika tena kuja kuongea.


Kama ilivyo kawaida ya watoto wadogo uadui huu
haukuendelea, kwani wakati wa mavuno ulipowadia tulijikuta
tunatega ndege pamoja. Baada ya mavuno tulizoea pia kupita
mashambani tukitafuta yale mawele yaliyosahauliwa
kuvunwa. Yale tuliyopata tulizoea kwenda kuuza kwa padri
mmoja wa Kizungu wa misioni yetu. Nakumbuka siku moja
baada ya kuuza mawele yetu tulipita kaburini ili kula mapera.
Tulipokuwa tumepanda tulisikia viatu vya padri akizunguka
kaburini akisoma kitabu kama ilivyo kawaida yao. Tulifikiri
kwamba alikuwa hawezi kutuona. Tulikaa kimya mtini.
Alipofika karibu na mti tuliokuwa tumeranda alisimama
akawa anasoma kitabu chake hapo. Alisimama kwa muda
mrefu; halafu tuliona kidevu chake kinainuliwa juu.
"Shukeni, ee!"

Tulishuka hali tukitetemeka. Alituongoza hadi chumbani
mwake. Tulipofika chumbani tuliambiwa kwenda kuzoa
mchanga nje. Tulifanya vile. Tulipoingia chumbani tuliambiwa
kuumwaga juu ya sakafu, na juu ya mchanga huu tuliamrishwa
kupiga magoti. Baada ya muda mfupi tulilia kwa maumivu.
Hapo ndipo alipotwambia kulala chini. Tulipigwa fimbo tano
tano.

"Haya kaeni!" Tulikaa.

"Baba zenu nani?" Tulimwambia.

"Ninyi watoto wa Wakristo ndio mwaiba mali ya kanisa!
Hamfahamu kwamba kuiba ni dhambi? Tajeni amri za
Mungu!" Tulizitaja.

"Rudieni amri ya saba mara nne!" Tulifanya hivyo.

"Mnajua kusoma?"

"Ndiyo," tulijibu pamoja.


13

Padri alitupa vijitabu viwili vya Katekesimu. "Haya nendeni
nyumbani! " Tulitoka kwa haraka kwa mchanganyiko wa
hasira na furaha.

Tulikuwa darasa la nane uadui uliporudi tena, lakini
mara hii kwa bahati mbaya. Wakati wa mavuno
ulikuwa umekaribia, mimi nilikuwa nimesimama juu ya
ulingongo katikati ya shamba la mawele la baba yangu;
Manase alikuwa katika shamba la baba yake. Tulikuwa
tukiwinga ndege. Tulianza mchezo wa kutupiana mawe kwa
teo. Kwa bahati mbaya Manase alinipiga kichwani damu
ikanitoka. Nilikimbilia nyumbani hali nikilia. Kwa muda
hatukuonana tena na Manase.

Tulikuwa marafiki tena tuliposhinda wote kuingia darasa
la tisa kwani tulishinda kwenda shule moja. Urafiki ulirudi
hasa siku niliyomwokoa kutoka mtoni. Tulikuwa tukioga
mtoni Manase alipoanguka mahali ambapo maji yalikuwa
marefu. Kwa kuwa alikuwa hajui kuogelea alianza kuzama.
Wenzangu walikimbia. Mimi niliogelea mara kwenda
kumchukua. Karibu nife naye, lakini kwa bahati nzuri
niliweza kumvuta mpaka maji mafu. Macho yake yalikuwa
mekundu. Jioni hiyo, baba yake aliposikia aliniletea kuku
wawili kama zawadi.


Wakati tukiwa darasa la kumi, kwa mshangao wa kila mtu,
akili za Manase ziliongezeka sana, akawa akiongoza darasa.
Mwaka huu mimi sikuumaliza. Nilipatwa na ugonjwa wa
kifua kikuu. Nilikaa hospitalini kwa muda wa mwaka mmoja
mzima. Nilipotoka hospitalini nilikuwa na nia ya kusoma
kufa kupona, lakini mwaka huo baba akashindwa kulipa ada
ya shule; shule nikaacha, nikatafuta kazi. Manase akawa sasa
miaka miwili mbele yangu. Kazi nilifanya kwa muda wa
mwaka mmoja ili kuhakikisha kwamba nilipata pesa za

14

kutosha kuweza kunifikisha darasa la kumi na mbili. Wakati
huu wote Manase alikuwa rafiki na jirani mwema mpaka
alipomaliza Makerere na kujinyakulia shahada ya B.A.
Wakati huu uhuru ulikuwa umekwisha ingia. Jina la Nyerere
likawa likiimbwa hata na watoto wadogo. Mwafrika akawa
Mwafrika; Mzungu akawa Mzungu; Mhindi akawa Mhindi na
Mwarabu akawa Mwarabu. Kwa ufupi kila mtu akaanza
kuona ukweli wa hali yake. Aliyejiona tofauti alirudi
kwao. Kina Manase wakawa watu waliohitajika sana ili
kushika uongozi wa nchi. Manase akawa ofisa mkuu wa
elimu, huko Tanga. Alifanya kazi vizuri sana. Akahamishwa
hadi Dar es Salaam. Akawa ametolewa kwenye matawi na
kuletwa kwenye shina.

Ilikuwa wakati huu Manase aliponifanyia ujeuri mkubwa.
Alifanya kosa ambalo nilikuwa siwezi kumsamehe. Kisasi
kilianza kuukera moyo wangu. Kosa hili ndilo lililotufanya
tuzungumze namna ile ofisini. Nilipoingia, kusema haki,
nilikuwa sitegemei kumkuta yeye, kwani baada ya kosa hili
nilikuwa sifahamu mahali alikokwenda.

Baada ya kukumbuka maisha yetu haya ya zamani, na
baada ya kulikumbuka kosa hili, nilijikuta nikisema moyoni:
"Lazima nijilipize kisasi; nimezaliwa kama yeye; mimi
mwanamume kama yeye. Haiwezekani. Lazima nijilipize
kisasi." Mara nilistukia nagongana na mwanamke fulani
njiani.

"Kaka, mbona hivi!" alisema. "Siku hizi hamwoni watu?"

"Samahani, dada yangu, mawazo yangu yalikuwa mbali,"
nilimjibu.

"Mawazo gani, unataka kuua mtu?"

Sikutaka kuzungumza naye zaidi. Niliendelea na njia
yangu. "Sasa ninakwenda wapi?" nilijiuliza moyoni. "Ndiyo,
njaa inaniuma, kwa hiyo nilikuwa na nia ya kutafuta hoteli."

15

Nilikumbuka kwamba hoteli niliyokuwa nikitafuta nilikuwa
nimeiacha nyuma. Nilirudi. Nyuma kidogo niliona kibao
kimeandikwa "Hoteli ya Wananchi". Niliingia ndani kuagiza
wali na nyama ya kuku.

Wakati nikila watu ambao walikuwa wameenea vumbi
waliingia hotelini. Ilionekana kwamba wafanya kazi wa humo
hotelini waliwatambua mara moja. Walikuwa wasafiri kutoka
Dar es Salaam, kama nilivyokuja kuelewa baadaye. Chakula
walicholetewa kilikuwa tofauti na kile walichoniletea mimi.
Ingawa nilikuwa mbali kidogo niliweza kuona kwamba wali
walioletewa ulikuwa mbaya. Lakini kwa kuwa walikuwa na
njaa kubwa hawakuweza kutambua kwamba walipewa uporo.
Sikushangaa sana. Mambo haya nilikuwa nimekwisha yaona
yakitendeka katika sehemu nyingi za nchi yetu wakati nikiwa
safarini.

"Mwishowe tumefika, saa ishirini na saba," mmoja kati yao
alianza kuzungumza.

"Mimi mgongo unaniuma sana, sijui kwa nini?"

"Sababu ya mabarabara mabaya."

"Sijui serikali inafanya nini?"

"Watajali nini wakati wao wanapita hewani?"

Mazungumzo yao sikuyafuata zaidi, kwani karibu na meza
niliyokuwa nimekaa walikuwa wamekaa wazee wawili
wakisimuliana hadithi zao za miaka miwili mitatu iliyopita,
na masikio yangu yalivutiwa upande huo.

"Bwana we! Niulize mimi nikwambie!" mzee mwenye
sharubu alimwambia mwenziwe huku akigonga meza kwa
mfupa kusisitiza wazo lake. "Kwa muda wa miaka miwili
nilikuwa dereva wa mkuu mmoja wa mkoa. Wewe fikiri mzee
kama mimi, mkuu wa mkoa ananiambia 'kanitongozee
msichana'. Ni jambo ambalo mara nyingi liliniudhi. Heshima

16

yangu yote kwenda kuipoteza mbele ya msichana mdogo!
Na mvi zangu kichwani! Halafu nikishamleta nyumbani
kwake au hoteli, anasemaje? 'Utakuja kumchukua saa kumi
na moja asubuhi umrudishe.'Mimi usingizi napoteza, yeye
analala vyema!"

"Wewe unajua upande mmoja tu," mwenziwe alidakia.
"Mimi nilikuwa nikishika faili zao za mishahara. Maofisa
wote hawa usiwaone nje matumbo kuning'inia! Wengi kati
yao wanapokea shilingi mia mbili kwa mwezi!"

"Kwa nini?"

"Madeni, ndugu yangu, madeni. Utakuta wengi wana
mikopo ajabu! Magari yote mikopo; maredio makubwa, yote
mikopo; majiko ya kupikia, yote mikopo; karibu kila kitu
cha maana kiko chini ya mkopo!"

Walipoona kwamba kila mtu alikuwa akiwatazama
walimaliza chakula chao wakatoka.

Kwa muda kulikuwa na hali ya unyamavu pale hoteli, hali
hii ilinifanya nimkumbuke Manase. Niliinuka kwa hasira
huku nikiuma meno. Bilauri ya maji iliyokuwa juu ya meza
yangu ilianguka na kupasuka. Nilikuwa karibu nitoke nje
niliposikia kelele.

"Bado hujalipa!"

"Samahani," nilisema. Nililipa.

Kwa mara ya kwanza wazo la kumkata Manase vipande
vipande lilinijia kichwani mwangu wakati nikirudi katika
nyumba ya wageni nilimokua nimekodi chumba cha kulala.
Jioni sikula.

Jioni hiyo kulikuwa na mchezo wa kuigiza katika jumba la
maendeleo. Mchezo huo ulikuwa ukichezwa na wanafunzi
wa shule ya wavulana ya Nsumba. Nilikata shauri kwenda
kuutazama ili kutuliza kichwa changu kidogo chenye kiburi.

17

Wanafunzi hawa walicheza michezo miwili. Mchezo wa
kwanza ambao ulichekesha sana watu ulikuwa juu ya baba
mmoja aliyekataa kupeleka mtoto wake mgonjwa hospitali.
Mchezo wa pili ulikuwa mchezo wa mapenzi. Yule mchezaji
aliyefungua mchezo huu alisimama katikati, na kwa sauti,
hali akisambaza mikono yake alitamka maneno haya:

"Ndugu zangu, katika mchezo huu mtaona kwamba chuki
haina nguvu kama wale uwachukiao wanakupenda. Utawezaje
kuwachukia wale wakupendao? Kweli, mwanadamu hawezi
kumchukia mwanadamu mwenziwe isipokuwa matendo yake.
Ndugu zangu, mtaona kwamba kujilipiza kisasi kwa watu
wakupendao ndio mwanzo wa mapenzi. Ndugu zangu,
mtaona kwamba mwisho wa mwanadamu ulianza alipoweza
kutembelea miguu miwili. Pia mtaona ugonjwa utakaowama-
liza akina mama wenye mabinti."

Aliinama. Watazamaji walipiga makofi.

Mchezo ulikwisha saa nne. Nilipotoka nje nilikuwa na nia
ya kwenda kulala mara moja, lakini kwa kuwa katika nyumba
ya wageni nilimokuwa nimekodi chumba kulikuwa na bar
nilikata shauri kunywa kidogo.

Mbele yangu alikuwa amekaa mwanamke mmoja aliyekuwa
akinitazama mara mbili mbili. Mimi sikuonyesha alama yo
yote ya kumhitaji; nilikunywa pombe yangu kimya. Mbwa
abwekaye haumi, aumaye ni yule kimya. Hii ndiyo ilikuwa
njia yangu kupata wanawake. Nilipoagiza chupa ya pili
mwanamke huyu alikuwa amehamia karibu nami.

"Unakunywa nini?"

"Tusker," alijibu kwa haraka.

Niliagiza chupa mbili za Tusker. Tulikunywa pamoja mpaka
saa sita. Walipofunga bar nilinunua chupa moja ya Grenado.
Chupa hii tuliinywa pamoja chumbani mwangu.

"Unatoka wapi?" aliuliza. Nilimwambia.

18

"Jina lako nani?" Nilitafuta moja.

"Kumbe unatoka sehemu moja na Manase." Nilikubali.

"Mhuni huyo! Amemwachisha kazi mwalimu mmoja, sasa
anaishi pamoja naye."

"Salima?" niliuliza kwa mshangao.

"Huyo huyo! Lakini siye huyo peke yake, ana msichana
mwingine katika mtaa wa Uhuru."

"Ndiyo kusema anataka kumwoa Salima?"

"Inaonekana vile, lakini tena tunasikia baba yake
amekwisha kumtafutia mchumba mwingine huko nyumbani
kwao. Wanasema kwamba Bwana Manase amemkataa kwa
sababu ni mshamba mno; wengine wanasema anataka kuwaoa
wote wawili."

Nilihisi kwamba huyo msichana wa shamba alikuwa Vumilia.

Mawazo juu ya Manase yalianza tena kuvuruga akili zangu.
Nilianza kunywa pombe nyingi ili nilewe upesi nisahau
mambo. Chupa ilikuwa bado kwisha mawazo haya yalipopotea:
mwanamke huyu aliweka kichwa chake juu ya miguu yangu.

"Bwanangu, mimi usingizi umenipata, tukalale!"

Hakuweza hata kusimama. Nilimbeba hadi kitandani. Hata
nguo nilipaswa kumvua. Nilishangaa kukuta hirizi kiunoni
mwake. Hirizi hii niliitoa na kuiweka juu ya meza. Baada ya
kumvua nguo zote nilifunga mlango, nikazima taa.

"Utakwenda lini nyumbani?" yule mwanamke aliniuliza asubuhi.

"Kesho."

"Utalala humu tena?"

"Ndiyo."

"Leo usiku usinipe pombe nyingi."

"Kwa nini?"

"Ninataka kukuonyesha mchezo halisi wa kwetu."

19

"Ahaa!"

Wakati huo alikuwa akijaribu kuinuka kutoka kitandani.

"Usinitazame!" aliniambia. Nilitazama pembeni.

"Aa! Iko wapi?" alipiga kelele.

"Nini?"

"Hirizi yangu ! "

"Hiyo hapo mezani."

"Kwa nini uliitoa?" aliuliza kwa wasi wasi.

"Kwa nini nisiitoe?"

"Mimi siwezi kutunza mtoto wako." Alivaa nguo kwenda
kuoga. Baada ya kuoga tulipeana kwa heri ya kuonana.

Alipokuwa amekwenda nilikumbuka kwamba nilipaswa
kumwona Manase asubuhi hiyo. "Jambo zuri ni kwamba
nilipata usingizi," nilisema moyoni. Wazo la kufika tu ofisini
nimchome Manase visu vya tumboni lilinijia tena kichwani.
"Huenda nami nikanyongwa," nilisema moyoni. "Sitapata
faida yo yote isipokuwa kuwaacha wazazi wangu taabuni.
Jambo la maana ni kujaribu kumpa Manase maisha magumu
hapa duniani. Nisipoweza basi nitajilipiza kisasi kwa njia
ingine." Nilikata shauri kwenda kumwona Manase ofisini
kila kisu.

Siku ya kwanza nilipoingia ofisini kwa Manase nilikuwa na
nia ya kuomba kazi ya muda. Yeye alifikiri kwamba nilikuwa
nakuja kumwuliza juu ya kosa alilofanya. Kwa hiyo alijaribu
kutumia lugha kali kama kwamba nilikuwa nakuja kwa
ugomvi. Kwa kuwa siku hiyo sikusema neno lo lote kuhusu
jambo hilo Manase aliona kwamba sikuwa na kinyongo. Sasa
nilipoingia hakuwa mkali kama siku ya kwanza.

"Karibu ukae, Kazimoto," alisema mara tu nilipoingia.

"Asante."

"Kuhusu habari ya kazi nafikiri utapata. Tunahitaji vijana
kama nyinyi katika kufanya kazi hii ya kuhesabu ng'ombe.

20

Wewe utapata shilingi mia sita kila mwezi ufanyao kazi."
Alifungua kabati kutoa karatasi za maswali na mambo
mengine yaliyohitajika kujazwa. Alinipa mkononi.
"Nafikiri sasa umefurahi, sivyo? Unaweza kwenda."

Nilikuwa karibu kutoka nje nilipofikiri kwamba ilikuwa
lazima nimwulize juu ya jambo hilo alilotenda - tendo la
kinyama.

"Manase," nilimwita. Alinitazama. "Jambo gani ulifanya?"
nilimwuliza hali nikimtazama usoni. Mara moja sura
ilimgeuka. Nilimwona anafungua mdomo pole pole.

"Kazimoto, huelewi vizuri hadithi yenyewe."

"Hadithi nimekwisha isikia, Manase."

"Halikuwa kosa langu."

"Ni kosa la nani?"

"Hakika Rukia mchokozi sana. Yeye ndiye alinianza."

"Alikuanzaje?"

"Unaona. Siku moja usiku nilipokuwa nimekwisha lala
usingizi nilisikia mtu anagonga mlango wangu, 'Nani huyo!'
nilisema kwa sauti. 'Ni mimi Rukia, fungua mlango.' Kuna
nini?' nilimwuliza. 'Wewe fungua mlango tu'. Nilipofungua
mlango aliingia chumbani mwangu; alilala juu ya kitanda
changu. Sasa wewe fikiri Kazimoto, mwanamume kama
wewe ungefanya nini?"

"Mambo yote ninayafahamu. Unafikiri sifahamu maisha
yako?"

"Hata mimi ninayafahamu maisha yako. Ninafahamu
kwamba usiku ulikuwa na Pili. Huwezi kunidanganya
kwamba wewe bikira katika mambo haya (nilishangaa kwa
nini sikuweza kumtambua Pili: mwanamke akiwa mawindoni
hugeuka sura). Pia ninayafahamu maisha ya Rukia. Bila shaka
utakubaliana nami nikisema kwamba Rukia alikuwa malaya
tangu alipoota maziwa."

21

"Unamwita malaya!" nilisema kwa hasira.

"Ndiyo."

"Hebu sema tena!"

"Rukia ni malaya. Kama umekasirishwa na jambo
lililotokea kwa bahati mbaya unaweza kufanya jambo lo lote
upendalo! Sijali sasa! " alisema kwa hasira. "Sasa hata kazi
hupati!" Karatasi nilinyang'anywa.

"Tutaona! " nilimwambia kwa hasira kubwa.

Nilipokuwa njiani kelekea chumbani kwangu niliweza
kuyakumbuka yale maneno barabara. Nilijaribu kuyarudia
moyoni:

"Ndugu zangu, katika mchezo huu mtaona kwamba chuki
haina nguvu kama wale uwachukiao wanakupenda. Utawezaje
kuwachukia wale wakupendao? Kweli..."

22

			2

Rukia hakuwa mwingine isipokuwa ndugu yangu aliyenifua-
ta mimi. Ndugu mwanamke pekee, mwema, ndugu mfanya-
kazi. Uzuri wake, kama nilivyosikia watu wakisema, ulikuwa
uzuri wa aina ya pekee. Uzuri ambao hata kipofu aliweza
kuuona. Kwa hiyo sisi nyumbani tukawa tunaona mwanga
mbele ya maisha yake. Tabia yake, kama tulivyoiona
nyumbani, ilikuwa nzuri ingawa ni vigumu kufahamu mambo
ya wasichana. Kwa kuwa alikuwa mzuri Baba na Mama
walitaka kumwachisha shule ili aolewe, kwani alipokuwa
bado darasa la sita alikuwa amekwisha chumbiwa na vijana
watatu. Mawazo ya wazazi wangu niliyapinga, nikayashinda.

Rukia alishindwa kuingia darasa la tisa, lakini mimi
nilikuwa na nia ya kumwelimisha. Nilimtafutia shule, na
baada ya kupita kichinichini kama ilivyokuwa kawaida,
nilipata shule moja huko Dar es Salaam. Taabu sasa ikawa

23

mahali pa kupanga: shule yenyewe haikuwa na malazi kwa
wanafunzi.

Manase wakati huu alikuwa akiishi Oysterbay, na kwa
kuwa alikuwa na nyumba kubwa nilifikiri ataweza kuishi na
ndugu yangu. Licha ya nyumba kuwa kubwa wakati huu
ulikuwa wakati ambao uhusiano kati yangu na yeye ulikuwa
mzuri. Nilipomwambia Manase taabu yangu alikubali kukaa
na ndugu yangu. Wakati huo mimi nilikuwa nimekwisha ingia
Chuo Kikuu.

Mwaka wa kwanza nafikiri ulipita salama. Mambo yalianza
mwaka wa pili alipoingia darasa la kumi. Nilipozungumza
naye mwaka huo alinieleza kwamba alikuwa na shida kidogo
tu. Kwa kuwa hakueleza vizuri shida yake nilifikiri kwamba
ilikuwa njia ya kuzungukia akitaka kuomba pesa. Nilimpelekea
shilingi sitini, nikitumaini kwamba msichana aweza tu
kujitunza akiwa na pesa za matumizi.

Nilipokutana naye siku ingine alinishukuru kwa pesa
nilizompa, lakini katika mazungumzo aliniuliza swali ambalo
lilinitia wasiwasi. Alisema: "Sijui Manase ni mtu wa namna
gani." Hapo ndipo nilipoanza kuhisi kiini cha shida yake.
Niliona wazi kwamba Manase alikuwa akijaribu kufanya
mambo yasiyotakikana.

Siku chache baadaye nilipata barua kutoka kwa ndugu
yangu. Ilikuwa imeandikwa kwa hasira. Msitari wa kwanza
ulisema: "Kaka usiponitafutia mahali pengine pa kukaa mimi
nitarudi nyumbani. Heri kuacha shule!" Niliona kweli
kwamba alikuwa amekwisha sumbuliwa sana. Siku hiyo
nilipanda basi hadi Oysterbay. Nilipofika nyumbani kwa
Manase sikukuta mtu ye yote nyumbani, isipokuwa mbwa
aliyekuwa amefungwa karibu na mlango kulinda wezi.
Nilirudi mjini. Nilijitahidi kutafuta nafasi, lakini rafiki zangu
wengine waliokuwa wakiishi mtaa wa Magomeni Mapipa

24

walikuwa na vyumba viwili tu. Chumba cha maongezi na
chumba cha kulala, basi. Niliona hatari zaidi katika uchache
wa vyumba kuliko katika tabia ya mtu mwenyewe. Kwa
hiyo nilimwandikia barua ndugu yangu nikimweleza shida
ya kupata mahali pengine. Nilimwomba avumilie, mwaka
huo uishe.

Kwa muda wa mwezi mmoja sikuonana naye na sikupata
barua kutoka kwake. Nilifikiri kwamba Manase alikuwa
ameacha mchezo wake na kwamba ndugu yangu alikuwa
akiishi bila kusumbuliwa. Ilikuwa baada mwezi mmoja
uliofuata nilipopata tena barua kutoka kwake, nayo
nilipoifungua ilikuwa imeandikwa, juu kabisa, neno "SIRI".
Niliisoma.

Kaka mpendwa,
Moyo wangu siku hizi hauna raha. Lakini leo
nimechukua kalamu ili nikueleze mambo yote.
Nimeona kwamba siwezi kuwa nakuficha wewe
mambo, hali mambo yenyewe sasa hayawezi
kufichika. Wewe ukiwa kaka yangu na ndiye
uliyenitafutia nafasi hii ya shule ninakupa heshima.
Fahamu kwamba mambo haya sijapata kumweleza
mtu mwingine isipokuwa wewe peke yako.

Kaka, uliponileta hapa nilikaa kwa raha kwa muda
wa juma moja tu. Baada ya juma hiyo niliona Manase
anaanza kunitazama kwa njia ya ajabu. Baada ya
majuma mawili mambo yalizidi kuwa mabaya, kwani
nilipokuwa naoga siku moja niliona jicho lake
kwenye tundu la ufunguo.

Mwishowe aliniambia wazi alichokuwa anataka.
Nilimwambia: 'Manase! Kaka yangu akifahamu
litakuwa jambo la aibu sana!' Lakini yeye alijibu

25

kwamba wewe ni mwanamume kama yeye. Alifikia
hata hatua ya kutumia nguvu! Na kweli alitumia
nguvu bila utashi wangu.

Kaka, sitaki kukupotezea muda wako wa kujifunza
kwa kusoma barua ndefu. Mimi maisha yangu
yameharibika. Shule nimekwisha acha. Jambo ambalo
limenisikitisha sana ni hili lifuatalo: Jana usiku, Manase
alirejea nyumbani mlevi. Alikuwa na tikiti ya basi.
Baada ya kunitukana kwa maneno ambayo siwezi
kukuandikia alianza kupanga vitu vyangu sandukuni.
Leo atanisindikiza hadi kituo cha basi. Kaka, machozi
yanilengalenga, sijui nitasema nini kwa Baba na Mama.
Usifike kuja kuniaga kwenye kituo cha basi nisije
nikazimia.

Sina mengi.

	Nduguyo, Rukia Mafuru.

Hasira iliyonipata baada ya kusoma barua hii haina kifani.
Nilijikuta nasema moyoni "Kulikokuwa na mwanga sasa giza!
Manase ana kiburi namna gani! Mimi mwanamume kama
yeye!"

Kwa muda wa siku moja sikuweza kuhudhuria masomo
kwa vile kichwa changu kilivyokuwa kimevurugika. Wakati
huu sikuweza kwenda kumwona Manase. Hasira yangu
ilikuwa kubwa vile kwamba kama ningekwenda bila shaka
ugomvi na vita vingalitokea. Licha ya hasira wakati wa
mitihani ulikuwa umekaribia, nami nikiwa mwaka
wa pili nilipaswa kufanya vizuri ili kuingia mwaka wa tatu.

Miezi miwili ilipita. Na baada ya mitihani nilikata shauri
kwenda nyumbani nikiwa na wazo la kutafuta kazi ya muda

26

kama ikiwezekana. Wakati huu sikuwa na habari kwamba
Manase alikuwa amekwisha hamishwa.

Nikiwa ndani ya stima kuelekea nyumbani kisiwani,
hadithi hii yote ilinijia kichwani tena. Nilitoa ile barua
niliyoandikiwa na ndugu yangu. Niliisoma tena kwa makini
kuona kama kulikuwa na uwongo ndani yake. Niliona wazi
kwamba Manase alikuwa akisema uwongo. "Manase anamwa
ndugu yangu malaya!" nilisema moyoni. Niliikunja ile barua
nikairudisha mfukoni. Nilianza tena kufikiri jinsi ya kujilipia
kisasi. Nilikumbuka kwamba nilikuwa nimekata shauri
kufanya maisha yake yawe magumu hapa duniani.

Watu walipoanza kuinuka waliniondoa katika ndoto.
Nilipotazama nje niliona kwamba mji wa Nansio ulikuwa
umekaribia. Niligundua kwamba hata stima ilikuwa
imekwisha punguza mwendo. Baada ya dakika tano tulifika.
Nilipotoka nje nilikwenda nilikwenda mara moja kwenye kituo cha
basi. Kwa nauli ya shilingi moja nilipanda basi lililokuwa
likipita katika kijiji cha kwetu-Mahande. Kutoka barabarani
pale basi liliponishusha, ulikuwa mwendo wa kilometa moja
kufika nyumbani. Njiani nilikutana na watu wengi; ajabu
ilikuwa kwamba kila mtu niliyekuwa nikikutana naye njiani
alinitazama kwa mshangao hata wale walionifahamu. Mtu
wa kwanza kuzungumza naye alikuwa kijana mmoja
tuliyekuwa tukisoma pamoja zamani. Yeye sasa alikuwa
ameoa na alikuwa na watoto watatu.

"Wewe kwa nini umekuja nyumbani?" aliniuliza kwa
mshangao bila hata kunisalimu kwanza.

"Kwa nini? Mbona huwa nakuja nyumbani karibu kila
likizo?"

"Heri ungebaki huko. Huku umejileta hatarini."

"Hatari gani?"

"Hatari gani? Hujui?

27

"Hata sina habari!"

"Ndugu yangu, utasimuliwa nyumbani."

Aliponiambia maneno haya ya mwisho alikwenda zake.
Sikupata nafasi ya kuweza kumwuliza zaidi. Lakini nilianza
kufikiri moyoni ni mambo gani aliyokuwa akizungumzia.
Sikuweza kuelewa.

Mtu wa pili kukutana naye alikuwa mzee. Mzee huyu
alikuwa akipeleka ng'ombe wake mtoni kunywa maji.
Alikuwa ameenea vumbi nyweleni.

"Kazimoto! Umekuja kujionea mwenyewe!" alisema.

"Kuona nini?"

"Ha! Huna habari?"

"Hata sina!"

"Mambo fulani yametokea pale nyumbani kwenu ambayo
yameshangaza kijiji kizima cha Mahande."

Nilianza kufikiri kwamba mimba ya ndugu yangu
ndiyo ilikuwa ikikanganya kijiji kizima. Lakini kwa wakati
huu hili halikuwa tena jambo la ajabu kama zamani. Lilikuwa
limekwisha tokea kwa wasichana wengi kijijini, wasomao na
wasiosoma. Zaidi ya hayo kwa njia gani mimba ya ndugu
iliweza kuniweka hatarini?

Nilikuwa nimekaribia kisima walichokuwa wakikoga na
kuteka maji wanawake wa kijijini. Njia hii ilikuwa ikipita
karibu sana na kisima hiki. Nilipokaribia karibu kabisa,
nilisikia sauti za wasichana. Kama ilivyo desturi, nilipiga
kelele.

"Vaeni nipite!"

"Nani wewe?"

"Vaeni wanaume tupite!"

"Ngoja kidogo!" walijibu. Baada ya muda nilisikia, "Tayari!"

Nilipojitokeza walikuwa bado hawajavaa. Nilipita na
sanduku langu, sasa begani, hali nikitazama pembeni.

28

Niliwasikia wakicheka. Lakini mimi sikuwatazama. Nilisikia
wakimwambia msichana mmoja: "Furahi basi! Bwana yako
amekuja!"

"Sasa mnataka nini?" msichana yule aliwajibu.

"Mbona sanduku lataka kumwangusha na wewe huendi
kumpokea?"

Nilifahamu huyo msichana alikuwa nani. Hata nilipokuwa
nimefika mbali kidogo niliweza bado kusikia sauti zao.
Walikuwa wakicheka. Niliona kwamba sasa wakati wa
kusahau vitabu ulikuwa umeingia na kwamba nilikuwa
nimeyafikia maisha yanayoitwa "maisha".

Njia ya kwenda nyumbani kwetu ilipita nyumbani kabisa
kwa Mzee Kabenga - baba'ke Manase. Nilimkuta Kabenga
amekaa juu ya kichuguu kilichokuwa karibu na mji wake,
fimbo mkononi, akitazama ng'ombe wake wawili wakila
majani.

"Kazimoto," alisema kwa unyenyekevu, "sisi tu wazima,
lakini mambo yanayotokea nyumbani kwenu hapo
yanatushangaza."

"Mambo gani?"

"Wewe nenda tu nyumbani. Baba yako hutamkuta, lakini
nafikiri mama yako ataweza kukueleza."

"Amekwenda wapi?"

"Hayo pia mama yako atakueleza."

Nilipokuwa nazungumza na Mzee Kabenga sauti yangu
ilikuwa imesikika nyumbani. Niliwaona wadogo zangu
wanakuja mbio kama kwamba atakayekuwa wa kwanza
kunifikia atapata zawadi. Mara moja sanduku langu
lilichukuliwa juu juu. Wengine hawakupata mzigo.

"Mimi ndiye nilikuwa wa kwanza kumwona."

"Mimi nilimsikia zamani!"

29

"Baba amekula kuku wako wote; alikuwa anasema
kwamba ukifika tukwambie kwamba wameliwa na bweha!"

"Machungwa yameiva; mwaka huu mengi sana!"

Mwishowe nilikata shauri kuzungumza nn mmoja tu kati
yao yaani Kalia, mtoto ambaye nilikuwa nampenda sana
kati ya wadogo zangu.

"Baba yupo nyumbani?" nilimwuliza Kalia.

"Baba! Nyumbani hayupo!"

"Amekwenda wapi?"

"Sisi hatukuambiwa."

"Nyumbani kuna mambo gani?"

"Siku hizi hatulali!"

"Kwa nini? "

"Utaona leo usiku. Siku hizi wanafika karibu kila siku."

"Watu gani?"

"Watu gani? Nani anawafahamu? Hakuna ambaye amekwisha waona."

"Wewe, Kalia, endelea tu kusemasema mambo hayo. Wewe
ndiye utapigwa leo," wenziwe walimwonya.

"Nani atawapiga?" niliwauliza. Wote walinyamaza.

Tulikuwa tumefika nyumbani. Kuingia tu niliona kwamba
kulikuwa na mambo fulani ambayo yalikuwa hayaendi sawa.
Kila mtu alikuwa na huzuni. Kila mtu alikuwa akitembea pole
pole kama mgonjwa, wala hapakuwa na mtu aliyefurahia
sana kufika kwangu nyumbani kama ilivyokuwa kawaida
nyakati zingine. Hata Mama hakufurahi.

Nilipomwona dada yangu Rukia na tumbo kubwa, fikara
kwamba Manase alikuwa amemharibia maisha yake ya mbele
zilinijia kichwani. Alinisalimu kwa mbali hali ameinamisha
kichwa. Hakujaribu kunitazama usoni. Mimi niliona kwamba
tatizo la Rukia ndilo lilikuwa bila shaka tatizo lililokuwa
likiwasumbua. Lakini baada ya kusalimiana na Mama

30

aliyekuwa amekaa juu ya ngozi ya mbuzi kwa huzuni,
nilishangaa kuona kwamba hakuzungumza juu ya tatizo hili
la Rukia. Badala yake alianza kuniuliza kwa nini nilikuja
nyumbani.

"Hufahamu kwamba sisi wote hapa maisha yetu yamo
hatarini? Kwa kuwa wewe umesoma nafikiri we ndiwe
utakuwa wa kwanza kuuawa."

"Kuuawa na nani?"

"Ungekuwa mtu mwenye kusikia maneno ya watu
ningekwambia urudi huko ulikotoka."

"Kwa nini?"

"Hayo si mambo ya kuuliza."

"Na Baba amekwenda wapi?"

"Nitakueleza kesho pumzika kwanza."

Wakati huo huo niliona moshi unaanza kutoka jikoni na
Rukia alikuwa humo amekaa karibu na mafiga.

Nilipomaliza kula nilianza kufungua sanduku langu ili
kutoa matandiko na kutayarisha kitanda. Nilikuwa nikipanga
vitabu vyangu mezani niliposikia mtu akibisha hodi.
Nilifungua. Kabenga akaingia.


"Karibu, Kabenga, karibu," nilisema.

"Asante, mwanangu," alijibu.

"Karibu kiti, usiogope."

"Vitabu hivi vyote umekwisha vimalizia kichwani?"
aliuliza huku akikaa.

"Mbona nimekuja na vichache tu, vingine nimeviacha
huko huko shuleni."

"Mm! Mna kazi!"

"Kazi tunayofanya ni kubwa mno; ngumu kama ya
jembe."

"Ah, mtoto wangu, usiseme kazi ya jembe. Kazi ya jembe
inamnyofoa mtu hata anakuwa mzee siku si zake."

31

"Sisi jembe letu ni kalamu."

"Kweli, lakini kalamu haimfanyi mtu akatoka jasho."
Alinyamaza kwa muda mfupi. "Kazimoto," alianza tena,
nimekuja kuuliza kama una habari yo yote kuhusu mtoto
wetu.

"Mtoto gani?"

"Huyu mwenda wazimu," alijibu.

"Manase?"

"Huyo huyo."

"Kwa nini unamwita mwenda wazimu?"

"Kazimoto, hata wewe unafahamu. Mambo aliyoyafanya
hayakutupendeza, mimi pamoja na wazazi wako. Wewe fikiri,
watu tumesikilizana namna hii kwa muda mrefu, halafu Manase
anatenda jambo kama hili!"

"Hata mimi niliposikia nilishangaa," nilisema.

"Ni mwenda wazimu. Ninakwambia ukweli ni mwenda
wazimu. Tena kabla ya kuendelea ningependa utusamehe
kwa mambo aliyoyatenda. Ni mwenda wazimu! Wewe tazama -
ndugu yako alipokuja nyumbani na kutueleza yote
yaliyotokea, mimi pamoja na mke wangu Tuza na wazazi
wako tulikata shauri amwoe. Tulimwandikia barua, na wote
tuliweka sahihi zetu. Mimi nilianza kazi ya kuposa. Barua ya
kwanza tuliyopata kutoka kwake ilisema kwamba atafikiri.
Hii hapa, unaweza kuisoma." Niliisoma.

"Umeona?"

"Ndiyo."

"Sasa, baada ya muda tulimwandikia tena barua tukimwuliza
kama alikuwa amekwisha kata shauri. Kusema kweli
tulimwambia wazi kwamba hapakuwa na haja ya kukata
shauri: alikata shauri siku ya kwanza alipoanza mambo hayo.
Lakini barua aliyotuandikia tena ilikuwa ya kijinga. Isome
mwenyewe, mimi siwezi kukwambia maneno ya kijinga kama

32

hayo kwa mdomo wangu." Niliichukua na kuisoma.
Haikuwa ndefu:

Ninawaarifuni kwamba kwa sababu fulani kubwa
siwezi kumwoa Rukia. Nimekwisha pata mchumba
mwingine, na mzuri kuliko Rukia. Kama nia yenu ni
kutaka mimi nioe, semeni tu, nami nitawaambia
mahali anapoishi ili muanze kazi ya kuposa. Lakini
Rukia siwezi.

"Umeona sasa kijana mwenzio!"

"Nimeona."

"Sasa sisi hatufahamu jambo la kufanya. Lakini siwezi
kuamini kwamba mtoto wangu Manase anaweza kuharibu
uhusiano wetu mzuri kati yangu na baba'ko. Vijana vya siku
hizi! Eti mpaka mjichagulie wenyewe! Msichana mzuri
huonekana na watu wengi. Hivi ulipokuwa safarini kuja
huku hukupata kuonana naye?"

"Ndiyo, nilimwona."

"Alisemaje?"

"Hata mimi mwenyewe niligombana naye. Anamwita ndugu yangu malaya."

"Unaona sasa! Watu mmesoma pamoja."

"Manase anaonekana kuwa mtu mwenyewe kiburi sana
siku hizi."

"Hicho ni kiburi hakika, na kiburi hakifai." Kabenga
alitikisa kichwa chake kwa huzuni. "Hata kama amekataa
kumwoa msichana huyu, maadam amekubali kwamba mimba
ni yake angekuwa anamtumia pesa za matumizi mbeba mwana.
Lakini mtoto wetu amekataa. Kama angetuma pesa sisi
tungeendelea kumnunulia samaki mpaka atakapojifungua,
maana mtoto ni wetu."

33

Tulinyamaza kwa muda.

"Labda una habari zo zote juu ya binti yangu Sabina,"
aliniuliza.

"Sabina sina habari zake maana huwa hatuandikiani barua."

"Labda naye amekwisha pata mimba, nasikia siku hizi
anafundisha huko Tabora."

"Sabina ni msichana atunzae usafi."

"Dansi ya kushikana wawili-wawili ilipoingia nchini
usafi ukaisha, mwanangu."

"Atakuja lini livu," niliuliza.

"Ametuandikia barua kwamba atakuja mwezi ujao. Mama
yako amekwisha kueleza mambo yanayotokea hapa?"

"Hata kidogo."

"Labda atakueleza baadaye."

"Ni mambo gani hayo?"

"Mambo haya yalianza kuonekana na baba yako.
Alipojaribu kufahamu watu wanaofanya hivyo alipigwa.
Baadaye alikuja kuniambia mimi. Tukiwa wawili tulijaribu
kuwatafuta kwa mikuki lakini kila mara nilipokuwapo
hawakuonekana. Ni wajanja sana."

"Mimi nitajaribu kuwapiga," nilisema.

"Wewe bado mtoto mdogo, afadhali usijaribu, watu hao
wana nguvu sana.

"Wana nguvu sana!" nilistaajabu.

"Ndiyo. Mambo yenyewe si ya kuambiwa, Kazimoto,
utayaona mwenyewe karibuni. Kijiji kizima kinafahamu."

"Kuna habari fulani ambazo zimenishangaza sana," nilisema.

"Habari gani?" Kabenga aliuliza.

"Nimesikia kwamba Manase atamwoa Vumilia karibuni.
Kabenga alishangaa. Hakuwa na neno la kusema kwa muda.

"Hayo pia nilikuwa nataka kukwambia. Mimi huwa sifichi
jambo lo lote," alisema.

34

"Nieleze, nilimwambia.

"Kwanza nikuulize swali moja," alisema.

"Uliwahi kusikia kwamba Manase ana kimada?"

"Nimesikia kwamba siku hizi ni kama ameoa."

"Jina la msichana huyo nimelisahau kidogo lakini ni jina
kama Salima."

"Salima! "

"Ndiyo, Salima. Sasa tuliposikia kwamba mtoto wetu
amepotoka na kwamba anataka kuoa mwanamke kutoka
mbali tulikata shauri kumtafutia mchumba mwingine. Mke
wangu Tuza akatoa wazo kwamba tumchumbie Vumilia kwa
sababu tuliona alikuwa hawezi kushaurika kumwoa Rukia.
Unaona?"

"Nimeona."

"Hata Manase naye tumemwandikia barua amekubali
kumwoa Vumilia. Kama mambo yakienda vizuri nafikiri
atamwoa baada ya miezi miwili."

Kabenga aliyasema maneno haya hali akiinuka
kwenda nyumbani kwake. Giza lilikwa limekwisha ingia. Aliniacha
mimi na mawazo mengi.


Ilikuwa usiku tunakula na wadogo zangu karibu na moto.
Wanawake walikuwa wakila jikoni, niliposikia mbwa wanaanza
kubweka hali wakitazama upande kulikokuwa mwembe.
Niliona watoto wanaanza kutetemeka kwa hofu. Wanawake
jikoni walikaa kimya.

"Kuna nini?" niliuliza. Watoto walinyamaza.
"Sh! Kamata!" niliwahimiza mbwa wawili. Hapo hapo
nilisikia sauti ya Mama kutoka jikoni.

"Kazimoto! Unataka kufanya nini? Wewe nyamaza tu!
Sikutaka kusikiliza maneno ya Mama. Niliinuka. Nilikwenda

35

chumbani kwa Baba kuchukua mkuki.

"Sh! Kamata!"

Mbwa waliponiona nakuja na mkuki mara moja walikimbia
kuelekea kwenye mwembe, mimi nikawa nawafuata nyuma.
Kwa kuwa nilikuwa nimekaa kwenye moto kwa muda mrefu,
sikuweza kuona vizuri. Nilikuwa sijafika mbali niliposikia
mbwa mmoja aliyekuwa ametangulia anabweka. Nilimwona
anarudi akichechemea, mguu mmoja juu, huku akilialia kwa
maumivu. Mbwa wa pili alikimbilia miguuni mwangu. Wadogo
zangu walikuwa wamekwisha kimbilia jikoni. Hofu kubwa
ilinipata kama kwamba simba wa Tsavo walikuwa mbele
yangu. Hofu yangu ilikuwa kubwa zaidi kwa sababu sikuwa
na bunduki, na wala sikufahamu hatari iliyokuwa mbele
yangu ilikuwa kubwa kiasi gani.

"Umeona?" Mama alisema. "Unafikiri wewe mwanamume
kuliko baba yako?"

Nilirudisha mkuki mahali nilipoutoa. Nilikwenda ndani ya
nyumba yangu kulala. Nilipofika kitandani nilianza kufikiri:
"Haya ndiyo mambo niliyokuwa nikiambiwa. Hao ndio watu
wanaosemekana kuwa na nguvu. Lakini kwa nini wawe
wanakuja nyumbani kwetu tu? Sijui nifanye jambo gani ili
niweze kuwakomesha! Siamini kwamba kuna wachawi
duniani. Lazima tu wawe watu wa kawaida. Na ni watu
ambao wanaishi kijijini humu humu."

Niliona kwamba watu wote wa nyumbani kwetu walikuwa
wamekwisha nyang'anywa utu wao, hapakuwa na mtu tena
pale nyumbani. Sikutaka kugeuzwa na hofu kama wao; wao
walikwisha kuwa watu ambao hawawezi hata kuguna.
Niliona kwamba kazi kubwa iliyokuwa ikinikabili sasa ilikuwa
siyo ya Rukia lakini kufikiria njia ya kuweza kuwakomesha
watu hawa waliokuwa wakiuchezea mji wa kwetu.

36

Usingizi ulikuwa bado kunipata wadogo zangu walipokuja
kulala chumbani ndani ya nyumba yangu. Rukia alikwenda
kulala na Mama ndani ya nyumba ya Baba. Usiku wa manane
nilisikia vishindo nti! nti! kuzunguka nyumba yangu.

Hofu ilinishika lakini nilipiga moyo konde. Niliamka
kwenda kuchungulia dirishani. Mara vishindo vilikoma, lakini
sikuweza kuona mtu ye yote. Vishindo vilipoacha kusikika
nilikwenda tena kulala kitandani. Nilikuwa bado sijajifunika
niliposikia ndani ya nyumba ya Baba, Rukia na Mama
wakipiga mayowe: "Tumekufa ! Tumekufa! "

Mara moja nilitoka nje na shuka yangu pamoja na panga
maana mimi ndiye mwanamume peke yangu niliyekuwa
nikitegemewa. "Kuna nini?" niliuliza. Nilipofika karibu na
nyumba nilisikia watu kama wawili wakikimbia. "Fungueni
mlango!" Walifungua, nikaingia: Niliona mchanga mwingi
sana juu ya vitanda.

"Basi - " Mama alisema, "mchanga huu ulikuwa ukimwagika
kama mvua kupitia dirishani.

"Ondoeni mchanga mlale," niliwaambia. Walifanya hivyo.

Niliondoka kwenda nyumbani mwangu. Nilikuwa bado
sijafika niliposikia wadogo zangu wanalia. Nilipoingia tu,
mchanga haukumwagwa tena.

Nilikata shauri kulala na kuwaacha wafanye mambo yao.
Sikusikia vishindo tena nilipolala kitandani. Kwa muda
nilifikiri juu ya maajabu haya, lakini mwishowe usingizi
ulinichukua mpaka asubuhi nilipoamshwa na Kalia.

Wakati nikipiga mswaki asubuhi nilitembeatembea
kuzunguka mji nikitazama chini. Niliweza kuona nyayo za
watu, lakini sikuweza kuzitambua. Nilipofika chini ya
mwembe niliona nyayo nyingi. Ilionekana kwamba hapo
ndipo walipokuwa wamesimama.

Siku nzima sikuwa na raha. Nilikuwa nikifikiria jambo la

37

kufanya. Hata chakula cha mchana sikula vizuri. Baada ya
kula nilijaribu kusoma hadithi lakini niliona kwamba
nilikuwa siifuati. Nilitupa kitabu juu ya meza, nikachukua
sabuni kwenda kuoga mtoni. Niliporudi nilianza kuchana
nywele zangu, mara nikamwona Kalia anaingia chumbani
mwangu hali akitabasamu.

"Umefurahia nini?" nilimwuliza.

"Yuko pale."

"Nani?"

"Yuko pale! Husikii!"

"Lakini nani?"

"Yule wako."

Mara moja nilifahamu, maana Kalia ndiye tulikuwa
tukimtumia kama posta yetu.

"Anafanya nini?" nilimwuliza.

"Anakungoja."

"Amesema hivyo?"

"Ndiyo, ameniambia kwamba ametangulia."

"Ametangulia wapi?"

"Amesema pale mahali penu pa kawaida."

"Asante, Kalia, nitakwenda sasa hivi."

"Amesema usikawie sana."

"Haya."

Kalia aliondoka chumbani anakimbia kuwaona wenzake
ambao walikuwa wakimpigia miunzi waende mtoni kuoga.
Nilipomaliza kuchana nywele nilifungua sanduku na kutoa
kitambaa cha gauni. Nilikikunjia ndani ya karatasi na
kuondoka kabla ya Mama kuniuliza mahali nilikokuwa
nakwenda. Maswali ya Mama kuhusu kokote nilikokwenda
yalikuwa yamekwisha niudhi.

Mahali petu pa kawaida hapakuwa mbali sana. Lilikuwa ni
shamba la mihogo mbali kidogo na nyumbani kwetu. Mwenye

38

shamba hili alikuwa mvivu kupalilia; kama angekuwa na
nguvu za kupalilia mahali petu pangekuwa wazi. Lakini kwa
mshangao nilikuta mihogo yenyewe imekwisha chimbwa na
mahali petu palikuwa wazi kama uwanja wa mpira. Nilikuwa
bado nikishangaa nilipoona, mbele kidogo karibu na shamba
jingine la mihogo, msichana amesimama amenipa mgongo,
kanga ilikuwa imeshuka kutoka kichwani kufunika mabega.
Moyo wangu ulianza kudunda; naye aliposikia viatu vyangu
alianza kung'oa vijani na kukata vijiti vilivyokuwa karibu.
Nilipomkaribia nilimshika begani na kujaribu kumgeuza
anitazama.

"Niache," alisema huku akicheka.

"Kwa nini?"

"Unaponishika unaniumiza."

"Mimi nakutazama tu."

"Kwani hujaniona, au labda umenisahau "

"Vumilia, habari ya siku nyingi?"

"Hali yangu nzuri kama mti usioliwa na mchwa."

"Mti usioliwa na mchwa una nini?"

"Unafanya nyumba isianguke mapema," alisema. Halafu
aligeuka kunitazama. "Kazimoto, mimi mzima kama shilingi
ya masikini iliyosahaulika mfukoni."

"Sielewi."

"Hata barua hamna!" Nilikosa la kujibu.

"Mama yako amefika? Tulikuwa naye kisimani."

"Amefika."

"Ndiye ameniambia kwamba alikuacha nyumbani wakati
alipoondoka; na jana je, ulifika salama? Tulikuona na sanduku
zito."

"Kwa nini hukuja kunisaidia?"

"Acha," alisema pole pole, "watu wanakuja."

"Niache nini?"

39

"Ninasema acha; mimi hayakunileta hayo."

"Acha mchezo," nilimwambia kwa ukali kidogo.

"Mwenye baridi ndiye ajongeaye moto. Wewe ulipaswa
kuja kabla yangu."

"Nilikuwa nataka kumtuma Kalia. Uliniwahi kidogo tu."
Alinitazama.

"Vumilia, kweli tuondoke hapa, tumesimama njiani."

"Tangulia," aliniambia.

Nilitazama kila upande wa njia, halafu niliingia mihogoni
hali nimeinama. Wakati huo nilikuwa nimesahau uanachuo.
Nilipofika katikati ya shamba nilikaa. Nilianza kung'oa
majani ili kutayarisha kitanda. Kwa muda wa dakika tano
sikusikia kama Vumilia alikuwa anakuja. Baada ya muda
nilimwona anakuja.

"Kwa nini umekawia namna hii?" nilimwuliza.

"Ulipotoka tu baba yako akapita. Anasema anatoka safari."

"Ameniona?"

"Hata!"

"Mbona unakaa mbali namna hii? Huoni?" Nilimwonyesha
majani yangu.

"Mm!" aliguna na kupandisha mabega juu kama alama ya
kukataa.

"Umesema mwenyewe - mwenye baridi ndiye ajongeaye
moto," nilisema. Niliinuka kwenda karibu naye. Nilianza
kumpapasa kiunoni. Nilianza kumvua nguo.

"Acha nivue mwenyewe!" alisema.

"Upesi kabla majani yetu hayajakauka."

Muda ulikuwa mfupi. Ilikuwa baada ya muda huu
nilipotambua kwamba majani tulikuwa tumekwisha yaacha
pembeni, na kwamba mti mmoja wa mhogo niliokuwa
nimekanyaga ulikuwa umeng'oka. Nilianza kumkumuta
mchanga kichwani.

40

"Kazimoto, unafahamu livu hii tunaagana!"

"Bado sijafahamu sawa sawa."

"Mpango wangu wa ndoa umekaribia kutekelezwa.
Nafikiri baada ya miezi miwili!"

"Bahati mbaya sana."

"Kwa hiyo utakapokuwa unakuja kunichukua usiku fika
kwa uangalifu, kwa sababu siku hizi Mama ananichunga sana.

"Nitakuja kukuchukua Jumamosi," nilimwambia.

"Jumamosi hapana."

"Kwa nini?"

"Sina nafasi siku hiyo; fika Jumapili."

"Haya nitakuja. Nilikuwa na zawadi kidogo ya kukupa."
Nilimpa kile kitambaa. Aliifungua upesi ile karatasi.
Alikiona. Alitabasamu.

"Asante sana," alisema. "Nafikiri kimekugharimu shilingi nyingi.

"Thelathini na tano tu."

"Thelathini ni pesa nyingi sana." Alikitia ndani ya kanga.
"Nakwenda. Kwa heri," alisema.

"Unapita wapi?" nilimwuliza.

"Huku."

"Mimi napita huku."

Kila mtu alishika njia yake na kutopa upande mwingine
wa shamba. Nilipofika nyumbani nilikuta kweli Baba amekaa
"Tutayazungumza kesho," alisema. Baada ya kumsalimu
nilikwenda nyumbani mwangu. Nilikuta Kalia amekwisha
toka mtoni. Alikuwa akitumia shanuo langu. Nipoingia aliguna.

"Kwa nini unaguna?" nilimwuliza.

"Hata mimi naona tu," alisema.

"Unaona nini?"

"... kwamba yule msichana ulimwona."

41

"Umefahamuje?"

"Tumekutana naye njiani anatoka huko huko ulikokuwa.
Alikuwa amefurahi sana. Mara kwa mara huwa anatuuliza
utakuja lini." Alinyamaza kwa muda.

"Ngoja niweke wei halafu nikupe mambo yako," alisema.
Alijaribu kuweka wei aliyokuwa anasema. Alipomaliza niliona
kwamba wei aliyoweka ilikuwa imejipinda kama alama ya
vema. Alichukua kitabu changu kimoja kilichokuwa mezani,
na humo alitoa barua.

"Hii barua yako. Nilikuwa nayo hata kabla hujaenda
kumwona. Lakini alikuwa ameniambia nikupe baada ya
kuonana."

Niliifungua kwa haraka. Bila kutegemea, poda nyingi
ilimwagika juu ya kitanda changu na kipande kidogo cha
karatasi kilitoka. Kalia alitoka nje huku anacheka. Nilimsikia
akiwaeleza wenziwe nje.

"Kalia, nitakupiga!" nilimwambia. Lakini Kalia alicheka
tu na kukimbilia nyumbani kwa Kabenga kula machungwa.
Nilisikia Kabenga akimwambia Kalia angoje mpaka kesho,
kwani ilikuwa haifai kula machungwa jioni.

Kalia alikuwa kijana ambaye mara nyingi aliweza
kuzungumza nami kama mwenzangu ingawa alikuwa na umri
wa miaka kumi na mitano tu. Tulikuwa tumezoeana, naye
alikuwa haniogopi tena. Mimi mwenyewe nilipenda kutembea
naye; wasichana wangu wote aliwafahamu na matendo yangu
nao aliyaona. Yeye pia alipenda sana kunifuata. Mara fulani
nilikuwa namrudisha nyumbani hasa nilipokuwa na safari
ya kwenda mbali. Alizoea kusikitika, kwa hiyo nikawa
namtoroka. Kalia alimaliza darasa la saba tu. Aliposhindwa
alianza kujishughulisha nyumbani na takataka; mwishowe
akawa fundi wa kushona viatu na kunyoa.

Kalia alipokimbia nilifungua kile kijikaratasi ili kusoma

42

ujumbe uliokuwamo. Niliona msitari mmoja tu: "Ninaomba
tupendane."

Giza lilikuwa limekwisha ingia na niliona Baba akikoka moto.
Furaha yangu ilipungua nilipokumbuka yale mambo
yalioyokuwa yakitokea nyumbani kwetu usiku. Niliona
kwamba hata mimi hofu ilikuwa imekwisha anza kunitawala.
Siku hiyo tulikula bila kusikia vishindo vyo vyote,
hata mbwa hawakubweka.

"Umekwisha zungumza na ndugu yako?" Baba aliuliza
baada ya kula.

"Bado," nilijibu.

"Jibu lako nililifahamu. Kazimoto, mambo ya wasichana
yamekuingilia vile kwamba watu wa nyumbani umewasahau."

"Mambo ya wasichana sihusiani nayo."

"Unasema nini? Mtoto gani wewe? Unataka kunidanganya
mimi? Kazimoto, uwongo huu wote uliupata wapi? Unafikiri
mimi sikukuona unanyatia mihogoni?"

"Basi, basi Baba, nisamehe," nilisema upesi.

"Ndiyo, Kazimoto, ukitaka kuwa rafiki yangu sema ukweli
daima."

"Ndiyo uliniona," nilisema.

"Kwa kuwa hufahamu habari za hapa nyumbani, basi mimi
nitakuambia. Kazimoto, tangu ufike hapa ndugu yako
amekataa kula,"

Alipomaliza kusema maneno hayo aliinuka kwa hasira
kwenda kulala na kuniacha mimi nikishangaa. Nami niliinuka
kwenda jikoni alikokuwa amekaa Mama na Rukia. Nilipoingia
jikoni nilimkuta Mama anakula; lakini niliona kwamba
hakula chakula kingi maana ugali ulikuwa umenyofolewa
mara tatu tu. Nilimwona Rukia amelala chini juu ya kanga,
kichwa chake amekiweka juu ya miguu ya Mama. Mama
alikuwa akimpangusa kwa kanga machozi yaliyokuwa

43

yakitiririka kila wakati.

"Rukia," nilimwita pole pole. "Rukia," niliita tena.
Hakuniitikia. Nilijaribu tena. "Rukia, jaribu kula chakula
kidogo." Hakuniitikia. Badala yake alianza kulia kwa kelele.

"Kazimoto," Mama alisema. "Kazimoto, tuache tupumzike,
tuache tulie. Huu ni ugonjwa umeletwa na vijana na utatuma-
liza sisi kina mama wenye mabinti. Ninajiona kwamba
nitakwenda pamoja na binti yangu."

Machozi yalimlengalenga. Niliona hapa hapa kuwa mahali
pangu. Niliondoka pole pole nikawaacha wanalia wote pamoja
huku wamekumbatiana.


Kesho yake asubuhi Kalia ndiye aliyeniamsha. Nilipokuwa
nikipiga mswaki niliwaona Kabenga na mkewe wakiongozana
kuja nyumbani kwetu. Kwa kuwa kulikuwa na baridi bado
wote walikuwa na shuka mabegani. Walipofika ndani ya
nyumba ya Baba, niliwasikia wakiuliza habari ya Rukia.
Mama aliwajibu kwamba mgonjwa aliomba uji asubuhi.
Walifurahi na kusema kwamba maadam ameanza kunywa uji
karibu atakula chakula cha kawaida. "Tunamwombea apone,"
walisema. Nilipomaliza kuvaa nilistukia kumwona Kalia
anakuja chumbani mwangu.

"Kazimoto, unaitwa na Baba."

"Wapi?"

"Ndani ya nyumba yake. Amesema harakisha."

Nilikwenda. Nilipofika chumba cha mazungumzo nilikuta
kiti kimoja kimebaki kwa ajili yangu. Kabenga na Baba
walikuwa pia wamekalia viti. Tuza na mama yangu walikuwa
wamekaa chini.

"Kazimoto," Baba alianza kuzungumza, "tumekuita ili
tujadiliane juu ya mambo ambayo hata wewe mwenyewe
umekwisha yaona. Yalipotokea, mimi pamoja na Kabenga

44

tuliona hawa hawakuwa watu wengine isipokuwa wachawi.
Nilifunga safari kwenda nchi za mbali kuwaona waganga.
Huko waganga wameniambia wazi kwamba ni kina Masesa
na watoto wake. Hawa ndio watu ambao huwa wanakuja
hapa usiku. Na sababu yenyewe nimeambiwa kwamba ni
mashamba. Unafahamu kwamba sisi tuliletwa hapa na
serikali, ingawa kweli tumekaa kwa muda mrefu. Sasa Bwana
Masesa anataka tuhame ili achukue tena mashamba yake."

"Masesa anaishi wapi?" niliuliza.

"Ni kaka yangu," Kabenga alijibu, "isipokuwa yeye anaishi
katika kijiji kifuatacho cha Kigara."

"Kwa hiyo mashamba haya ni yenu?" nilimwuliza Kabenga.

"Ni yetu ndiyo, lakini mimi sina matata."

"Sasa tufanyeje?" Baba aliuliza.

"Hata mimi nimo hatarini," Kabenga alisema, "kwa hiyo
mimi naona afadhali tupeleke mambo haya barazani."

"Barazani kama kwamba tumekwisha waona!" Mama
alisema.

"Wachawi hatuwezi kuwaona," Tuza naye alijitokeza.

"Mimi nitawashika," nilisema.

"Wewe!" Baba alishangaa.

"Ndiyo," nilijibu haraka.

"Wachawi wajanja," Kabenga alisema. "Hata sasa
inawezekana wapo hapa wanatusikiliza."

Hapo ndipo nilipowaambia maneno niliyoambiwa na
padri mmoja:

"Kuwashika wachawi ni jambo rahisi sana," nilianza.
"Jambo moja kuhusu wachawi ni kwamba wana pua kali sana
kama wanyama. Wanafahamu sana harufu ya mwanadamu,
kwa sababu mtu ambaye huota moto ana harufu ya pekee.
Wachawi wakitaka kwenda kutembea usiku hawasogelei
moto muda wa siku tatu nne; halafu wakitoka nje usiku

45

huvaa nguo ambazo huwa zimetunzwa nje majanini ili
kupoteza harufu kwa umande. Wengine huenda uchi. Kwa
hiyo watembeapo ni vigumu kuwaona. Ukitaka kuwaona
fanya kama wao."

"Labda kuna ukweli ndani yake," Kabenga alisema.

"Jaribu," Baba alisema.

"Leo," Mama alisema.

"Mimi sidhani kwamba atafanikiwa," Tuza alisema.

"Leo haiwezekani," nilijibu, "kwa sababu nguo zangu
lazima zikae nje kwa muda wa siku kadhaa."

Mkutano ulipokwisha, wote walikubali kwamba nijaribu.
Kwa muda wa siku tatu sikukaa karibu na moto na mara
nyingi mchana nikawa nakaa kivulini ili kupoteza harufu
yote ya kibinadamu. Nguo za kaniki zilipelekwa majini.
Mwishowe siku ambayo nilikuwa nimeahidi kuwavizia ilifika.
Nilitengeneza kiti cha kamba juu ya mwembe ambao, chini
yake, nilizoea kuona nyayo zao. Ilikuwa siri kubwa, hata
wadogo zangu nyumbani hawakufahamu isipokuwa sisi
watano. Siku hiyo Kabenga alikuja kulala kwetu ili kuona
yatakayotokea. Siku hiyo nilikula chakula cha jioni kama
saa kumi na mbili. Baada ya kula nilipanda mtini pamoja
na upinde, mishale minne na mkuki. Usiku huo hawakuja.
Nilifanya hivi kwa muda wa siku tatu, lakini sikufanikiwa.
Kiini cha mambo haya kiliendelea kuwa fumbo kubwa.

46

			3

Jumanne, niliondoka nyumbani asubuhi. Nilikuwa na nia
ya kumtoroka Kalia. Rukia alikuwa bado hajaanza kula
vizuri, lakini niliona lazima kwenda kumsalimu rafiki yangu
na kumpa pole kwa maafa yaliyompata. Rafiki yangu,
Kamata, alikuwa akiishi katika kijiji cha Saku. Kamata
alikuwa mmoja kati ya rafiki zangu ambao nilizoea kuwate-
mbelea mara nne au zaidi wakati wa likizo. Yeye alikuwa
ameoa na alikuwa na watoto wawili. Alikuwa na mji wake
peke yake, wenye nyumba mbili, ya kulala na jiko.
Nilipokuwa nikisoma naye katika shule ya msingi, Kamata
alikuwa amenitangulia mwaka mmoja, lakini alishindwa
kuingia darasa la tisa. Aliposhindwa, hakufanya uhuni
wafanyao watoto wengi washindwao darasa la saba siku hizi.
Alitambua mara moja kwamba kazi ya ofisi haikuwa yake
tena. Alikaa miaka miwili halafu akaoa. Mama yake alipofariki,

47

siku chache baada ya harusi, Kamata alishika mji na
kuuchukua. Baba yake alikufa zamani, na Kamata hakupata
kuona sura yake; alikuwa bado mtoto mchanga wakati huo.

Kamata alikuwa mkulima stadi. Alikuwa na shamba kubwa
la migomba; shamba la mpunga karibu na ziwa; kishamba
kidogo cha kabichi na shamba kubwa la viazi. Alikuwa pia
na mitego mitano ya samaki. Alikuwa kijana nadhifu sana.
Wakati alipokuwa hafanyi kazi nguo zake zilikuwa safi daima.
Baiskeli yake ilikuwa ikisafishwa karibu kila siku. Visu vyote
nyumbani vilikuwa na makali daima. Ubaya wake ambao
ulifanya vijana majirani wamchukie kidogo ni kwamba
alikuwa haazimi kitu chake. Hata juu ya baiskeli yake alikuwa
ameandika: "Utaazima Kesho".

Huyu ndiye Kamata, rafiki yangu, ambaye nilikuwa
nikienda kumtembelea. Asubuhi kabisa nilichukua baiskeli
yangu juu juu ili isipige kelele na kumwamsha Kalia ambaye
alikuwa bado usingizini. Nilipoitoa nje nilifunga mlango pole
pole. Baba, Mama, Rukia, sikuwasabahi. Niliondoka bila
kumwambia mtu ye yote mahali nilikokuwa nakwenda.
Ulikuwa karibu umbali wa kilometa tano hivi kutoka
Mahande kwenda Saku. Njiani nilikutana na watu wengi:
wenye majembe; wenye watoto mgongoni na wengine
waliokuwa na safari kama mimi. Niliendesha baiskeli yangu
nikipanda vilima na kushuka. Ule utoto wa kupanda kila
kilima ulikuwa umekwisha ondoka.

Nilifika nyumbani kwa Kamata saa nne. Nilimkuta Matilda,
mke wa Kamata, akichanja kuni kwa shoka. Mtoto mmoja
alikuwa mgongoni, wa pili alikuwa amekaa chini ya kivuli
cha mti, kiazi mkononi. Mji wote ulikuwa umefagiliwa vizuri.

Matilda alitupa shoka chini aliponiona.

"Karibu! Karibu!" alipiga kelele.

"Starehe, Kamata hayupo?"

48

"Hayupo. Amekwenda kuondoa mitego yake majini."

"Atarudi karibuni?"

"Lazima atakuwa hapa kabla ya saa sita."

"Ninakwenda ziwani kumngojea."

"Kaa tu atakuja."

"Ninakwenda kupunga hewa ziwani kidogo."

"Kazimoto, hata wewe unafahamu Kamata alivyo.
Asipokukuta nyumbani atakuja kunikaripia kwamba
sikukukaribisha vizuri."

Baada ya kuzungumza naye kwa muda aliniruhusu kwenda
ziwani. Nilimwacha akiingiza baiskeli yangu ndani.

Nilipofika ziwani nilikuta wavuvi watano wakishona
matundu ya mitego yao. Walikuwa wakifanya kazi hii kwa
haraka sana. Mikono yao ilikuwa myepesi sana. Walikuwa
wakifanya kazi hii hali wakisimuliana hadithi na kucheka
kwa sauti za ajabu.

"Kamata anaweza kuwa wapi?" niliuliza.

"Kamata?" mmoja aliniuliza tena.

"Ndiyo," nilijibu.

"Kuna uzima au msiba?"

"Uzima."

"Wewe nani?"

"Kazimoto."

"Kazimoto?"

"Ndiyo."

"Mtoto wa nani?"

"Mafuru."

"Kijiji gani?"

"Mahande."

"Hapo Mahande unatoka sehemu gani?"

"Karibu na mto."

"Kamata atarudi karibuni. Ameondoka zamani na

49

mtumbwi wake, Wewe mgeni wake, sivyo?"

"Ndiyo."

"Unaweza kukaa hapo mchangani umngoje."

Nilikaa, nikawa nawatazama wanafanya kazi yao. Kijana
mmoja ambaye nilifikiria mjinga kati yao ndiye alikuwa
akisimulia hadithi. Alikuwa kijana mfupi mwenye ndevu.
Meno yake yalikuwa nje daima utafikiri anacheka.

Baada ya kijana huyu kusimulia hadithi yake ambayo
ilichekesha sana watu, kila mmoja alianza kutoa hadithi yake;
zote zilihusu wanawake. Walisema kwa lugha ya matusi vile
kwamba nilianza kufikiri moyoni kama walikuwa wamekwisha
sikia kitu fulani kiitwacho dhambi. Mmoja kati yao alijidai
kwamba kwa wanawake tu alikuwa amebakiza makabila
machache ya nchi hii. Alianza kutaja kila kabila akitoa
kasoro zao. Hapo ndipo nilipoanza kufikiri moyoni kwa
nini nilisoma mpaka Chuo Kikuu. Nilianza kujiuliza kwa nini
nilisoma kile kitabu cha zamani - Biblia. Niliwaonea wivu
wenzangu ambao tuliachana darasa la nne. Wao sasa walikuwa
wakicheza zeze na kupiga vishindo kwa furaha. Niliona
kwamba elimu ilikuwa sumu ya furaha yangu. Kila siku
kusoma vitabu na magazeti nisiwe nyuma ya wakati. Sasa
niliona tofauti kati ya maisha yangu na yao. Kwa wakati huu
wazo la kuacha shule ili niishi kama wao lilinijia kichwani.

Sikuona sababu ya kusumbuliwa na mawazo, kuwa na
wajibu mkubwa zaidi, halafu kufa kama wao na labda
kwenda motoni, wao mbinguni - faida gani?

"Huyo Kamata anakuja," walisema wakitazama ziwani.
Jinsi walivyoweza kuona mtumbwi sijui, maana mimi
sikuweza kuuona.

"Inaonekana kwamba leo hakupata samaki wengi," mmoja
kati yao alisema.

Alipofika karibu niliona mtumbwi wake ukipanda na

50

kushuka juu ya mawimbi. Alipofika karibu sana niliona
kwamba hakuwa na shati kifuani. Mwishowe mtumbwi wake
uligusa mchanga. Kamata alitoka na kusukuma mtumbwi
wake. Alikuwa amekwisha niona.

"Kazimoto! Nisamehe, sikujua! La sivyo nisingekawia
sana huko majini."

"Umefanikiwa?" wavuvi walimwuliza.

"Siku hizi samaki wamekataa kufa," aliwajibu.
Na kweli hakufanikiwa. Wale samaki wachache aliokuwa nao
aliwafunga kwenye ncha mbili za mti. Yeye alisimama
katikati na kuwabeba. Wengi walikuwa bado wazima na
mikia yao ilikuwa ikipigapiga.

"Twende nyumbani, Kazimoto," aliniambia. "Jamani
mtanisamehe nimepata mgeni."

"Lakini utakuja?" wavuvi walimwuliza.

"Wapi?"

"Kule. Umlete mgeni." Walipeana alama fulani ambazo
sikuelewa.

"Ndiyo nitakuja," aliwajibu.

Tuliondoka kuelekea nyumbani. Tulipokuwa njiani Kamata
aliniita "Kazimoto."

"Naam."

"Bila shaka ulikuwa umekwisha sikia mambo yaliyonipata."

"Ndiyo, nilisikia bado nikiwa Dar es salaam. Kusema haki
nimekuja leo kukupa pole kwa yote yaliyokupata. Nilifika
Jumamosi; ingawa Rukia hana hali nzuri nimeona vizuri kuja
kukusalimu mapema."

"Nitakusimulia tukifika nyumbani," alisema.

Tulipofika nyumbani, Matilda alituandalia chakula - ndizi
mbichi ambazo zilikuwa zimepikwa vizuri sana, samaki
wengi sana na viazi vichache. Matilda alikula peke yake
jikoni pamoja na watoto. Baada ya kula Kamata alianza

51

hadithi yake.

"Kazimoto, furahi kuniona sasa. Nilikuwa maiti, na
ninafikiri kwamba sasa ungekuwa unalia karibu na kaburi
langu. Nilikuwa mfu. Hadithi yenyewe ni hivi: Siku moja
vijana wawili walinipitia hapa kwenda kunywa pombe. Vijana
hao ni majirani. Tulipofika huko kwenye pombe tulikunywa
sana. Kumbe wenzangu walikuwa na hila mbaya.
Giza lilipoingia walianza kuwa wanajitilia pombe kidogo,
mimi nikitiliwa pombe nyingi. Mwishowe nilijiona naanza
kulewa. Niliwaomba ruhusa kuondoka, lakini wao walikataa.
Waliahidi kunisindikiza mpaka nyumbani. Niliendelea
kunywa. Karibu kama saa sita za usiku waliniambia kwamba
walikuwa tayari kunisindikiza. Nilijaribu kusimama, nilijiona
bado na nguvu za kuweza kutembea bila kushikiliwa.
Tulipofika mbali kutoka mahali pa kunywea pombe, mmoja
wao alisema: 'Kamata'."

"Nilisimama. Mara niliona kila mmoja kati yao ameshika
rungu. Hofu kubwa ilinishika na pombe yote iliruka. Niliona
mwisho wa maisha yangu hapa duniani.

"'Jamani! Kweli mniue! Mniue kabisa', nilijitetea."

"'Ua kabla hajasema maneno mengi!' mmoja alisema.
Hapo hapo nilipigwa rungu la mgongo. Nilianguka chini."

"'Jamani kweli sasa mmeniua!'"

"Mara moja nilisikia rungu linalia juu ya kichwa changu.
Nilizimia. Kesho yake asubuhi nilipozindukana nilijiona
nimelala ndani ya maji. Majani yalikuwa marefu hata sikuweza
kuona mahali po pote. Akili ziliponirudia sawa sawa nilikaa
kwa muda nikifikiri. Nilikumbuka hadithi kidogo. Niliona
nguo zangu zimeenea damu. Nilipojishika kichwani nilishangaa
kutupa vidole ndani ya shimo. Nilianza tena kuogopa.
Nilijiona maiti tena. Nilijaribu kusimama. Maumivu yalikuwa
mengi mno. Niliposimama niliona kwamba nilikuwa nimelala

52

karibu na ziwa. Nilisikia sauti za watu. Nilijivuta pole pole.
Wale watu waliponiona walistuka, kama kwamba waliona
mzuka fulani. Ndio wale vijana ambao ulikuwa nao ziwani.
Nilipowakaribia walinitambua: "'Kamata! Umekuwaje?'"
waliniuliza.

"Nipelekeni nyumbani nikamwone mke wangu," niliwaambia.

"'Waliponifikisha nyumbani, mke wangu alianza kulia
badala ya kunitafutia maji na kunisafisha.' Wale vijana waliosha
vidonda vyangu. Maumivu yalikuwa makali. Niliomba
nipelekwe hospitali mara moja. Baada ya kuwaeleza kwa
ufupi walinipeleka hospitali ya Bukonyo. Siku hiyo daktari
alikuwa amelala. Nilishugulikiwa na mayaya. Baadaye
tuliambiwa kwamba daktari alikuwa amelewa pombe ya
moshi na alikuwa hawezi kuwaona wagonjwa. Kesho yake
asubuhi daktari aliniona. Nilimweleza kisa chote. Polisi
walipelekwa kuwashika wale vijana ili wawekwe rumande
mpaka nitakapopona. Inasemekana kwamba mtu fulani
aliwaona huko Uzinza Geita wakijiita majina mengine.
Mimi nilikaa hospitali kwa muda wa mwezi mmoja. Tazama
kichwa hiki!" Alinionyesha ngeo yake.

"Kule mtoni ulifikaje?" nilimwuliza.

"Mimi sikuwa na fahamu wakati huo. Lakini inaonekana
kwamba waliponipiga sana na kudhani kwamba nimekufa
waliniburura na kunitupa ziwani. Mungu bariki walinitupa maji
mafu, na badala ya kuanguka kifudifudi nilianguka chali pua
na mdomo juu ya maji. Umande wa usiku pamoja na maji
chini ya mgongo yalinisaidia na kunifanya nizindukane asubuhi.

"Unafahamu kwa nini walitaka kukuua?" nilimwuliza tena.
Kamata alitazama upande wa jikoni. Matilda alikuwa naye
akisikiliza.

"Sababu yenyewe mpaka leo hii sijapata kuielewa vizuri,"
alisema.

53

"Lakini mimi ninafahamu wazi kwamba sijawatendea jambo
lo lote baya," alimaliza. Tulinyamaza kwa muda.

"Kazimoto, utaweza kukaa hapa nasi majuma mangapi?"
aliuliza.

"Ikiwezekana nitarudi leo saa kumi; hiyo ndiyo saa
niliyokuwa nimepanga."

"Labda unataka kunichekesha. Huwezi kuja kuzungumza nasi
kwa muda mfupi namna hii. Lala mpaka kesho. Huu ni
mji wako, Kazimoto."

"Ndiyo - lakini kama nilivyokwambia hapo awali nilimwa-
cha Rukia mgonjwa sana."

"Bado hajajifungua?" Matilda aliuliza kwa sauti.

"Bado."

"Labda atazaa mapacha. Nilimwona majuma mawili
yaliyopita. Tumbo lilikuwa kubwa."

"Sijui wasichana wanafikiri nini,"Kamata alisema. "Ulikuwa
umekazana kumsomesha lakini shukrani yake ni kutojiheshimu.
Nafikiri amekusikitisha sana."

"Sana," nilijibu.

Kamata alitazama jua. Aliinuka. Alijinyosha halafu alipiga -
mwayo mrefu.

"Matilda sisi tunakwenda matembezi. Tutarudi usiku.
Fahamu kwamba tuna mengi."

"Kamata, huo ndio ubaya wako. Sasa unakwenda
kumnywesha mgeni. Yeye atarudi amelewa wewe mzima.
Usimpe mgeni mapombe mengi."

"Kwani mimi nitakuwa namnywesha? Lete kibuyu.
Nitakuletea hata wewe." Matilda alitafuta kibuyu upesi
upesi. Alikileta baada ya kukiosha ndani.

"Twende, Kazimoto." Tuliondoka. Tulipokuwa tumefika
mbali na mji, Kamata aliniita, "Kazimoto."

"Naam."

54

"Sikutaka kukueleza pale nyumbani kisa kilichofanya
nipigwe."

"Ebu nieleze."

"Sababu yenyewe ni kwamba wale vijana walijaribu
kumtongoza mke wangu. Alipowakataa waliona kwamba
alikuwa akiwakataa kwa sababu mimi nilikuwa hai. Kwa
hiyo walikata shauri kuniua. Lakini siku za mwanadamu
kweli zimehesabika. Makumi yangu yaliyokuwa yamewekwa
pembeni na Mungu kwa ajili yangu yalikuwa hayajatimia."

Kamata aliponiambia hivyo niliamini, kwa sababu Matilda
alikuwa mwanamke mzuri sana. Ingawa alikomea darasa la
saba watu wengi wa maana - yaani wenye vyeo vya juu -
walipeleka posa. Uzuri wake ulivuma Ukerewe nzima.
Alipokata shauri kuolewa na Kamata kila mtu alishangaa.
Wazazi wake walijaribu kupinga uchumba huu, lakini Matilda
hakupenda kuolewa na mtu mwingine isipokuwa Kamata.
Mwishowe wazazi wake walikubali, lakini moyoni kitu fulani
kilikuwa bado kikiwachoma. Kwa kutaka kumkatisha tamaa
Kamata walidai mahari makubwa sana. Kamata alikuwa
tayari kulipa, kwani baba yake alipofariki alimwachia pesa
nyingi kutokana na kazi ya uvuvi. Kamata alimwoa Matilda.
Watu wengi walisema kwamba Matilda alivutwa na ule usafi
wa Kamata. Kwa kuwa Kamata mwenyewe alipenda usafi
alimtunza mkewe vizuri sana akawa anaonekana bado
msichana hata baada ya kuzaa watoto wawili.

"Hata mimi zamani nilikuwa na nia ya kuoa msichana
mzuri sana, sasa ninaona kwamba ni hasara," nilisema.

"Unasema uzuri wa sura?" aliniuliza.

"Ndiyo."

"Kwa nini usioe msichana mzuri?"

"Wanaomtamani wanakuwa wengi mno. Kutoka maskini
hadi tajiri."

55

"Labda usemayo ni kweli, Kazimoto; mke wangu
amekwisha nipoanza mara nyingi mno. Na mara hizo zote
nikiponea chupu chupu. Utaoa lini?" aliniuliza.

"Sijapata bado msichana anayenipenda. Ye yote
nimwendeaye ananirusha. Mwishowe nimekata tamaa."

"Usikate tamaa," aliniambia. "Katika kutafuta mchumba
usiogope kushindana. Hata kama alikurusha usikate tamaa.
Mimi mwenyewe wakati nikitafuta mwanamke wa kuoa
nilirushwa mara nyingi sana. Mwishowe nilianza kufikiri
kwamba labda duniani hapa nilikuwa wa mwisho katika
ubaya. Lakini hiyo yote ilikuwa kumbe haraka ya bure.
Wangu alikuwa bado hajaja. Kwa hiyo, Kazimoto, wako yupo
atakuja. Lakini hawezi kujileta kama wewe hujaribu."

"Lakini mimi ninataka kuoa mapema iwezekanavyo;
mwaka kesho kama ikiwezekana."

"Haraka ya nini? Kijana kama wewe na elimu yako hiyo
wanawake utawaona wengi baada ya masomo. Kwa sasa wewe
soma tu. Sisi wakulima na wavuvi tunaoa mapema kwa
sababu ndilo jambo la maana tu tunalofahamu katika maisha
yetu na watu wengine. Lakini wewe elimu bado iko mbele yako. "

"Hakuna huku msichana ye yote asomaye?" niliuliza.

"Huku wanaosoma ni wachache. Wengi wanakomea darasa
la saba. Kama unataka hao ni wengi."

"Nikioa msichana wa darasa la saba lazima awe mzuri
sana."

"Kwa nini?"

"Bila shaka umekwisha sikia kichekesho cha mwanamke
aliyekwenda kwao kwa sababu bwana'ke alisema 'some
coffee to day'."

"Kazimoto, mke ni mke tu. Kwani wale waliosoma
wameongeza nini katika hali yao ya uke? Utalipiga litalia

56

kama buyu."

"Ingawa litalia kama kibuyu, lakini linafikiri na ninaweza
kujadili nalo mambo ya juu yaliyoandikwa na wataalamu."

"Kazimoto, acha mchezo. Mambo ya maana ya kuzungu-
mza na mke wako ni yale yahusuyo aila. Na hayo
hayakuandikwa." Nilisikia mlio wa ngoma na kelele za watu.

"Kuna harusi?" niliuliza.

"Hapana. Hizo ni ngoma ziitwazo Mbugutu; zinachezwa
kwenye pombe, hasa pombe ya ndizi."

"Ndiko tunakokwenda?"

"Ndiyo, tumefika."


Tulipofika wale wavuvi walikuwa wametungoja kwa hamu
sana. Mara tu walipotuona walitukaribisha. Huo ndio
ulikuwa mji wao. Ulikuwa mji mkubwa sana wenye nyumba
kumi. Kama tukihesabu na majiko zilikuwa nyumba kumi na
tano. Mji wote ulikuwa umezungukwa na shamba kubwa la
migomba, na ulikuwa mji wenye mawe mengi katikati. Mawe
haya ndiyo wanywaji walikuwa wamekalia. Wapiga ngoma
walikuwa na mtungi wao mkubwa sana. Mimi na Kamata
tulipelekwa katika kikundi cha wazee. Nafikiri kwamba
hawa wazee walikuwa pia wamekaribishwa kama sisi. Kundi
la vijana na wanunuzi lilikuwa mbali kidogo na wazee. Wengi
kati ya vijana walikuwa wakicheza ngoma. Kulikuwa na
vikundi vingine vidogo vidogo vimetapakaa huko na huko
kati ya migomba. Wanawake fulani fulani walikuwa
wamechanganyikana na wanaume. Wanawake watatu
walikuwa wakicheza ngoma.

Tulipokaa nilimwona yule kijana aliyekuwa akisimulia
hadithi kule ziwani asubuhi, amebeba mtungi mkubwa kati
ya mikono na miguu yake. Aliuweka katikati. Tulimshukuru.
Baada ya kuuwekea mchanga pembeni ili usianguke aliuacha.

57

"Wazee," alisema, "na mgeni wetu ambaye ametujia leo.
Karibuni. Wakerewe walisema kwamba asiye na kiuno naye
huvua. Hiki ndicho nilichoweza kupata."

Wote tulishukuru pamoja. Tulianza kunywa tukifuata
duara. Pombe ilikuwa nzuri, nami niliinywa kwa pupa.

Mazungumzo ya wazee yalianza. Kila mtu alikuwa kimya
na walikuwa wakizungumza mmoja mmoja. Walizungumza
juu ya watemi wa zamani; mwanzo wa makabila na matawi
mbali mbali ya watu wa Ukerewe. Walizungumza juu ya vita
vya zamani; juu ya watu mashuhuri; watu ambao waliweza
kupanda mti hali mkono mmoja wameshika fahali; watu
ambao waliwanyoa wenzao kwa chupa watake wasitake.
Walizungumza juu ya mwanamke aliyesemekana
kaanguka kutoka mbinguni na mkia akazaa watoto na
baadaye akatoweka. Walizungumza juu ya mashindano
ya ngoma kati ya Wakerewe na Wasukuma. Kwa vyo vyote,
mambo mengi yalikuwa mazuri kusikiliza lakini mimi
nilijiona niko nje ya mazungumzo hayo. Niliwauliza
maswali kadhaa, lakini hayakujibiwa vizuri. Baada ya kuchoka
na hadithi zao walinielemea mimi. Walianza kuniuliza
maswali:

"Unasoma wapi?" mzee mmoja aliniuliza.

"Dar es salaam. "

"Rafiki yako alikuwa akisema unasoma Makerere."

"Ndiyo," Kamata alidakia, "nilikuwa nikiwaeleza kwamba
unasoma katika shule kama ile ya Makerere."

"Kumbe wewe umesoma sana," yule mzee aliniambia.
"Sijui kama utaweza kunieleza jambo hili: Uhuru tumekwisha
upata. Zamani mkoloni alikuwa akitengeneza pesa kidogo
kwa sababu alikuwa hataki tuendelee na alikuwa akituonea
katika mambo mengi. Hii haikuwa nchi yao. Yote haya
tumeambiwa na wanasiasa. Sasa uhuru tumepata. Kwa nini

58

Serikali haiwezi kutengeneza pesa nyingi sana kila mtu awe
tajiri?"

Lilikuwa swali gumu la uchumi kueleza hasa kati ya wazee
kama hawa. Uchumi nilikuwa sijui lakini ili kutunza heshima
yangu ya elimu nilijitahidi kuwaeleza lakini hata hivyo
walikuwa bado wakinitazama tu wakitegemea kuelezwa zaidi.
Niliona kwamba walikuwa hawaelewi. Mzee yule aliendelea
kuniuliza, "Lakini wewe huoni dhahiri kwamba wakuu wa
Serikali ndio wanaozitengeneza. Wao wanazo sisi hatuna; na
hawafanyi kazi kutuzidi."

Nilijaribu kueleza. Hata hivyo hawakutosheka na jibu langu.

Mzee mwingine aliuliza, "Swali la pesa tuliweke pembeni.
Mimi nitafurahi sana kama utaweza kunieleza kwa nini
mwezi unapoonekana ni mdogo na unapotua unakuwa
mkubwa na mwekundu."

Hapo nilipashwa kukiri kwamba nilikuwa sijui. Niliwaambia
kwamba nilikuwa sijifunzi somo hilo na kwamba somo hilo
liliitwa Jiografia. Niliposema hivyo tu wazee hawakuwa na
shauku tena ya kuniuliza maswali. Hawakuona tofauti kubwa
kati yangu na wao. Mambo yaliharibika nilipoanza kuwaambia
kwamba huenda hakuna Mungu. Wazee wote walikataa kabisa.
Mzee mmoja aliinuka kwenda nyumbani.

"Mnazungumza na mwehu!" alisema kwa kelele. "A!
Anasema kwamba hakuna Mungu! Yeye nani! Labda yeye
ndiye anataka awe Mungu. Hakuna Mungu! Mtoto wa nani?
Mababu na mababu wamekwenda; wamechukuliwa na nani?
Nafikiri mnafunzwa kusoma kumbe mnafunzwa kuvuta
bangi!" Alipomaliza kusema maneno haya alikwenda
nyumbani akitupa mikono juu kwa kutokubaliana na usemi
wangu: "Hakuna Mungu! Mwehu! Mwehu!"

Nilisikia yule kijana aliyeleta pombe akimnong'oneza
Kamata: "Mgeni wako ameanza kupatwa na pombe. Lakini

59

mwambie azungumze juu ya mambo mengine au aache kabisa
la sivyo ataharibu kikao."

"Tunaweza kuhama," Kamata alimwambia.

"Ndiyo. Mnaweza kwenda nyuma ya nyumba yangu.
Nitawaletea pombe yenu huko."

Kamata aliponiambia kuhama sikupinga, nilikuwa nimesikia
maneno yote. Tulipofika nyuma ya nyumba hiyo, kijana
alituletea mtungi mdogo wa pombe. Kamata alikaribisha
vijana wawili zaidi waje wanywe pamoja nasi, lakini yule
kijana alikataa na kuwafukuza.

"Kama pombe ikiwashinda chimbeni shimo mumwage
humo," alisema. Tulianza kunywa peke yetu. Kwa kuwa kila
mmoja kati yetu aliogopa kulewa sana tulikunywa pole pole.

"Unamwona yule mwanamke aliyevaa kitambaa kichwani,"
Kamata aliniambia. Kabla sijajibu aliinuka na kwenda
kuzungumza naye.

"Kila kitu tayari," Kamata alisema aliporudi, "isipokuwa
angependa kuzungumza nawe kwa muda mfupi."

"Yaani niende pale alipo kama wewe?"

"Hapana atakuja hapa mwenyewe." Baada ya muda mfupi
yule mwanamke kweli alikuja.

"Kaka, habari?" alisema.

"Nzuri," nilimjibu. "Unakaribishwa."

"Asante."

"Kazimoto," Kamata alisema, "ninakwenda kucheza
ngoma kidogo, nikute mambo yenu yamekwisha malizika."

Aliondoka. Nilianza kufikiri namna ya kumwanza huyu
mwanamke ambaye nilikuwa sijapata kukutana naye.

"Karibu pombe."

"Asante," alijibu.

Nilimtilia pombe nyingi. Alikunywa kidogo halafu
akanirudishia. "Nafikiri rafiki yangu amekwisha kueleza kila

60

kitu, sivyo?" Aliinamisha kichwa chini.

"Bado," alisema.

"Unataka nirudie tena maneno yale yale."

"Rudia."

"Ninakuhitaji wewe."

"Unanihitaji mimi?"

"Ndiyo."

"Mm!" aliguna.

"Sasa unasemaje?"

"Unanihitaji mimi vipi?" aliuliza.

"Mwanamke anahitajika kwa kitu gani?"

"Kwa ndoa; wengine kwa siku moja."

"Tuseme kwa siku mbili."

"Haiwezekani."

"Kwa nini?"

"Sina nafasi."

"Sasa tukatishe mambo. Leo usiku au vipi?" Alinyamaza
kwa muda. Alinitazama.

"Wewe nani?"

"Nitakwambia tukionana."

"Unasoma au unafanya kazi?"

"Ninasoma."

"Kumbe mtoto mdogo. Unasoma wapi?"

"Dar es salaam. Bado hujajibu swali langu."

Aliinama. Halafu sauti ndogo ilitoka. "Haya."

"Sikusikia," nilisema kwa sauti.

"Haya," alirudia tena kwa sauti hali ameinama.

"Kunywa pombe." Alikunywa kidogo. Halafu aliinuka
kuondoka.

"Unaondoka!"

"Ninakwenda kucheza. Nitamwambia Kamata zaidi."

"Asante."

61

Nilimwona akizungumza na Kamata. Baada ya mazungumzo
yao alikuja kunywa pombe. Yule mwanamke aliendelea
kucheza. Tulikunywa mpaka tulipoona kwamba tulikuwa
tumekwisha lewa. Kwa vyo vyote tulikuwa hatuwezi
kuumaliza ule mtungi. Tuliwaita wale vijana waliotukaribisha.
Tuliwashukuru na kuwaomba ruhusa ya kuondoka. Walitwa-
mbia twende na pombe yetu. Pombe iliyotushinda tuliiweka
ndani ya kibuyu. Wale vijana walitusindikiza kidogo halafu
walirudi. Tulipokuwa njiani peke yetu Kamata aliniambia,
"Yule mwanamke amesema atakuja nyumbani peke yake.
Yeye akisema huwa hadanganyi. Huo ndio uzuri wake."

"Labda wazazi wake wakali. "

"Wapi! Ni wajinga. Binti yao huwa anawatukana
wanapomzoza."

"Kwa nini?"

"Kwa sababu yeye ndiye huwa anawalisha na kuwavika
kwa pesa apatazo kutoka kwa mabwana mbali mbali."

"Kwa nini hawawezi kumwoza?"

"Hajapata wachumba. Nani ataoa makapi. Huyo sasa
amekuwa mpira, wa kudunda na kuacha hapo, wengine pia
wadunde."

Tulipofika nyumbani Matilda aliamka mara moja kuja
kutupokea. Alituletea chakula. Ajabu kwangu ilikuwa kuona
wingi wa samaki unapita ugali. Wakati wa kula, Kamata
alinihimiza kumeza samaki tu niache kula ugali.

Baada ya kula tulianza kunywa pamoja na Matilda. Pombe
hiyo ndiyo ilinifanya nilewe kuzidi kiasi changu. Tulipokuwa
tunakunywa tulisikia hodi mlangoni.

"Karibu," Kamata alisema.

Yule mwanamke aliingia. Alikuwa amevaa nguo zingine,
na alikuwa akinukia marashi. Alikaa. Tulikunywa pamoja
naye.

62

"Jina lako nani?" nilimwuliza.

"Nyabuso," alijibu. "Na wewe jina lako nani?"

"Mimi Kazimoto bin Machozi ya Simba." Alicheka kidogo.

Tuliendelea kwa muda. Kamata alipotambua kwamba
usingizi ulikuwa umenipata aliniomba nifuatane naye ili
anionyeshe kitanda changu. Tulikwenda kulala.

Kesho yake asubuhi Matilda ndiye aliyeniamsha.

"Kazimoto, saa nne sasa, amka!"

 "Saa nne!" nilishangaa. Nilipotazama saa yangu niliona
kwamba ilikuwa saa nne na nusu. Nilitafuta suruali yangu ili
nivae, lakini sikuiona. "Suruali yangu niliacha wapi?"
niliuliza.

Nilipouliza hivyo tu Matilda alicheka sana. Nilimsikia
Kamata pia akicheka. Nilihisi kwamba jambo la ajabu lazima
liwe limetokea. Kama si la ajabu basi lilikuwa jambo la
kuchekesha.

"Lakini suruali yangu niliacha wapi? Sidhani kwamba
nililewa vile kwamba nilianza kutembea uchi!"

"Kazimoto," Kamata alisema, "nitakueleza baadaye. Kwa
sasa nitakuazima suruali yangu moja."

"Maji ya kuoga nimekuwekea tayari uani," Matilda
aliniambia. Nilikwenda kuoga. Baada ya kuoga nilijiona
afadhali kidogo. Nilivaa suruali ya Kamata. Suruali ya
mwingine ni ya mwingine. Niliona kwamba upepo ulikuwa
ukiingia mwingi sana. Kamata alikuja chumbani kunieleza.

"Kazimoto," alisema hali akicheka, "suruali yako
imechukuliwa na Nyabuso."

"Kwa nini?" niliuliza.

"Anasema wewe si mwanamume."

"Mimi! "

"Ndiyo, wewe. Hukuweza kufanya jambo lo lote."

"Sema kweli!"

63

"Amechukua suruali yako kama adhabu."

"Adhabu!"

"Ndiyo. Ulimpotezea muda wake na ulimsumbua bure."

"... Sumbua bure?"

"Ndiyo. Bila shaka unafahamu ninataka kusema nini."

"Sasa nitafanya nini?"

"Utafanya nini? Sahau tu suruali yako."

"Suruali yangu ninaweza kuisahau. Lakini..."

"Lakini nini?"

"Sifa yangu imeharibika. Yule mwanamke atatangaza."

"Unataka kurudisha jina lako?"

"Kama ikiwezekana." Aliinuka. Alinipiga begani.

"Kazimoto, jina la bure lakini moto hauwaki. Nitamleta
tena leo. Usiniaibishe tena."

"Leo sitakunywa pombe. Unafahamu usiku nilipofika
kitandani nilikufa."

"Haya tutaona leo. Usife tena kwa usingizi."

Baada ya chakula cha mchana Kamata aliondoka nyumbani.
Aliniambia nimngoje nyumbani kwa muda mfupi."

"Unakwenda wapi?" nilimwuliza.

"Hapa karibu. Nitarudi sasa hivi."

Alipoondoka nilikwenda kupiga usingizi kidogo. Kwa kuwa
nilikuwa bado nimechoka usingizi ulinipata mara tu nilipoweka
mbavu zangu juu ya godoro. Matilda aliniamsha saa kumi na
moja. Aliniambia kwamba nilikuwa naitwa katika chumba
cha maongezi. Niliinuka. Nilipofika chumba cha maongezi
nilimwona Kamata na vijana wawili kati ya wale watano
wamekaa kimya wakiningoja. Mtungi mkubwa wa pombe
ulikuwa mbele yao. Nilikaa. Baada ya kusalimiana na wale
vijana Kamata alisema, "Kazimoto, jana tulikuwa
tumekaribishwa na hawa vijana. Mimi nilikuwa bado
sijakufanyia jambo lo lote. Kwa hiyo leo nami nimejaribu

64

kupata kitu kidogo kama hiki ambacho tutakifurahia pamoja
na vijana hawa."

Wote tulishukuru. Tulianza kunywa. Lakini mimi nilikuwa
mjanja. Mara nyingi niliweka mdomo tu. Muda mrefu
haukupita mara Kamata akatambua. Alinishurutisha kumaliza
kiasi alichonitilia. Wakati huu mazungumzo kuhusu vijana wa
siku hizi yalianzishwa na wale vijana. Mwanzoni mazungumzo
yalikuwa kati yao wawili tu.

"Nasikia binti Kasembe ana mimba ya miezi saba," mmoja
kati yao alisema.

"Mama yake anasema mitano."

"Mimi nimesikia saba na ametiwa mimba hiyo na kijana
fulani mchafu mchafu. Sijui wasichana hawana macho?"

"Msichana alikuwa darasa la kumi na mbili na ametiwa
mimba na kilevi kama sisi."

"Wazazi wa msichana huyu wamekataa kumkubalia kijana
huyo kumwoa binti yao."

"Kwa nini?" niliwauliza.

"Wanasema hastahili," mmoja kati yao alisema.

"Mnafikiri nini kisa cha uovu huu wote?" niliwauliza.

"Uovu gani?" Kamata aliniuliza.

"Huu uovu wa watoto kuanza mchezo mbaya wangali
watoto wadogo."

"Kazimoto," Kamata alisema, "mimi nafikiri maovu haya
yote yameletwa na watu wa nje. Kwanza Waarabu. Hao ndio
wameharibu nchi za pwani. Halafu Wazungu hawa, Waingereza.
Mjerumani nasikia hakukaa muda mrefu sana. Lakini
Mwingereza ameleta sinema, magazeti na mambo mengine
mengi ambayo hukimbiliwa na vijana wa siku hizi."

"Hayo yote ni bure," kijana mmoja alisema, "sababu hasa
ni kwamba ulimwengu umegeuka. Zamani mvulana alipata
umri wa miaka kumi na tisa au ishirini kabla ya kujiona mtu

65

mzima. Siku hizi mvulana mwenye umri wa miaka kumi na
minne amekwisha anza kununua wembe dukani. Wasichana
hao ndio wamezidi. Miaka kumi tu, utafikiri maziwa ya
mwanamke mzima. Ulimwengu huu umegeuka."

"Haya yote ni sawa," Matilda alisema, "lakini nionavyo
mimi sababu yenyewe hasa ni kwamba malezi ya watoto
siku hizi yamelegea sana. Wakati mimi nilipokuwa kama wao
ilikuwa mwiko kukutwa na kaka nimesimama na mvulana ye
yote; siku hizi kaka anaweza kumletea ndugu yake barua
kutoka kwa mvulana mwenziwe. Maana yake nini? Wengine
wanaweza kushikana viunoni dansini - kaka na dada!"

Kijana mwingine alitoa wazo lake pia. Yeye alisema
kwamba sababu kubwa ilikuwa kwamba vijana wa siku hizi
wanadharau wazazi wao. Dharau hii imeletwa na elimu.
Wanafikiri kwamba mawazo yote ya wazee ni ya kijadi.

Mazungumzo yaliendelea kwa muda mrefu, kila mtu
ameshikilia wazo lake. Mimi mwenyewe ingawa niliuliza
swali hili, nilikuwa sijapata kulifikiria kwa makini. Nilikaa
kimya.

Tuliendelea kunywa mpaka saa mbili usiku Matilda
alipoivisha chakula. Baada ya kula tuliuzunguka ule mtungi.
Saa tatu Matilda alikwenda kulala. Alituacha sisi tunaendelea.
Saa tatu na nusu Kamata alikwenda kufungua mlango wa
nyuma. Alikawia sana kurudi. Tulifikiri kwamba alikuwa
amekwenda kujisaidia. Aliporudi alininong'oneza sikioni:

"Yumo tayari chumbani mwako."

"Tunafahamu sana," kijana mmoja alisema.

"Kwa nini msimwambie aje kunywa tu pombe pamoja
nasi," kijana mwingine aliongezea.

Sisi hatukutaka kusema zaidi juu ya jambo hilo. Kwa kuwa
wote tulikuwa tumekwisha patwa na pombe tulianza kuimba.
Kamata ndiye alianzisha:

66

Kula tunakula lakini wafuasi wangu,
Tunakwenda tunalia kama bibi arusi,
Kule gizani kwenye mlango usiofunguka,
Kwa yule amezaye bila kutafuna,
Kuzimuni wote tutakwenda.

Wote tuliitikia kwa kurudia maneno hayo hayo. Wimbo
huu hata mimi niliufahamu kichwani kwa sababu ulikuwa
wimbo wa mshairi mashuhuri kisiwani ambaye nyimbo zake
zilikuwa zikiimbwa hata na watoto wadogo.

Pombe ilikwisha saa tano usiku. Tulipeana kwa heri ya
kuonana kesho yake asubuhi.

"Wazee wetu walisema kwamba usiku wageni
hawasindikizwi," Kamata aliwaambia wale vijana. Waliondoka
kwenda kwao wakiyumbayumba.

"Kila mtu amekwisha ingia ndani ya nyumba?" Kamata
aliuliza baada ya muda mfupi

"Ndiyo," nilimjibu.

Alifunga mlango wa nyumba. Nilipoingia chumbani mwangu
taa ilikuwa bado ikiwaka. Yule mwanamke alikuwa amekwisha
lala. Pembeni niliona suruali yangu imewekwa juu ya kiti
kama kikombe cha mashindano. Ilikuwa imefuliwa na
kunyooshwa vizuri sana. Nilikaa kitandani. Yule mwanamke
aliamka. Aliponiona alipiga mwayo mrefu.

"Usingizi ulikuwa umenipata," alisema.

"Umechoka sana leo nini?" nilimwuliza.

"Shauri ya pombe," alijibu. Alianza kunipapasa mgongoni.
"Nilisikia watu wakiimba," alisema.

"Tulikuwa sisi."

"Nilikuwa nawasikia kwa mbali."

"Kwa nini hukuja kunywa pombe?"

"Sikutaka wale vijana wanione, ni waongo sana."

67

"Mbona wamekuona?"

"Basi kesho utasikia maneno. Leo pia umelewa sana?"
aliniuliza.

"Leo ni mzima kabisa."

"Jana ulifanya nini? Ulinisumbua bure. Sikuweza kupata
usingizi."

"Utanisamehe. Tuone leo mambo yatakwendaje."

Baada ya kuvua nguo zangu nilijitupa kitandani tukawa
tunatazamana uso kwa uso. Tulicheka.

"Wewe kijana mpole sana. Kijana mpole namna hii kwa
nini hutafuti mwanamke mzuri ukaoa kuliko kusumbuka na
mikweche kama sisi?"

"Kwani wewe mkweche?" nilimwuliza.

"Unanionaje?"

"Nakuona bado u msichana.

"Nina watoto wanaolingana na wewe."

"Ninafahamu kwamba una watoto wawili wadogo."

"Kamata ndiye amekwambia?"

"Watu wengine. Ninataka nami unizalie watoto wangu."

"Nani atawatunza?"

"Wewe na mimi," nilisema. Tulitazamana machoni.
Tulinyamaza na kuzima taa.

Kesho yake asubuhi yule mwanamke aliniamsha saa kumi
na moja. Tulizungumza kwa muda wa robo saa. Aliniomba
anwani. Niliwasha taa na kumwandikia. Yeye pia alinipa
yake. Saa kumi na moja na nusu aliniomba nimsindikize ili
afike nyumbani kwao kabla ya wazazi wake kuamka. Tukiwa
njiani kwenda kwao aliniomba nisimsahau kwa barua.
Aliniomba nirudi tena kumtembelea Kamata kabla ya kwenda
shule. Mimi nilimwahidi kwamba sitamsahau kamwe.
Nilimwambia kwamba nikipata nafasi nitarudi tena. Nilimsindikiza

68

mpaka nyumbani. Alipoingia ndani ya nyumba nilirudi
peke yangu. Nilifika nyumbani kwa Kamata saa moja na nusu
baada ya kutangatanga. Sababu yenyewe ilikuwa kwamba
nilipotea njia. Nilipofika nyumbani nilikuta maji ya kuoga
yenye moto tayari uani. Baada ya kuoga nilimwambia
Kamata na Matilda kwamba nilitarajia kuondoka siku hiyo
saa kumi. Wote walisikitika sana. Waliniomba nikae nao juma
moja. Niliwaeleza hali ya nyumbani. Mwishowe waliniruhusu
niondoke lakini kwa huzuni.

Mazungumzo yetu siku hiyo yalikuwa juu ya yule
mwanamke - Nyabuso. Waliniambia kwamba huyo Nyabuso
aliweza kunifuata hata Dar es salaam kama akipata nauli.
Walinieleza kwamba alikuwa mwanamke ambaye alikuwa
akichukiwa sana na wanawake kijijini. Yeye aliweza kumfuata
mume nyumbani na kumwita "bwana'ngu" mbele ya mke
wake halali. Aliweza kumzomea mwanamke ye yote ambaye
alikuwa akifahamiana na bwana'ke. Walinieleza kwamba
walimu wa shule moja ya msingi ndio walikuwa mawindo
yake. Walinieleza pia kwamba Mkuu wa Wilaya alikuwa naye
amejijenga hapo. Mazungumzo yaliendelea mpaka saa sita.
Ingawa yalikuwa mazuri, hayakuwa ya kusisimua sana.
Kamata na Matilda walikuwa bado na huzuni kwa sababu ya
kuondoka kwangu siku hiyo.

Baada ya chakula cha mchana, Kamata alichukua mundu
wake. Aliniomba nimngoje kwa muda mfupi. Aliingia ndani
ya shamba lake la migomba. Baada ya muda mfupi alirudi
na mikungu miwili ya ndizi. Alikwenda tena. Alirudi na
mikungu mingine miwili. Saa zangu za kuondoka zilipokaribia
alifunga mikungu hii juu ya baiskeli yangu. Aliifunga kwenye
ncha za mti mikungu miwili upande mmoja, miwili upande
mwingine. Saa kumi kamili niliondoka. Niliwaambia kwamba
muda ulikuwa hauniruhusu kukaa zaidi. Niliwaambia wawape

69

salamu zangu wale vijana na wawaambie kwamba sikuweza
kufika kwao kuwaaga kwa sababu ya haraka. Kamata alifunga
nyumba. Alichukua baiskeli yangu kunisindikiza. Mbwa wake
alikuwa mbele kabisa akiongoza njia. Naye alikuwa akikojoa
katika kila njia panda. Kamata na baiskeli alifuata. Mimi
nilikuwa nyuma yake nikifuatwa nyuma na Matilda na
watoto. Walinisindikiza mpaka barabarani, kilometa moja
hivi kutoka nyumbani.

"Nafikiri sasa utaweza kupanda mpaka nyumbani bila
kushuka," Kamata alisema. "Hakuna mipando mingi.
Tutakuacha ujiharakishe mwenyewe."

"Asante kwa kunisindikiza," niliwambia.

"Utarudi lini kututembelea?" Matilda alisema.

"Sidhani kama nitapata nafasi tena. Nina kazi nyingi sana
nyumbani."

"Fika tena siku ingine," Matilda alisema kwa sauti yenye
masikitiko.

"Haya, nitajaribu, lakini siwezi kusema kwa uhakika."

Kamata alinipa baiskeli yangu. Tuliagana tena. Nilipanda
na kukanyaga baiskeli yangu. Niliondoka. Nilipotazama
nyuma niliwaona bado wamesimama wakinitazama. Baadaye
nilipotazama nyuma tena sikuweza kuwaona. Nilikuwa
nimekwisha kata kona ya barabara. Mimi mwenyewe nilianza
sasa kusikitika. Niliwakumbuka kina Kamata, Matilda, wale
vijana na yule mwanamke. Nilijaribu kukumbuka jina lake.
"Nyabuso," nilisema moyoni.


Nikiwa juu ya baiskeli nilijiona katika hali ya upweke.
Mawazo mengi yalinijia kichwani. Mara niliona baiskeli
yangu inaongeza mwendo: nilikuwa nimefikia mteremko
mkali. Nilijaribu kufunga breki baada ya kuona kundi la
ng'ombe mbele yangu barabarani kabisa. Nilifunga breki

70

kwa nguvu. Nilisikia kitu fulani kama mlio wa chuma.
Badala ya kupunguza mwendo, baiskeli ilianza kwenda
kasi sana. Nilitambua mara moja kwamba sikuwa tena
na breki za nyuma. Niliogopa kutumia za mbele.
Kutahamaki niliona ng'ombe mmoja hatua kumi hivi
mbele yangu. Nilimgonga ubavuni. Nilisikia ng'ombe
analia. Baiskeli ilianguka mbali na mimi nilipita juu ya
mgongo wa ng'ombe na kuanguka upande mwingine.
Kidogo ng'ombe yule anikanyage tumboni aliporuka
kuwakimbilia wenzake. Nilisikia watoto waliokuwa
wakichunga wale ng'ombe wakinicheka na kunizomea:

"Hilo! Lina bahati! Kama lingeanguka juu ya pembe, leo
lingeona cha mtema kuni!"

"Tazama mandizi yake!" walisema.

Niliinuka. Niliona damu kidogo juu ya goti. Nilipotembea
sikusikia maumivu yo yote. Baiskeli yangu haikuharibika.
Usukani tu ndio ulikuwa ukitazama pembeni. Niliunyosha
tena. Ndizi zangu kweli ziliharibika sana, lakini kati yake
mikungu miwili ilikuwa mizuri bado. Ile iliyoharibika
niliifunga vizuri juu ya karia, miwili mingine niliiacha
ikining'inia pembeni. Nilipotazama baiskeli vizuri niliona
kwamba mnyororo ulikuwa umetoka. Niliuweka tena. Nilipanda.
Niliona inakwenda sawasawa. Kwa kuwa haikuwa na breki
nilishuka katika kila mteremko. Kwa sababu hii nilifika
nyumbani usiku kabisa kila mtu amekwisha lala. Mbwa wa
nyumbani kwetu waliponiona walibweka, lakini waliponita-
mbua walikuja kunilaki na kupigapiga mikia yao juu ya miguu
yangu.

71

			4

Ile mibweko ya mbwa mwanzoni ilimwamsha Mama.
Nilipofika chumbani mwangu nilikaa kwanza kwa muda juu
ya kitanda nikifikiria mambo niliyoyaona kwa siku mbili
zilizopita. Lakini mara nilisikia mlango unagongwa.

"Ingia!" nilisema kwa sauti. Mama aliingia mikono nyuma
kama mtu aendaye kilioni.

"Ulikuwa wapi?" aliuliza kwa upole.

Mimi nilinyamaza kwa sababu mara nyingi nilikuwa
nimemwambia asiniulize swali kama hilo.

"Kazimoto, ulikuwa wapi kwa muda wa siku mbili
zilizopita? Uliondoka bila kutuarifu na kurudi kwenyewe
unarudi usiku wa manane. Umezaliwa, Kazimoto, na kuna
watu wanaokujali."

"Unataka nini?" nilimwambia.

"Kazimoto, fahamu kwamba mimi ninakupenda sana,

72

huwezi kuondoka bila kunipasha habari. Ungeuawa je -
tungemshuku nani?"

"Mapenzi ya kitoto namna hiyo mimi siyapendi. Kila siku
niondokapo nyumbani unaniuliza 'Unakwenda wapi?'. Mimi
nimekwisha kuwa mtu mzima sasa, na sitaki wewe uwe
unafahamu njia zangu zote. Hata kama nikiwa nakwenda kwa
wanawake unataka nikueleze?"

"Kazimoto, mtoto wangu, ulimwengu wa sasa hauna rafiki.
Mambo yanayotokea hapa yaonyesha kwamba lazima
ujiangalie. Jana usiku mambo haya yametokea tena. Kwa
hiyo jihadhari."

"Mimi siioni hatari yo yote."

Alinitazama. Mara moja aliona vumbi kidogo juu ya nguo
zangu.

"Umeanguka nini?"

"Ndiyo, lakini sikuumia."

"Huwezi kutambua sasa, maumivu utayasikia kesho.
Lakini bila shaka umeumia. Nikuchemshie maji?"

"Hapana, sikuumia. "

Aliondoka. Nilifunga mlango. Mara baada ya muda mfupi
mlango uligongwa tena. Nilifungua tena.

"Kazimoto, usifunge mlango, ninakutayarishia chakula."

"Usihangaike namna hiyo. Nitakula kesho."

"Hapana, huwezi kulala na njaa."

Alikwenda jikoni. Baada ya muda mfupi chakula kililetwa.
Nilishangaa kumwona mama analia machozi. "Kazimoto,
ninasikitika mboga haitoshi."

"Inatosha sana," nilimwambia.

Baada ya kuweka chakula mbele yangu, nilianza kula.
Yeye alisimama pembeni kidogo. Aliponiona nakula
alitabasamu kidogo.

"Utakapomaliza kula weka vitu pembeni. Nitavichukua

73

kesho asubuhi." Alitoka nje. Ingawa alitoka amefurahi kidogo
nilianza kumhurumia. Nilianza kujilaumu kwamba nilikuwa
mkali kwake bila sababu. Lakini baadaye niliona kwamba
nilifanya vizuri kumwambia, kwani nilikuwa sitaki mapenzi
ya namna hiyo yaendelee.

Kesho yake asubuhi, yaani Ijumaa, Mama ndiye alikuwa wa
kwanza kuja chumbani mwangu kuchukua vyombo. Kwa
kuwa sasa nilikuwa nasikia maumivu kwenye goti na bega
nilimwambia Mama atafute njia ya kuweza kunikanda. Kwa
haraka alitafuta yale majani yatumikayo katika kazi hii.
Baada ya muda mfupi niliitwa jikoni. Majani yalikuwa
yamelazwa juu ya makaa ya moto. Alianza kunikanda mguu,
halafu bega. Wakati akinikanda nilimwuliza habari kuhusu
Rukia. Aliniambia hali yake haikuwa mbaya sana. Alikuwa
amekwisha anza kula kidogo.

"Lakini kwa nini Rukia amesikitishwa sana na mimba?
Wasichana wengine wanapata mimba, lakini wanacheka na
kufurahi kama kawaida."

"Aibu, Kazimoto, aibu ndiyo inamsumbua. Rukia ni
msichana mwenye haya sana. Hataki kuonana na watu. Na
anaona aibu hasa mbele yako."

"Lakini kweli hakuna sababu ingine?"

"Ninakumbuka siku moja nilipokuwa namtuliza
aliniambia, 'Mama hufahamu masikitiko yangu. Nilitegemea
sana kukusaidia lakini sasa siwezi: maisha yangu yameharibika.'"

Baada ya kunikanda nilimwambia achukue zile ndizi
chumbani mwangu, ili akampikie Rukia badala ya ugali.
Mama alifurahi sana.

Saa tatu, Baba na Kabenga waliingia chumbani mwangu.
Hawakukaa. Baba alichungulia tu, aliponiona aliniambia
niende nyumbani kwake. Nilipokwenda niliwakuta Kabenga
na Baba wananingoja. Nilipokaa Baba alianza: "Kazimoto,

74

tuna maneno machache ya kukwambia. Kabenga, ebu
mweleze mtoto huyu."

"Ndiyo, Kazimoto," Kabenga alianza, "unafahamu sasa
umekuwa mtu mzima. Huwezi kurudi kutoka safari ukafika
kukaa ndani ya nyumba yako kimya mpaka baba yako aje
akuone. Mtu akitoka safari anasalimiana na watu wote wa
nyumbani. Hata kama hukutoka safari ni kawaida kuamkia;
lazima ufahamu uzima wa nyumba ingine ingawa mnaishi mji
mmoja. Ukitembea huko nje watu watakuuliza 'nyumbani
hawajambo?' Utajibuje kama hukuwasabahi asubuhi? Kuna
hadithi ya kijana mmoja ambaye alikuwa hamjulii hali mama
yake wakati wa asubuhi. Mama yake alikufa usiku. Yeye bila
kujua alikwenda kilabuni kunywa pombe. Watu walikuja
kumpasha habari huko huko kilabuni. Kazimoto, wewe ni
mtu mzima sasa."

"Jambo la pili," Baba alisema, "ni kwamba uliondoka hapa
bila kutuarifu. Mama yako alikuwa halali. Siku moja alitembea
kijiji kizima akiuliza kama maiti yako ilikuwa imeonekana
mahali fulani. Mambo ya kina mama usiyachukulie kama ya
kipuuzi. Ninasikia ulimjibu kwa ukali sana usiku. Ninataka
kusikia ukinijibu hivyo hata mimi."

Sikutaka ubishi nao. Kwa hiyo nilikiri makosa yangu.
Baada ya kunipa maonyo zaidi walinipa ruhusa kuondoka.

Kwa muda wa siku mbili kichwa changu kilikuwa
kimepumzika huko nyumbani kwa Kamata. Sasa matata
yalianza tena. Nami nilikuwa nimekuja nyumbani likizoni
kupumzisha kichwa changu ambacho kilikuwa kimekwisha
anza kuwanga kwa sababu ya kusoma.

75

			5

Ikiwa siku ya Jumapili, siku ambayo Vumilia alikuwa
ameniambia niende kumchukua, na ndugu yangu akiwa
amekwisha anza kula kidogo ingawa si sana, sikuona
kipingamizi cho chote cha kuweza kunizuia kwenda
matembezi usiku. Ni kweli kwamba Baba alikuwa amenionya,
lakini sikuona kwa nini alipaswa kuhusika sana na mambo
yangu. Kwa hiyo siku nzima nikawa namfikiria Vumilia,
jinsi ya kumleta na kumrudisha bila mama yake kutambua.
Katika kumfikiria, hadithi yake ilinijia tena kichwani.
Vumilia alikuwa mmoja kati ya wale wasichana ambao
hutunza ahadi. "Mungu mmoja, sikuongopei!" alizoea kusema
wakati akitoa ahadi. Lakini Vumilia hakuonekana kuwa
msichana mwenye furaha: alikuwa hajapata kumwona baba
yake. Jambo hili lilimfanya apoteze wachumba kwani wengi
walimwita mtoto wa vichakani.

76

Hili halikuwa kosa lake. Lawama yote ilimwendea Tegemea
- mama yake. Tegemea alipokuwa bado mwanamwari
alifanya kazi ya umalaya. Alikuwa ametembelea miji mingi
ya mwambao, Mombasa hadi Mtwara. Katika kurandaranda
kwake alizaa watoto kadhaa, lakini wote hao walichukuliwa
na baba zao. Tegemea alipoona kwamba vijana walikuwa
hawamchukui, na kwamba kwa siku nzima alilala na shilingi
tatu tu za mlevi fulani, alijiona siku zake zinakwisha, akakata
shauri kuacha umalaya. Mimba aliyokuwa nayo aliitunza
vizuri, akamzaa Vumilia, na mara moja akarudi kisiwani
Ukerewe kabla ya yule bwana aliyehusika kuja kudai mtoto wake.

Mahali alipokuja kuishi hapakuwa mbali sana na kwetu.
Tegemea akajulikana sana kijijini kwa Kiswahili chake cha
upesi na mawimbi; akaitwa Mswahili. Buibui alilokuja nalo
kutoka pwani likawa kitisho kijijinii, akaacha kulivaa. Pole
pole Uislamu akauvua, akaanza kula nyamafu na Ramadhani
akawa anaisikia tu redioni. Mwishowe akaanza kuwa anapika
pombe ya moshi. Pesa alizopata humo ndizo zilizomwezesha
kuishi, kwani aliporudi kutoka pwani mikono yake, kama ya
kiwete, ilikuwa haiwezi kushika jembe kutwa nzima.

Maisha ya Tegemea mimi nilikuwa siyajali. Mimi nilimfa-
hamu sasa Vumilia ambaye nilikuwa na uhusiano naye. Ya
zamani hayanuki. Usiku ulipoingia, baada ya kula, tulikwenda
kulala. Tulipoona kwamba wazee walikuwa wamekwisha
lala, mimi na Kalia tulichukua fimbo zetu, tukashika njia
kuelekea nyumbani kwao Vumilia. Kwa kuwa tulikuwa
wawili na mwezi ulikuwa ukiwaka hatukuogopa cho chote.
Nilishangaa nilipomwona Kalia aliyekuwa nyuma yangu,
anakimbilia mbele.

"Kuna nini?" nilimwuliza.

"Mtu anatufuata!"

77

Kutazama nyuma tuliona mbwa wa nyumbani kwetu.
Tuliwarudisha kwa kuwatupia mawe. Tuliendelea. Yeye
mbele, mimi nyuma.

Mwishowe tuliukaribia mji wa Tegemea. Mji wenyewe
ulikuwa na nyumba moja yenye vyumba vinne. Yeye alilala
chumba chake, Vumilia chumba kingine karibu na mlango wa
nyuma. Chumba kingine kilikuwa cha maongezi, na kilicho-
baki kilikuwa kikitumika kama jiko. Tulipofika nyumbani
kwa Tegemea tulianza kutembea pole pole kwa uangalifu,
lakini hata hivyo, ng'ombe aliyekuwa amefungwa kwenye
mti alitoa pumzi ndefu tulipopita karibu naye. Kalia sasa
alirudi nyuma yangu, tukawa tunanyatia kuelekea upenuni.
Ndani ya chumba cha Vumilia taa ilikuwa imekwisha zimwa.
Chumba cha Tegemea kilikuwa bado na mwanga.

"Tumewahi sana," Kalia alisema pole pole.

"Nyamaza," nilimwambia.

Tulikwenda kwa vidole mpaka mlango wa nyuma,
tukajibanza ukutani.

"Ha! ha! ha! ha!" tulisikia sauti ya jambazi fulani likicheka
chumbani kwa Tegemea. "Kama ningeoa mwanamke kama
wewe, nafikiri ningepata furaha hapa duniani. Mke wangu,
ingawa nimezaa naye watoto wamekua, nilimwoa kwa
kufanyaje tu. Leo nikitoka hapa nafikiri nitampa mgongo
usiku mzima."

"Uwongo wako!" Tegemea alisema.

"Babu atafufuka kama nikisema uwongo. Unafikiri nina
haja naye tena?"

"Uwongo wako! Mbona hata hujafikiria kunioa?"

"Mimi ningeweza kukuoa isipokuwa jambo moja kuhusu
wewe linanichukiza."

"Jambo gani hilo?"

"Usikasirike lakini."

78

"Sema, ni jambo gani?"

"Una tamaa sana ya pesa, yaani huwezi kumpenda mtu
bila pesa. Huku shamba mwanamke hanunuliwi. Lakini mimi
umenimalizia karibu pesa zote anazoniletea mtoto wangu.
Hata hivyo bado hutosheki. Sasa unadai gauni. Unafikiri
mimi pesa nitazitoa wapi?"

"Kama jambo la gauni limekuudhi vaa suruali yako uende
zako! Gauniii! Gauni! Gauni limekuwa gauni. Vaa suruali
uende zako! Leo hufanyi jambo lo lote nami. Yaani
unanifikiria mimi masikini omba-omba. Gauni! Mwenzio
napoteza heshima yangu yote mbele ya binti yangu kwa ajili
yako; unafikiri kuwa hatusikii! Mapenzi gani kuliko hayo?
Gauni! Haya chukua suruali yako!"

"Hasira yote hii ya nini?"

"Nimesema v-a-a s-u-r-u-a-l-i u-ende zako!"

"Unataka kunitoa nje kama kwamba sikuzaa! Haya
chukua!"

"He! he! he! " Tegemea alicheka. "Sasa hizi pesa umezitoa
wapi? Bwana'ngu kila siku matata. Ngoja kidogo niweke mto
wa pili." Tulisikia mlango wa chumba unafunguliwa.
"Ninakwenda kujisaidia, nitarudi sasa hivi. Nikute umelala."

Tuliposikia hivyo tuliondoka karibu na ukuta. Tuliinama
ndani ya majani yaliyokuwa karibu na nyumba. Tegemea
alitoka nje na kanga moja, akakojoa karibu sana nasi.
Hakukawia akarudi ndani.

Tulirudi tena ukutani. Kalia alikuwa akicheka kwa ndani
hali ameziba mdomo.

"Anayezungumza humo ndani umemtambua?" aliniuliza.

"Nafikiri nimemtambua."

"Ni Kabenga."

"Kumbe mzee huyu hatari! Uhusiano ulianza lini?"

"Tangu zamani," Kalia alisema, "isipokuwa mlikuwa bado

79

hamjagongana kama leo. Nasikia uhusiano huu ndio umeleta
ule mpango wa kumwoza Vumilia kwa Manase. Tuza anapinga
sana uchumba huu, na Manase mwenyewe hapendi. Juzi juzi
walimtuma Vumilia kwenda kuzungumza kidogo na Manase.
Lakini nasikia Vumilia alimkuta Manase anaishi na kimada.
"Gonga dirisha umechukue mke wako twende, naona baridi."

Alipomaliza kusema hivi mlango wa nyuma ulifunguliwa
pole pole.

"Mbona mnazungumza kwa sauti ya juu namna hii?"
Vumilia alisema.

"Tayari twende?" nilimwuliza.

"Ngoja nivae,"alijibu. Alirudi ndani. Hakukawia.
"Twendeni; tangulieni mbele kidogo."

Tulitangulia. Tulimwacha nyuma akifunga mlango.
Baada ya muda alikuwa pamoja nasi.

"Wanaume wawili bado mnatembea na fimbo; woga
gani huo!" alisema.

"Hatuogopi kitu cho chote," nilijibu.

"Mtanirudisha saa ngapi?" aliuliza.

"Saa kumi na mbili."

"Saa kumi na mbili kutakuwa karibu mchana. Mimi nataka
kurudi saa kumi. "

Wakati huu nilisimama kujisaidia. Kalia na Vumilia
waliendelea mbele. Hawakufika mbali nao wakasimama
kuningoja. Nilimwona Kalia anamshika Vumilia kiunoni.

"Acha! Humwogopi kaka yako?" Vumilia alisema.

"Wewe shemeji yangu, kwa hiyo usijali sana."

Nilipowakaribia Kalia aliondoa mkono wake. Tuliendelea
kimya mpaka nyumbani. Tulipofika nyumbani, tulipita
mlango wa nyuma. Ndani ya nyumba Kalia alianza kutoa
manung'uniko yake ambayo nilifikiria kuwa ya kitoto.


 miaka mia moja iliyopita, Afrika Mashariki
imekumbwa na mabadiliko mengi ya kiuchumi na kisiasa.
Mifumo ya jamii imebadilika. Katikati ya karne iliyopita
baadhi ya jamii zetu zilikuwa katika hatua mbalimbali za
mfumo wa ujima; baadhi zilikuwa katika hatua mbalimbali
za mfumo wa ukabaila. Bali katika kipindi hiki dharuba ya
ubeberu katika umbo la ukoloni na baadaye ukoloni mam-
boleo imezisukumizia jamii zote hizi katika mfumo wa
ubepari. Ukoloni umerutubisha mbegu za upinzani na utaifa,
na umejikuta ukikabiliwa na madai ya wananchi ya uhuru na
demokrasi na usawa wa kiuchumi. Baada ya uhuru madai
haya yamepenya pia - na ilibidi yapenye - katika utamaduni,
katika fasihi, na hasa katika ushairi. Mikatale ya kisiasa na
kiuchumi ya ukabaila na ukoloni imekataliwa. Mikatale ya
kisanaa (km. katika ushairi) vile vile imekataliwa. Mipaka ya
kisanaa iliyowekwa na jamii hizo kwa matumizi na manufaa
ya mabwana wa jamii hizo imekiukwa.

Mgogoro huu wa ushairi ni sehemu na ni tokeo la
mivutano hiyo ya kijamii. Mazingira mapya ya mwamko wa
kitaifa baada ya uhuru, mwamko wa kujitafuta asili na
kujitafutia mustakbala wenye matumaini mapya kwa umma
umewachochea watu waanze kusaili mapokeo yote, mazuri na
mabaya, na waanze kutafuta miundo mipya ya kijamii na
miundo mipya ya kisanaa yenye kusadifu vizuri zaidi hali na
migogoro ya leo. Bali miundo hii mipya ya kisanaa haitafutwi

2

ile iwe badala ya ile ya zamani; inatafutwa ili iwe ni nyongeza
kwa ile iliyopo, na iwe ni mchango wa kizazi hiki katika utajiri
wa sanaa tulioachiwa na vizazi vilivyotangulia. Na si miundo
yote ya sanaa inayopendekezwa kutumika sasa ni mipya;
baadhi ni ya kale iliyokuwa imesahauliwa na ambayo sasa
inafufuliwa kwa sababu inaweza kubeba maudhui ya leo.
Baadhi ni miundo ya kawaida ya kifasihi simulizi ambayo
inaingizwa katika fasihi andishi ya Kiswahili.

Mgogoro huu, basi, ni wa kihistoria na umekusanya nguvu
zake toka nyakati za nyuma. Tangu mwanzo wa ukoloni
pamekuwa na ukinzano "usiotamkwa" baina ya wale
waliotunga kwa kufuata kanuni za mapokeo na wale
waliotunga mashairi guni. Mvutano huu uliendelea hadi
ukafikia wakati ambapo ilibidi hata kina Amri Abedi
waukubali ushairi huu ni mtindo katika ushairi wa Kiswahili,
hasa baada ya tafsiri ya Shakespeare: Juliasi Kaisari,
iliyofanywa na Rais J.K. Nyerere. Kadhalika mgogoro huu
umekusanya nguvu kutoka katika uwili wa fasihi yetu: fasihi
simulizi na fasihi andishi, na mwamko wa kifasihi wa
kuiangalia fasihi simulizi kwa jicho jipya, kwa madhumuni ya
kuitumia kuirutubisha fasihi andishi (katika ushairi wa fasihi
simulizi ambayo haijaathiriwa hata kidogo na maandishi ni
nadra sana kukuta vina na urari wa mizani). Kwa hiyo, basi,
chimbuko la mgogoro huu limechangamana sana. Maelezo ya
wanajadi hayatuambii lolote juu ya jambo hili.

Licha ya mazingira ya kiuchumi na kisiasa, hata
mazingira ya kiisimu ni mazuri, na yanaurutubisha mgogoro
huu. Hivi leo Kiswahili si lugha ya Pwani tena kama
ilivyokuwa karne mbili zilizopita, ila inazidi kuwa chombo cha
utamaduni wa Afrika Mashariki nzima. Leo hii maana ya
dhana "fasihi ya Kiswahili", "ushairi wa Kiswahili" si ushairi
au fasihi ya watu wa Pwani, bali ni ushairi na fasihi ya watu
wa Afrika Mashariki inayoeleza hali halisi ya hapa kwa lugha
ya Kiswahili. Kwa ufupi, leo Kiswahili katika matumizi yake
mbali mbali (ya kawaida, ya kifasihi, n.k. ) hakikubali
ufafanuzi wowote uliojikita katika misingi finyu ambayo
haizingatii hali mpya iliyopo.

Maendeleo na mabadiliko ya kiuchumi na kisiasa
tuliyoeleza yamekuwa na tokeo moja kubwa na muhimu sana
la kitamaduni: kukua na kupanuka kwa elimu. Baada ya
Uhuru, elimu ya msingi, sekondari, vyuo na chuo kikuu

3

imepanuliwa. Somo la Kiswahili (lugha na fasihi) limewekewa
mkazo mkubwa katika mashule na vyuo. Wanafunzi na
walimu wa Kiswahili wamepata nafasi ya kudadisi kitaaluma
masuala mengi ya kifasihi, likiwemo suala la "ushairi ni nini".
Wamepata pia nafasi ya kusoma fasihi za mataifa mengine, na
hivyo kupanua mawazo yao kuhusu fasihi. Wameona namna
watu wa mataifa mengine wanavyotunga au walivyokuwa
wakitunga ushairi wao. Wameulinganisha ushairi huo na
ushairi wa Kiswahili na wa makabila mbali mbali ya Afrika
Mashariki na wamegundua kuwa, mbali na lugha, yapo
mambo mengi yanayofanana baina ya ushairi wa mataifa
mbali mbali - ule ulioandikwa na ule unaosimuliwa kwa
mdomo tu. Imedhihirika pia kuwa msisitizo juu ya vina na
mizani ulikuwa umeukwamisha ushairi wa Kiswahili katika
umbo lisilobadilika. Hali hii ilipingana kimsingi na kanuni ya
sanaa ya uumbaji. Washairi wengi wa Kiswahili wakawa
hawaumbi; wakawa wanayapanga tu mawazo yao katika
umbo la vina na mizani na mhariri wa Uhuru na Mzalendo
anayachapisha.

Zaidi ya hayo, imedhihirika pia kuwa fikra kuwa vina na
urari wa mizani ni "roho" na "uti wa mgongo" wa ushairi
imepotoka kimsingi; ni nadharia ya ushairi ambayo haiwezi
kuthibitika katika uchambuzi thabiti wa kitaaluma. Kwa hiyo,
basi, upotofu wa fikira yenyewe ni kichocheo kingine cha
mgogoro huu.

Katika makala haya nia yetu ni kuyachunguza madai na
hoja za wanajadi ambazo wamekwisha kuzitoa katika
mjadala huu. Tutachunguza dai lao kuwa ushairi wa mtiririko
ni wa kigeni (Kizungu); tutachunguza fikira zao kuhusu
ushairi guni wa Kiswahili; tutachunguza fafanuzi zao juu ya
hulka ya ushairi; tutayahakiki maelezo yao juu ya maana ya
ushairi; na kisha tutatoa maelezo yetu kuhusu ushairi ni nini.
Kwa hakika mawazo mengi ambayo tutayasema hapa tulik-
wisha kuyasema katika makala ambazo tumeandika juu ya
suala hili, katika makongamano, mihadhara, malumbano ya
kishairi, n.k. Hata hivyo, kwa faida ya wale ambao
hawajasoma makala zetu, na kwa manufaa ya wale wadhanio
kuwa nia yetu ni kuua ushairi wa Kiswahili, na mwisho, kwa
faida ya wale wadaio kwamba eti sisi tunadai kuwa "ushairi
wa Kiswahili wenye kanuni za kawaida haufai tena",
tunaziweka hoja na maelezo yetu hapa ili yaeleweke

4

kinaganaga, kama watakuwa tayari kuyasoma kwa nia ya
kuelewa.

Upekee wa ushairi wa Kiswahili uko katika kanuni za
vina na urari wa mizani?

Vina na urari wa mizani ni mambo ambayo kwa karne
nyingi yalifikiriwa kuwa muhimu sana katika ushairi wa Asia
na Ulaya. Mpaka hii leo, ushairi wa Kiarabu, kama ushairi wa
Kiswahili, bado unayasisitiza mapambo haya. Lyndon Harries
ameeleza hivi:

Kwa mujibu wa arudhi ya Kiarabu, ilishikiliwa
kuwa, bila ya kujali urefu wa shairi, vina vya
mwisho katika kila ubeti lazima vipatane tangu
mwanzo hadi mwisho wa shairi. Kwa hiyo hata
katika tungo zenye vina vya kati, mtunzi akisha
amua tu kutumia kina fulani katika kipande eha
kwanza, ilibidi akitumie kina hicho hicho hadi
mwisho. Watunzi wengi walipendelea zaidi kutunga
mashairi ambayo vina vyake vya kati ni tofauti na
vile vya mwisho... Utaratibu wa namna hii bado
unafuatwa katika mashairi mengi ya Kiswahili.

Maneno haya karibu yanakubaliana na maneno ya Mnyam-
pala, ambaye amesema:

Shairi liwe na vina vinavyopatana, hususa mwishoni
mwa kila ubeti, kwa shairi lote zima, ingawa vina
vya katikati vikosekane kwa utenzi wote.

Kauli ya Amri Abedi pia inakubaliana na maneno hayo:
Kwa desturi vina vya silabi ya 16 (vya mwisho) huwa
vya namna moja katika beti zote za shairi zima.
Sheikh Amri Abedi mwenyewe, kwa kusoma mashairi ya
Kiingereza, Kihindi, na Kiarabu, alikiri kuwa ushairi wa
Kiswahili hauna upekee wowote na wala siyo tofauti sana na
ushairi wa mataifa hayo:

Mpaka makamo haya nimesoma mashairi ya lugha
ya Kiingereza, ya Kiurdu, ya Kiarabu, na kadhalika
ya Kiajemi aliyonifundisha mmoja katika masheikh
zangu, Maulana Jalal-ud-Din Qamar H.A. Kwa njia
hii nimeweza kujua angalao chembe namna watu wa
mataifa mengine wanavyokusanya fikira na
Kuzipanga, namna ambayo si mbali na ile
iliyotumiwa na watungaji mashuhuri wa Kiswahili

5

wa zamani na sasa.

Katika utangulizi wake kwa diwani ya Mnyampala, Waadhi
wa Ushairi,Amri Abedi alitoa kauli ambayo inabidi ijadiliwe
kwa kuwa imezua upotofu usio wa lazima. Alisema:
Wasemao kuwa mashairi ya Kiswahili asili yake ni
Kiarabu wanazua. Lau wangekuwa wanajua
Kiarabu wasingesema hivyo. Taratibu za mashairi
ya Kiarabu na ya Kiswahili ni tofauti kabisa. Ukweli
ni kwamba Waislamu waliandika habari na
masimulizi ya dini na nyimbo au ushairi wa Kiarabu
kwa herufi za Kiarabu. Lakini kanuni za mashairi ya
Kiarabu ni tofauti kabisa na za mashairi ya
Kiswahili.

Kauli hii ya Sheikh Amri Abedi ni potofu kabisa. Ushairi wa
Kiswahili na Ushairi wa Kiarabu si tofauti kabisa. Sheikh
Saadani Kandoro, kwa kutaka kuonyesha ushairi wa
Kiswahili ulivyo tofauti kabisa na ushairi wa Kiarabu,
anaziorodhesha tofauti hizo:

1. Ubeti wa shairi la Kiswahili huwa na mistari 3,
4, 5, au zaidi. Na hivyo ndivyo yalivyo mashairi
mengi ya Kiswahili katika vitabu na magazeti.
Lakini ubeti wa shairi la Kiarabu huwa na
mstari mmoja tu.

2. Mstari huo wa shairi la Kiarabu hugawanyika
sehemu mbili na kila sehemu inaitwa misraa.

3. Mashairi ya Kiarabu hayana shuruti za vina.
Shairi lenye kuendeleza vina vya kati mpaka vya
mwisho huonekana si shairi la Kiarabu.

4. Mashairi ya Kiswahili si lazima vina vya mwisho
vifanane tangu mwanzo hadi mwisho, ingawa
huwa vizuri zaidi hali hiyo ikiwepo katika shairi
la Kiswahili. Kitu cha lazima ni kufanana kwa
vina vya kila ubeti."
Hebu tuzidadisi kauli hizi za Kandoro.

Anasema ubeti wa shairi la Kiswahili huwa na mistari 3,
4, 5 au zaidi. Kauli hii inabidi kurekebishwa na kuwa: ubeti
wa shairi la Kiswahili huwa na mistari 2, 3, 4, 5 au zaidi.

Anasema kuwa ubeti wa shairi la Kiarabau huwa na
mstari mmoja tu. Jambo hili lazima litazamwe kwa uangalifu
zaidi, na haifai kulipitia juu jau tu. "Ubeti" (wingi: beti) ni
neno lenye asili ya Kiarabu. Kufuatana na utaratibu wa kijadi

6

wa shairi (kasida) la Kiarabu, kila ubeti unazo misraa mbili.
Lakini neno hili, katika ushairi wa Kiswahili, inavyoelekea
limepanuka: shairi la Kiswahili siku hizi laweza kuwa na
ubeti wenye vipande au "misraa" nyingi. Hili si jambo la
kustaajabia. Isitoshe kabla ya kuingizwa kwa hati ya Kirumi,
mashairi na tenzi nyingi za Kiswahili zilizoandikwa kwa hati
ya Kiarabu zilikuwa na mstari mmoja tu kila ubeti. Mstari
huo (au ubeti huo) ulitakiwa ujitosheleze kwa maana.

Sifa hii ya kujitosheleza imo pia katika ushairi wa
Kiswahili, ingawa Saadani Kandoro hakuitaja. Washairi wa
Kiswahili wanakubaliana kuwa ubeti wa shairi la "jadi" ni
lazima ujitosheleze kwa maana, yaani maana yake isiwe nusu
nusu. Kadhalika, mstari wa shairi la Kiswahili unapaswa
kujitosheleza, yaani utoe dhana kamili, usiwe nusu sentensi.
Kanuni hii ya kujitosheleza imo pia katika ushairi wa Kiarabu.
Mtaalamu mmoja wa ushairi wa Kiarabu, A. J. Arberry,
anaeleza hivi "Katika ushairi wa Kiarabu, ilifikirika kuwa ni
dosari kuruhusu muundo wa sentensi kuvuka ubeti (au
mshororo mmoja wenye misraa mbili) na kuendelezwa katika
mshororo unaofuata, kila mshororo ulifikiriwa kuwa ni kauli
inayojitosheleza."

Anasema kuwa "shairi la Kiarabu halina shuruti za vina".
Kauli hii lazima irekebishwe na kuwa: Shairi la Kiarabu
halina shuruti za vina vya kati. Na kwa nini "shairi lenye
kuendeleza vina vya kati mpaka vya mwisho" lionekane siyo
la Kiarabu? Kwa kweli hata shairi la Kiswahili halina shuruti
ya vina vya kati na yapo mashairi mengi ambayo hayana vina
vya kati na bado yanakubalika kuwa ni ushairi wa Kiswahili.
Utenzi wa Hamziya, mathalan, una kina cha bahari tu, hauna
vina vya kati.

Mashairi mengi ya zamani (kabla ya mwaka 1700) hayana
vina vya kati (vya misraa), yamezingatia kabisa kawaida za
ushairi wa Kiarabu kama anavyozieleza Kandoro (ingawa
anasahau au hajui kuwa baadhi ya mashairi ya Kiarabu yana
vina vya kati). Aidha, kauli hii ya Kandoro haikubaliani sana
na kauli ya Amri Abedi isemayo:

Kwa desturi vina vya silabi ya 16 huwa vya namna
moja katika beti zote za shairi zima, na vina vya
silabi ya 8, kwa desturi inayotumika sana, huwa
tofauti ubeti hata ubeti.

Sheikh Amri Abedi alitaka kutueleza kuwa ushairi wa

7

Kiswahili ni tofauti kabisa na wa Kiarabu, jambo ambalo
hakuthibitisha. Kandoro alitaka kututhibitishia kuwa ushairi
wa Kiarabu ni tofauti na wa Kiswahili. Je, ni kweli kuwa
ushairi wa Kiswahili ni tofauti kabisa na ushairi wa Kiarabu?

Kwa hakika ingewafalia sana wanajadi iwapo wangejion-
doa katika "uzalendo" finyu, katika gamba la "Uswahili", na
kuuona ukweli kuwa arudhi ya Kiswahili imeathiriwa sana na
arudhi ya Kiarabu, ingawa ushairi wa Kiswahili asili yake siyo
Uarabuni. Kanuni iliyotajwa hapo juu, ya "vina vya silabi ya
mwisho kuwa vya namna moja katika beti zote za shairi zima,
na vina vya kati kuwa tofauti tofauti" iko katika ushairi wa
Kiarabu na wa Kiswahili. Vile vile urari wa mizani katika beti
zote za shairi ni kanuni katika ushairi wa Kiarabu na wa
Kiswahili. Mifano aliyoitoa Kandoro katika kitabu chake
haitupatii picha sahihi ya muundo wa shairi la Kiarabu kwa
kuwa amedondoa mshororo mmoja mmoja tu. Hebu tutoe
mfano wa shairi zima hapa chini:
(Katika hati ya Kiarabu)

(Katika hati ya Kirumi)

Abu Nuwas

Hamil - ul - hawa ta'ibu yastakhifuhu - utarabu
Inn baka'a yahikku lahu laysa maa bihi la'abu

8

Kulama inaqadha sababu minki 'ada li sababu
Tadhakina lahiyatan wal - muhibu yantahibu
Ta'a jabiyna min sagamy sihaty hiya al - ajabu 14

Maana yake:

Mtu mwenyewe hawa yu mchovu, jaziba humpepesua.
Akilia yuna haki, jukumule si mzaha.
Sababu moja ya dhiki yangu ikiisha nyingine hurejea
kwangu toka kwako.
Wewe wacheka kwa furaha wakati muhibu wako aom-
boleza.
Waajabia dhiki yangu -  kwamba ningali na siha ndiyo
ajabu kabisa.

Hapa tunaona kuwa kina cha kati katika mstari wa kwanza
kinapatana na kina cha mwisho, lakini vina vya mwisho ni
vile vile toka mstari wa kwanza hadi wa mwisho. Na hii ndiyo
desturi ambayo imekuwa ikifuatwa katika ushairi wa
Kiarabu, na hata leo hii inafuatwa.

Suala la athari za ushairi wa Kiarabu kwenye ushairi wa
Kiswahili si jambo ambalo lahitaji mjadala mrefu kwa vile ni
dhahiri sana. Waandishi wa kwanza wa mashairi ya Kiswahili
wali kuwa masheikh na walimu wa dini, waliotaalamika
katika lugha ya Kiarabu na Kurani (wengi wao wakiwa
Waarabu au wale waliochanganya nasaba). Na kwa kuwa kila
kitu eha asili ya Kiarabu kilikuwa ndicho kipimo eha
ustaarabu, hata walipoanza kuandika mashairi au kutafsiri
kasida au tenzi za Kiarabu kwa Kiswahili walilichukua kuwa
ni jambo linalokubalika kuwa shairi lazima liwe na urari wa
vina na mizani. Dhana nyingi za ushairi wa Kiarabu zikaanza
kutumika katika ushairi - andishi wa Kiswahili. Msamiati
wenyewe unaotumika, shairi, ubeti, mizani, hamziya, tasmit,
takhimis, tathlitha, tarbia, n.k., ni wa Kiarabu. Ni kweli
ingawa mitindo mingi ilianzishwa, lakini mitindo hiyo yote
ilikuwa kwenye urari wa mizani na vina. Hali inayosemwa
hapa inafanana na ile iliyousibu ushairi wa Ulaya baada ya
enzi za ustawi wa himaya ya Wayunani, ambapo washairi
wengi walifuata kanuni zilizokuwa na asili ya kanuni za
ushairi wa Kiyunani.

Kumbe utungaji wa mashairi katika vina na urari wa
mizani si aambo liwezalo kuupambanua ushairi wa Kiswahili:

9

kwa asili si jambo la Kiswahili, bali ni athari ya kigeni
(Kiarabu). Kuyaita mambo haya "roho" ya ushairi wa
Kiswahili ni sawa na kusema kuwa hapakuwa na ushairi wa
Kiswahili kabla ya kufika kwa Waarabu. Maneno ya wanajadi
yangeweza kusemwa pia na Mwarabu au Mwajemi kuhusu
ushairi wa kwao. Kwa kweli yalikwisha kusemwa na
mtaalamu mmoja wa ushairi wa Kiarabu, R.A. Nicholson, am-
baye anatuambia hivi:

Ushairi usio na vina ni jambo geni kwa Waarabu,
ambao kwao vina si pambo la kuvutia au "kifungo
chenye udhia", bali ndiyo roho ya ushairi.

Kwa upande mwingine, ushairi wa asili wa Kiswahili (na wa
Kibantu kwa jumla) hausisitizi vina wala urari wa mizani.
Kwa hiyo basi malenga wa Kiswahili wanaotetea vina na
mizani hawatetei mambo ya msingi katika ushairi wa
Kiswahili, bali wanatetea athari za Kiarabu, ijapokuwa
kinafsi sio kusudi lao. Kwa kweli wengi wanaamini kuwa
wanachokitetea ndio "Uafrika". Vina na mizani haviupam-
banui ushairi wa Kiswahili, bali vinaunasibisha na ushairi wa
kigeni, hasa wa Kiarabu na Kiajemi.

Lipo dai moja la kuchekesha kuwa ushairi wa mtiririko ni
barua, insha au mkusanyo wa maneno tu bila utaratibu
wowote. Dai hili ni la kuchekesha kwa sababu hakuna andiko
lolote lenye mantiki na maana ambalo halina utaratibu
wowote. Pili barua si lazima iwe nathari. Katika ushairi wa
Kiswahili ipo desturi ya kuandikiana barua kishairi. Barua
hizo huitwa risala, na kwa kawaida huanza kama hivi: "Risala
ninakutuma..." au "Tumwa ukifika (mahala)..." n.k. Kwa hiyo
inawezekana shairi fulani la mtiririko likawa ni barua na ni
ushairi wakati huo huo.

Kuhusu ushairi wa mtiririko kuwa "insha" jibu litatolewa
baadaye tutakapojadili maana ya ushairi na mbinu za
ushairi. Jambo la kudokeza hapa ni kwamba mashairi ya
mtiririko si "huru" hata kidogo, yanazo mbinu, kunga na
kanuni yake, na si rahisi kuyatunga. Ila katika kanuni zake
hizo kuna uhuru mkubwa wa kubuni na kutunga. Kanuni
yake kuu, ambayo kila mtungaji wa shairi yabidi aitimize,
kanuni ambayo ndiyo roho ya mashairi haya, na roho ya fasihi
kwa jumla, ni kwamba muundo wa shairi lazima uamuliwe na
kufungamana na mawazo, mtiririko wa hisia, na makusudio ya
mtunzi. Msimamo wetu hapa ni kwamba hakuna muundo au

10

miundo maalum ambayo lazima ivaliwe na kila shairi, au
sheria maalum zisizotanguka ambazo lazima zikaririwe na
kila mshairi kama "sala ya bwana".

Sasa na tuyapitie kwa ufupi madai mawili yanayotumiwa
na wanajadi kuuhujumu ushairi wa mtiririko. Dai la "ugeni"
na dai la "uguni".

"Ugeni" katika Ushairi wa Kiswahili

Wanajadi kama vile hayati Chiraghdin, Mayoka, Kandoro,
Al - Amin Mazrui na Ibrahim Sharif wanakubaliana kuwa
vina na urari wa mizani ndivyo vitambulisho vya ushairi wa
Kiswahili. Ndiyo maana wakauita ushairi wa mtiririko wa
kina Kezilahabi, E. Hussein, Jared Angira, Crispin Hauli. F.
Senkoro, na wengine kuwa ni mtindo wa Kizungu kwa lugha
ya Kiswahili. Wanajadi wengine, kama Tigiti Sengo,
wanaukubali kuwa ni ushairi, lakini si ushairi wa Kiswahili.
Msimamo huu wa wanajadi unatokana na fikira potofu juu ya
"ugeni", au "upya"; pili unatokana na kutoijua hulka na
historia ya ushairi wa Kiswahili.

Kwani ugeni wanaouhofu ni nini? Ugeni si jambo la ajabu
sana. Ugeni wa kitu katika uwanja fulani wa maisha unaweza
kujitokeza kwa namna tatu: ama kitu chenyewe ni kipya
kabisa, na kimetoka nje; au kitu cha asili kilichokuwepo
kimeathiriwa na kitu kigeni ama kitu hicho ni kipya na
kimegunduliwa mahali hapo hapo. Ndipo watu baadaye
huweza kusema kuwa "kitu hiki kina asili ya huko" au "kile
kimeathiriwa na hicho", au "hiki kilibuniwa na fulani". Kwa
mujibu wa maelezo haya, Uislamu una asili ya Kiarabu,
Ukristu una asili ya Kiyahudi, mifumo ya elimu na serikali
tuliyo nayo ina asili ya Kizungu, riwaya na tamthiliya ya
Kiswahili vina asili ya Kizungu, taarabu ina asili ya Kiarabu,
.nk. Sasa je, ushairi wa mtiririko una asili ya Kizungu?

Kwa hakika, dai hili la wanajadi lingekuwa sahihi iwapo
mtindo wa namna hii usingekuwapo katika fasihi simulizi ya
Kibantu, ambayo ni pamoja na ile ya Kiswahili; na iwapo
ingekuwa ni kanuni mojawapo ya sanaa ya ushairi kutovyaza
mitindo mingine ghairi ya ile iliyopo. Mtindo usiofuata vina na
urari wa mizani ni wa kijadi katika fasihi ya Kiswahili na
Kibantu. Na ujadi wa mtindo huu ni ujadi wa utangu; mtindo
wa vina na urari wa mizani umekuja baadaye kabisa.

Kwa mtu yeyote ambaye amekwisha kushughulika na

11

fasihi simulizi lau kidogo jambo hili si gumu kueleweka. Ipo
mifano mingi ya ushairi wa namna hii. Hapa chini tutatoa
mifano michache kwa manufaa ya wale ambao hawajui
tunaongelea nini.

Mfano wetu wa kwanza ni wimbo (ushairi) wa kubem-
bele za mtoto:

silie mama silie
ukalia waniliza
wanikumbusha makiwa
makiwa ya baba na mama
baba na mama watende
wanioza dume kongwe
halisafiri halendi
kazi kumega matonge.

Huu ni wimbo ambao umekuwa ukiimbwa na kina mama wa
Kiswahili kubembelezea wana wao, ingawa unagusa pia hali
halisi ya kukandamizwa kwa wanawake: kulazimishwa na
wazazi kuolewa na mwanamume mzee. Athari ya mguso wa
wimbo huu hasa unatokana na lugha ya mkato, na takriri,
yaani marudiorudio ya maneno au silabi fulani fulani
yanayovuta hisi za msikilizaji, mwimbaji, au msomaji (silie...
silie... wani... wani... makiwa...makiwa... baba na mama... baba
na mama... wa... wa... hali... hale... ). Katika wimbo huu
tunaona kuwa kipande cha kwanza, cha pili, cha tatu, cha
tano, cha sita, cha saba, cha nane vina urari wa mizani nane;
kipande cha nne kina mizani tisa. Vina katika maana ya
wanajadi havipo ila katika misitari minne ya mwisho tunaona
utaratibu namna hii:

baba na mama watende
wanioza dume kongwe
halisafiri halendi
kazi kumega matonge

Katika mstari wa kwanza fungu-konsonanti -nd- linalingana
na fungu-konsonanti la mwisho katika mstari wa tatu; na
silabi ya mwisho mstari wa pili -ngwe- inatofautiana kidogo na
-nge- ya mstari wa nne. Lakini, ukweli ni kuwa urari wa
mizani unatokana na mahadhi ya wimbo huo, na haupo kwa
sababu ni "roho" ya ushairi!

Sasa tutazame mfano wa ushairi wa majigambo kutoka
kwenye fasihi simulizi ya Kihaya. Jigambo hili ni la kiwindaji;
mwindaji alilitamba mbele ya mtemi baada ya kutoka kwenye

12

uwindaji wa mafanikio:
( Akaruru)
Natonya nko'rulabyo, ninye Nilyegira eya Ngaiza
Ngaiza eya Ruyango
Ruyango eya Karashani
Karashani eya Keitirimbila
Keitirimbila eya Kagomborora
Kambaile ndy'omwange mpulila engoma zajuga zona
Ngambila mukazi wange Kabigumila
Nty'ompe eichumu Iyange Kanywa-bwamba
amoi no omuhoro gwange. Rutema bitega
nturuke ntabale
Omukazi ai mushaija wange
kankuchumbile akatoke
Nti mukazi wange tokichumba
byakuhya mara kandi tokokya
byakujumbula, nti shana okwate
akashweko kake ondabye omumaino
nturuke ntabale!
(Akaruru)
Nilwo nayebembeize embwa yange
Owo Otakiau
Ekajumala kuluga Omwihangiro
Lyamkumbya na Kairu, ekashoora
Omurushanga Iwa Karebe
nkahulila yambilikira, nti tora!
Waitu elyo nachumisile nilyo
Rugaba kandekelele ao,
ebigambo bingi bikatanga enkoko
okwekukusa
Waitu batole ebikwato byange ebi.
Tafsiri:
(Vigelegele)
Naingia kama radi, ni mimi Niyegira mtoto wa
Ngaiza
Ngaiza mtoto wa Ruyango
Ruyango mtoto wa Karashani
Karashani wa Keitirimbila
Keitirimbila wa Kagombolola
Nilipokuwa kwangu nilisikia ngoma (za wito)
zinalia

13

Nikamwambia mke wangu Kabigumila
Nipe mkuki wangu "Mnywa-Damu"
pamoja na mundu wangu "Mkata-Miguu"
nitoke kuitika wito.
Mke wangu akanisihi:
Mume wangu hebu nikupikie ndizi kwanza
Mimi nikamwambia:
Mke wangu huwezi kupika zikaiva
Wala huwezi kuchoma upesi upesi
labda chukua jani la mgomba (lililotumika
kufunikia ndizi)
Unipitishie katika meno
Niitikie wito.
(Vigelegele)
Ndipo nilipotangulia na mbwa wangu Usiyem-
dhania
Aliteremka kutoka mbuga ya Lyamkumbya
na Kairu hadi kwenye msitu wa Karebe
Nikasikia ananiita (kwa kubweka )
Nikamjibu Kamata !
Mheshimiwa, mkuki mmoja niliotupa mnyama
akawa maiti...
Ee, Mpaji (Rugaba) nikomee hapo
Maneno mengi yalimzuia kuku kutawaza
(baada ya kwenda haja)
Mpaji, pokea mawindo haya.

Hatuna haja ya kujadili mbinu zilizotumika katika kijigambo
hiki. Jambo muhimu hapa ni kuona kuwa hakuna urari wa
mizani na vina katika ushairi huu. Na ushairi wote katika
fasihi simulizi za Kibantu uko hivi - labda tu uwe umeingiliwa
na maandishi pamoja na kanuni za vina na urari wa mizani.

Kwa nini jigambo hili tunaliita "ushairi"? Jibu la swali
hili tutalipata hapo baadaye tutakapojadili maana na kunga
za ushairi. Kutokana na mifano hii, tunaweza kuhitimisha
kuwa dai la wanajadi kuwa ushairi wa mtiririko una asili ya
Kizungu halina msingi wowote. Wahenga wetu wamekuwa
wakiimba au kusema ushairi wa namna hii kwa miaka nenda
miaka rudi. Hapa lazima tuongeze jambo moja: tusidhani
kuwa ipo tofauti ya ajabu baina ya "free verse" ya Kiingereza
na ushairi huu. Pengine tofauti kubwa tunayoweza kuitaja ni
kuwa "free verse" ni ushairi wa vitabuni, na ushairi huu ni

14

ushairi uishio pamoja na shughuli za kimaisha, kama kubem-
beleza mtoto, kujigamba, n.k.

Je, mtiririko ni mashairi gani?

Suala la ushairi guni lilijitokeza katika mgogoro huu hasa
kwa sababu ilitokea rai kuwa mashairi "mapya" ya mtiririko
ni mashairi guni. Ushairi guni, Chiraghdin anasema, ni "tungo
ambayo haikutosheleza sharuti za lugha, mizani, na vina".
Kwa Sheikh Amri Abedi, ushairi guni ni ushairi "usio na
vina". Kandoro na Mayoka wanakubaliana kuwa ushairi guni
ni "ushairi wenye dosari". Kwa jumla, wanajadi
wanakubaliana kuwa ushairi guni haufuati kanuni za vina au
za urari wa mizani, au yote mawili. Kwa nini basi mashairi sa
mtiririko yasiitwe mashairi guni, hasa kwa kuwa hayafuati
kanuni za "kijadi"?

Swali hili limepatiwa majibu tofauti toka kwa wataalamu
na washairi mbalimbali. Farouk Topan anasema mashairi
haya hayawezi kuitwa guni kwa kuwa "uguni" ni tokeo la
kushindwa kufuata kanuni za vina, urari wa mizani na
kutosheleza na watunzi wa mashairi haya hawajashindwa
lolote. Chiraghdin naye, kwa kuwa anaamini kuwa mtindo
huu ni wa Kizungu (blank verse au free verse), hawezi kuyaita
mashairi guni. Hatuelezwi tofauti iliyopo baina ya mashairi
guni na blank verse au free verse, bali tunaelezwa tu kuwa
"tungo hizi zikikubaliwa .. basi ushairi wa Kiswahili utakuwa
umeanguka kitakotako" (Iwapo ushairi guni umekuwepo
tangu zamani na haujauangusha ushairi wa Kiswahili, kuna
haki gani ya kudai kuwa ushauri wa mtiririko utauangusha
ushairi wa Kiswahili?) Hata hivyo, msimamo wa Chiraghdin
unaelekea kuwa na mkinzano ndani yake. Katika utangulizi
wake kwa Malenga wa Mrima, anasema: "Shairi la Kiswahili
hukosa umbo lake likikosa vina na mizani; na hapo huwa
haliitwi tena shairi." Kisha anaongeza: "Umbo lake likilemaa
huwa bado ni shairi, lakini huwa ni guni." Iwapo umbo la
shairi ni vina na mizani, tungo itaendeleaje kuitwa shairi
Iwapo haina vina na mizani? Upotofu wake unazidi
anaposema kuwa umbo la ushairi la vina na mizani limekuwepo
tangu ukale wa ushairi, na kwamba kilichobadilika ni kuv-
yazwa kwa bahari mbalimbali za ushairi: "Kumetokea na
kukua kwa bahari mbalimbali za ushairi katika hilo umbo
lake." Tumeshaonyesha kuwa vina na urari wa mizani ni

15

athari za kigeni; hatuna haja ya kujirudia hapa.

Mayoka na Kandoro wanakubali kuwa shairi guni ni
shairi lenye dosari, lakini wanakanusha kuwepo kwa ushairi
huu katika ushairi wa Kiswahili. Mayoka anasema: "Kwa
kweli ushairi guni hauko katika ushairi wa Kiswahili." Kan-
doro naye anasema: "Kwa ufupi wa maneno, hakuna aina ya
shairi 'guni'. Mtunzi mwenye kujua hawezi kujigamba kwa
kutunga tungo zenye kasoro na kuziita mashairi. Hathubutu
hata kidogo kwani jambo hilo litamvunjia hishima yake."
Ama kweli hii ni "ufupi wa maneno.. kwani "urefu" wake
unaonyesha kuwa ushairi guni upo, hata kama wautungao
hujivunjia "hishima".

Kitu ambacho Amri Abedi mwenyewe (ambaye wanadhani
wanatetea sheria alizoandika) alikikiri na kukiheshimu,
Mayoka na Kandoro wanakikanusha. Yaelekea walifanya
hivyo kwa kudhani kuwa wakikubali kuwepo ushairi guni
katika ushairi wa Kiswahili basi tungedakia na kuuita
mtiririko ushairi guni.

Kwa kuwa yaelekea wapo watu wengine wenye fikira
kama za kina Mayoka, basi inafaa tuchunguze, lau kidogo,
iwapo kweli guni ni umbo mojawapo katika ushairi wa
Kiswahili, au la.

Historia ya ushairi-andishi wa Kiswahili inatuonyesha
kuwa ushairi guni umekuwepo tangu zamani. Pili, historia hii
inatuonyesha kuwa kwa kadiri ushairi guni ulivyozidi kuishi
pamoja na ushairi uliofuata kikamilifu kanuni za vina na
urari wa mizani, ndivyo ulivyozidi kukubalika kuwa ni fani
mojawapo ya ushairi wa Kiswahili, hasa baada ya malenga
mashuhuri kuukubali, na hata baadhi yao kuutunga.

Tuchunguzapo kurasa za matoleo mbalimbali ya gazeti la
Mamboleo tunakuta mashairi ambayo hayakufuata kanuni
hizo. Katika toleo la 10, Oktoba 1923, tunakuta shairi
"Shangilieni Mgeni Mambo Leo Kaingia", lililotungwa na
Said Bin Kikulacho, ambalo, kwa kadiri ya kanuni za
wanajadi lina dosari. Hapa tunadondoa beti chache:

Mamboleo ana sifa zilizotupendeza
Na mtakapo sifa zake kidogo nitawaambia
Habari nyingi za pwani na bara hutuambia
Shangilieni mgeni Mamboleo kaingia...

16

Na zikiwa habari ambazo hazipendezi
Wenyi kuleta habari za fitina na kutukanana
Fahamu atakujibu pasipo jina kutaja
Shangilieni mgeni Mamboleo kaingia...

Atupa habari za wezi waliopo tuwajue
Twajua kuvunja nyamba kuna na wa Relwe
Kuna Kampuni Sinzia mikononi hukuibia
Shangilieni mgeni Mamboleo kaingia..."

Kwa kweli, baadhi wa washairi wa siku hizo walikuwa
hawajali vina vya kati kamwe (k.m. Mdanzi Hanassa), na
wengine hawakujali sana urari wa mizani (Limo, Mdanzi)
Lakini shairi ambalo halikutumia vina kabisa ni lile lililotoka
kwenye Mambo Leo ya Desemba 1928, juu ya mnazi,
lililotungwa na A. Pacha. Kwa vile sanaa ya shairi hili ni ya
hali ya juu inafaa tulidondoe lote.

Mnazi (Jibu la Shairi la Mti Gani wa Faida Ushindao Miti
Pia?
la Bwana Khamis)

1. Hili ni jawabu, la maswali yako
Nililojaribu: na kwa Mamboleo
Nasihi niseme: uniwie radhi,
Ewe! Bwana Khamis: idadi ya miti
Uliyohasibu: imepungukiwa
Kwani mimi MNAZI umenirukia.

2. Sitafidhulika: wala kudharau,
Utani wa miti: iliyo wenzangu,
Kila mmojawapo humfaa bin Adam,
Kwa leo, kwa kesho: humleta usalam.
Hapana kibovu: kwa mwenyi busara,
Na Mwenyezi Mungu yote amelinga.

3. Niruhusu bwana: nitoe sauti,
Nionye mafaa: yashindayo miti,
Hapa Tanganyika: Unguja na Pemba.
Ni tangu asili: watu hunipenda.
Linafahamisha: MNAZI jina langu
Upunga, kitale, kidaka na dafu.

17

4. Koroma na nazi: mbata na majoya
Ni majina nane: tunda langu moja:
Kila mtu huchuma: kwa maonji yake.
Chakula, cha kunywa: apendavyo yeye.
Faida ingine: sijasema bado,
Nisaburi tena usivunje moyo.

5. Ijapo kungine: naliwa na mwezi
Pia kwa nasibu, kuwa zimwi nazi,
Makumbi usumba: hufaa kwa mengi;
Hata na kifuu: cha kuteka maji
Kizio cha nazi: kombe la kunywea.
Sisangae, Bwana, bado sijakoma.

6. Na tui la nazi, bin Adam hufyonza
Akiisha kunguta: huweka machicha
Kisha pata mbata: huwapa vinyama
Vifae kunona: huleta faida.
Uwongo sisemi, sicheki dhihaka
Sifa yangu mnazi nani atasema?

7. Na matawi yangu, hutumiwa pia.
Bora fuadi uwe, ujue kusuka
Ukuti ununu: na kifumuwale,
Kuti la ukumba: kuti la upande,
Kuti la kiungo: toka upongoo,
Ufikiri sasa ukaone mambo.

8. Shambani tembea, kaone majengo
Yao walimaji, vinyumba vidogo,
Pasi mti na nyasi: mimi peke MNAZI,
Nakifu kukinga: mvua jua kali,
Sokoni enenda: pakacha taona,
Ni chombo kizuri pakia matunda.

9. Hayo ni mafaa: na wangu uzuri,
Ukiri, naomba: tazama matawi,
Kwa pepo mwanana: vizuri hunepa
Kama binti Fundi: mikono hupunga.
Shingo langu refu: mikono ya mbinu,
Umbo langu lote mapambo matupu.

18

10. Hilo ni jawabu: la maswali yako
Nililojaribu: na kwa Mambo Leo
Nasihi niseme: uniwie radhi.
Ewe! Bwana Khamisi: idadi ya miti
Uliyohasibu: imepungukiwa
Mimi peke Mnazi naweza kushinda.

Shairi hili (isipokuwa kwa mistari 6 hivi yenye mizani 13)
linao urari wa mizani 12, iliyogawanyika nusu kwa nusu,
mizani 6 kila kipande. Ingawa tunakuta hapa na pale upo
upatanifu wa vina vya mwisho katika mistari miwili, lakini
upatanifu huo umetokea kwa nasibu tu. Katika shairi hili
mtunzi, badala ya kuongea yeye mwenyewe na Bwana
Khamisi, ameupa mnazi nafsi ya utu; na mnazi umeongea ana
kwa ana na Bwana Khamisi kueleza sifa zake. Mbinu hii
imelifanya jibu la mtunzi liwe na mvuto wa pekee - mvuto am-
bao pengine usingepatikana iwapo Bwana Pacha engeongea
ana kwa ana na Bwana Khamis juu ya sifa za mnazi.

Bwana Pacha si mtunzi pekee wa kiwango cha juu aliyediriki
kutunga ushairi guni. Shaaban Robert, yule "Simba wa
Uswahilini, alitunga ushairi huu pia. Ubeti wa kwanza wa
shairi lake "Muombwa" umekaa hivi

Muombwa ni wewe Mungu
Na jamii ya umati,
Miili itie nguvu
Na heri katika nchi,
Astawi kila mtu
Zitakate na nafsi.

Na katika shairi lake "Nimeambiwa" ubeti wa kwanza una
mpangilio huu:

Habari nimeambiwa Tanganyika yastawi,
Habari hii ni njema nikikumbuka matendo,
Na kazi walizofanya watu wenu wa zamani,
Kwa bidii kubwa sana mpaka hili likawa.
Matendo ya watu wetu, wanawake na waume,
Katika kila taifa yanawanyanyua watu,
Na nchi ikawa nzuri au kuwatupa chini.

19

Mfano mwingine wa shairi guni lililotungwa na Shaaban
Robert ni "Mtu Mwema", na ubeti wake wa kwanza uko hivi:

Mtu ambaye ni mwema japokuwa hana dini,
Awe kafiri mkubwa wa sala na wa ibada,
Lakini huonekana hadhuru mtu mwingine,
Na mwanawe hamdhuru au mwana wa mwenziwe,
Mwana ambaye si wake kinuni hatamponda,
Kisha akaoe mke kusudi azae mwana!
Wema ni kama johari tena ni nuru ya mtu.

Katika mifano hii ya beti za mashairi ya Shaaban Robert,
tunaona kuwa ijapo yanafuata urari wa mizani lakini
hayakufuata utaratibu wa vina. Na mifano hii inaelekea
kutangua, au kurekebisha, ufafanuzi wa Shaaban Robert juu
ya ushairi. Katika hotuba yake ya mwaka 1958, anasema:

Ushairi ni sanaa ya vina inayopambanuliwa kama
nyimbo, mashairi, na tenzi... Kina ni mlingano wa
sauti za herufi...

Mifano hiyo hapo juu inatuonyesha kuwa mashairi haya si
sanaa ya vina hata kidogo. Tukifuata ufafanuzi wa Amri Abedi,
ni mashairi guni. Tukifuata ufafanuzi wa Kandoro, labda si
guni kwa sababu watunzi wameyatunga hivyo kwa
kukusudia, si kwa kushindwa.

Amri Abedi, alipokuwa akiandika kitabu chake Sheria za
Kutunga Mashairi na Diwani ya Amri, alitambua kuwa mashairi
guni yapo ila hakuyashughulikia kwa kuwa "hayatiliwi nguvu
na sio maarufu". Ndiyo maana Juliasi Kaizari kilipochapishwa
na Lyndon Harries akarukia na kusema kuwa mtindo wa taf-
siri umefuata ushairi guniwa Kizungu, Amri Abedi
alikanusha dai hilo kwa kusema:

Ajabu ni kwamba hivi karibuni tu Rev. Lyndon
Harries alitamani sana ionekane kuwa baadhi ya
mashairi ya Kiswahili yana asili ya mashairi ya
Kiingereza. Mheshimiwa Baba wa Taifa alipotoa
tafsiri ya Julius Caesar kwa ushairi wa guni au usio
na vina Lyndon Harries alirukia kusema kuwa
washairi wa Kiswahili hawana desturi ya kuandika

20

mashairi yasiyo na vina, na kwa kuwa Waingereza
ndiyo wenye desturi hiyo basi kazi ya Baba wa Taifa
asili yake ni ya Kiingereza! Ilimradi hawaoni raha
kuona cho chote kina asili ya Kiafrika! Kikifanana
na Kiarabu basi Kiarabu ndiyo asili, kikifanana na
Kiingereza basi Kiingereza ndiyo asili! Je, Kiswahili
chenyewe hakiwezi kuwa na fani ambazo asili yao ni
Kiswahili chenyewe?

Kweli, bila kusahau kuwa tamthiliya inayozungumziwa ina
asili ya Kiingereza, Kiswahili kinazo fani ambazo asili yake ni
Kiswahili chenyewe, na miongoni mwa hizo ni ushairi guni na
ushairi wa mtiririko. Maneno hayo ya Sheikh yangefaa kuam-
biwa wanajadi wanaoshikilia kuwa mtindo huu ni wa
Kizungu.

Kutokana na hayo tuliyokwisha sema, tunaona kuwa
ushairi guni ni mtindo katika ushairi-andishi wa Kiswahili
ambao umekwisha kukubalika. Ingawa mwanzoni ulihusishwa
na 'dosari', lakini katika miaka ya 1960 ulikuwa unatam-
buliwa kuwa ni mtindo wenye hadhi kamili katika ushairi wa
Kiswahili. Ndiyo maana Shaaban Robert hakuhofu "kujivun-
jia hishima" kwa kuandika ushairi guni, kama ambavyo
Bwana Pacha, katika mwaka 1928, hakuingiwa hata na fikira
ya kujivunjia hishima" mbele ya malenga wenzake. Sasa basi
ushairi huu "mpya" tunaweza kuuita "ushairi guni"?

Jibu la swali hili litategemea mtazamo wa mtu kuhusu
ushairi guni. Iwapo tutashikilia rai ya Farouk Topan, kwamba
"uguni" ni tokeo la kushindwa kufuata kanuni za vina na
urari wa mizani, tutasema kuwa mtindo huu siyo guni. Iwapo
tutashikilia dhana ya Amri Abedi kuwa mashairi guni ni yale
yasiyo na vina tu, bali yana mizani (kama mifano ya shairi la
Pacha na mashairi ya Shaaban Robert inavyoonyesha), vile
vile tutahitimisha kuwa mashairi haya siyo guni kwa kuwa
siyo lazima yawe na urari wa mizani. Lakini iwapo tuna
dhana ya "uguni" ambayo ni pana zaidi, ishikiliayo kuwa guni
ni shairi lisilofuata kanuni za urari wa vina na mizani, basi
mashairi haya tutayaita mashairi guni. Kwa mujibu wa
mtazamo huu ushairi wa kitamthiliya tuukutao kwenye kitabu
cha F. Nkwera Johari Ndogo na J.K. Nyerere (Mfasiri) Juliasi
Kaizari ni ushairi guni; na pia ushairi wa kimasimulizi wa E.
Hussein katika kitabu chake, Jogoo Kijijini, tutauita ushairi

21

guni uliochangamana na ushairi wenye kufuata kanuni za
vina na urari wa mizani.

Yamkini sasa tumefika mahali ambapo inabidi tuliingilie
suala lenyewe la msingi: Ushairi ni nini?

USHAIRI NI NINI?

Hadi hapa tumekwishakuona kuwa ushairi wa Kiswahili si
sanaa ya vina kama Shaaban Robert alivyotuambia; na wala
vina na urari wa mizani siyo roho au uti wa mgongo wa
ushairi wa Kiswahili kama Abdilatif, Mayoka na wanajadi
wengine wanavyohubiri. Kwa hakika, mojawapo ya sababu ya
wanajadi kuamini kuwa shairi lazima liwe na umbo maalum,
na kuwa umbo hilo lazima litawaliwe na vina na urari wa
mizani, ni kuwa dhana yao ya ushairi imetawaliwa na utaratibu
wa kimaandishi. Hebu tulidadisi jambo hili zaidi.

Ni rahisi kuthibitisha kuwa umbo la shairi la vina na
mizani ni la kimaandishi, kwani karibu watu wote hapa kwetu
hulitambua shairi kama linavyoonekana kwenye ukurasa wa
karatasi (uwe ukurasa wa Uhuru, au wa Mzalendo au wa
diwani yoyote ya mashairi). Kwa mujibu wa mtazamo huu, in-
sha ni insha kwa vile huonekana imeandikwa kwa njia ya
mjazo; na shairi ni shairi kwa vile laonekana lina vina na
urari wa mizani. Hebu tuangalie andiko hili hapa chini:

Pasipo na mwanamke dunia ingekuwaje?
Mwanamme peke yake sijui angeishije! Maisha yetu
ya kwanza yangekosa msaada; ya kati yakawa giza
kwa furaha kuwa shida; na ya mwisho yangekuwa ni
ghali kwa pesa moja: ingekuwa si dunia kwa
uchache wa faraja.

Andiko hili lililoandikwa kwa njia ya mjazo, bila shaka
laonekana kuwa nathari. Lakini andiko hilo hilo tukigeuza
umbo lake, "dhana" ya watu wengi juu ya hulka yake itageuka
pia:

Pasipo na mwanamke dunia ingekuwaje?
Mwanamme peke yake sijui angeishije!
Maisha yetu ya kwanza yangekosa msaada;
Ya kati yakawa giza kwa furaha kuwa shida;

22

Na ya mwisho yangekuwa ni ghali kwa pesa moja:
Ingekuwa si dunia kwa uchache wa faraja.

Umbo hilo haliwakanganyi watu wengi: waliangaliapo mara
moja hurukia kusema kuwa ni shairi, na wakiulizwa kwa
nini hujibu kuwa andiko lina vina, urari wa mizani, n.k.
Tuchukue andiko jingine lifuatalo:

Wakadha namshukuru Mungu
Kwa ajili ya sahibu yangu
Mtunzi na kungwi wa mizungu
Mathias Mnyampala
Mfadhili na mwenye jamala
Mashuhuri kwa mashairi ya muwala
Na uandishi wa makala
Ambaye ameniomba niandike hii dibaji
Asaa iwafariji wasomaji
Ambao sanaa hii wanaitaraji
Niwabainishie yaliyo muhimu
Kuhusu Kiswahili na utungaji
Na kubatilisha riwaya za mafukala.

Katika andiko hili tunaona upatanifu wa aina fulani wa vina
vya 'ngu', 'la', na 'ji', ni 'mu' tu ambayo haina kina chenziye. Na si
ajabu wapo watu ambao wanaweza kuliita andiko hili ubeti
wa shairi lenye dosari au guni, kwa sababu wameona
upatanifu fulani katika umbo lake. Kumbe andiko lenyewe
katika uasili wake lilikuwa katika umbo la mjazo kama
ifuatavyo:

Wakadha namshukuru Mungu kwa ajili ya sahibu
yangu, mtunzi na kungwi wa mizungu, Mathias
Mnyampala, mfadhili na mwenye jamala,
mashuhuri kwa mashairi ya muwala na uandishi wa
makala, ambaye aliniomba niandike hii dibaji asaa
iwafariji wasomaji ambao sanaa hii wanaitaraji,
niwabainishie yaliyo muhimu kuhusu Kiswahili na
utungaji, na kubatilisha riwaya za mafukala.

Kutokana na hayo yaliyokwishasemwa, tunaona kuwa
"ana ya ushairi" ya wanajadi imefinywa kwenye "umbo
maalum lenye utaratibu wa vina na urari wa mizani", ambayo

23

kwa kweli ni dhana ya kimaandishi. Na nathari kwao ni an-
diko lolote ambalo halina utaratibu huo. Wanayaangalia
matumizi ya lugha katika tabaka mbili zisizoingiliana:
matumizi ya kishairi na yale ya kinathari. Mtazamo huu
kuhusu lugha umepotoka sana, na hapo baadaye tutaonyesha
upotofu wake. Kwa sasa inafaa tulikabili suala la ushairi ni
nini.

Iwapo "umbo" lionekanalo kwenye karatasi haliwezi
kutiwa maanami katika ufafanuzi wowote thabiti wa
ushairi, basi ushairi ni nini? J.A. Ramadhani, katika makala
yake juu ya ushairi, ameeleza kwa urefu na kwa undani
maana na sifa za ushairi. Mambo mengi muhimu ameyataja.
Anatuambia kwamba:

(1) Ushairi huanza na hisi au mchomo unaosababishwa na
mazingira;

(2) Hisi hizo huwasilishwa kwa msomaji kwa njia ya lugha
teule ya kitamathali;

(3) Hisi hizo lazima ziambatane na mawazo na mtazamo
wa fikira;

(4) Hali ya kishairi inahusiana kidogo na hali ya kindoto
au tabia ya kuona yasiyoonekana na kuwania
yasiyowezekana;

(5) Ushairi umefungamana na ubuni, na kwa hiyo hauwezi
kuwekewa sheria zisizobadilika, na kwamba kuogopa
kubuni kunadumaza maendeleo ya ushairi wa
Kiswahili;

(6) Uwezo wa kubuni wa mshairi umetoka kwa Mungu am-
baye ndiye mfalme wa sanaa zote.

(7) Shairi ni muungano wa fani na yaliyomo (maudhui).

Kimsingi, ufafanuzi huo wa ushairi hautofautiani sana na
ufafanuzi alioutoa Kezilahabi. Anatuambia kwamba:

Ushairi ni tukio, hali au wazo ambalo limeonyeshwa
kwetu kutokana na upangaji mzuri wa maneno
fasaha yenye mizani kwa ufupi ili kuonyesha ukweli
fulani wa maisha.

Fafanuzi hizi mbili zinarekebisha ile fikira ya wanajadi
kwamba ushairi lazima uwe na urari wa mizani na vina. Hata
hivyo, fafanuzi hizi zina upungufu wake.

Upungufu wa maelezo ya Ramadhan umo hasa katika
imani yake kuwa uwezo wa kishairi unatoka kwa Mungu.
Hapa sipo mahali pa kujadili imani ya kidini ya Ramadhan

24

juu ya uwezo wa kishairi; suala hili ni kubwa na pengine
linahitaji makala ya pekee. Inatosha tu tukisema kuwa ni
kawaida ya falsafa za kidhanifu kumuweka Mungu kuwa
chimbuko la mema aliyo nayo mtu; na kumuweka shetani
kuwa chimbuko la mabaya yote. Upungufu wa kauli ya
Kezilahabi hasa umo katika fungu la maneno "ukweli fulani
wa maisha". Je, ni kweli kuwa ushairi lazima ueleze ukweli
fulani wa maisha, na siyo uongo? Hali halisi inatueleza kuwa
wapo washairi wasemao ukweli fulani kuhusu maisha, na
wapo wengine wasemao uwongo, na pia mshairi mmoja
anaweza kusema ukweli katika shairi moja na uwongo katika
shairi jingine. Fikra hii ni potofa kama ile isemayo kuwa
mshairi ni chemchemu ya hekima.

Jambo ambalo halikutiwa maanani katika fafanuzi hizo
linahusu dhima ya fasihi na ushairi kama vyombo vya
kuburudisha na kustarehesha watu. Ushairi hauelezi mawazo
tu kama kemia au fizikia. Ushairi lazima uguse hisi, lazima
umsisimue yule anayeusema, kuusoma au kuuimba na yule
ausikilizae. Shairi lisilogusa hisi ni kavu na butu, na hata
kama limesarifiwa katika vina na urari wa mizani, shairi hilo
litaishia katika kuhibiri tu. Na fasihi ikisha hubiri mahubiri
makavumakavu kama kasisi mimbarini, bila mvuto wowote
wa kifasihi, itakuwa imeshindwa kugusa pale ambapo
inapaswa kugusa - hisi za watu. Kwa hiyo basi ufafanuzi
thabiti wa ushairi lazima uzingatie uwezo wake wa kugusa hisi
za watu.

Kutokana na hayo tuliyokwisha sema, tunaweza kutoa
ufafanuzi wa ushairi ambao unazingatia yale yaliyokwisha
semwa na hao hapo jua, pamoja na dhima ya ushairi ya
kugusa moso au hisi. Nao ni huu: Ushairi ni sanaa inayopam-
banuliwa kwa mpangilio maalum wa maneno fasaha na yenye
muwala, kwa lugha ya mkato, picha au sitiari au ishara, katika
usemi, maandishi, au mahadhi ya wimbo, ili kueleza wazo au
mawazo, kufunza au kueleza tukio au hisi fulani, kuhusu maisha au
mazingira ya binadamu, kwa njia inayogusa moyo. Hapa lazima
tuseme kuwa, ingawa ushairi wa aina yoyote unaweza
kuimbwa, lakini siyo kila kiimbwacho kitaitwa ushairi.
Ushairi ni sanaa ya lugha, na usanaa wake uko katika
"mpangilio maalum wa maneno fasaha yenye muwala, kwa
lugha ya mkato... kwa njia ya kugusa moyo", siyo katika uim-
baji, unaweza kuuongezea (au hata kuupunguzia!) mguso.

25

Kwa mujibu wa maelezo haya, uimbaji wa hesabu au aya
kutoka kwenye kitabu cha siasa si ushairi.

Ufafanuzi huo wa ushairi unazingatia halka ya ushairi
usiofuata urari wa vina na mizani na ule unaofuata urari huo;
ule ulio katika fasihi simulizi na ule ulio katika fasihi andishi.
Jambo moja linalojitokeza ni kuwa ushairi ni lugha katika
hali ya matumizi maalum; na matumizi maalum haya ni
matumizi ya kisanaa ya vipengele vya lugha. Hapa chini
tutajadili kwa ufupi baadhi ya vipengele muhimu
vinavyoupambanua ushairi.

VIPENGELE VYA USHAIRI

Washairi wa jadi wanadai kuwa "vina na mizani ndio uti wa
mgongo wa ushairi." Dai hili ni batili kifasihi, kwani linageuza
kipengele kimoja kidogo cha kisanaa kuwa ndicho msingi wa
sanaa yenyewe.

John Ramadhani amezieleza sifa za ushairi kwa urefu na
vizuri zaidi. Yeye ametaja mambo yafuatayo yaliyo mahimu:

1) Katika ushairi vitu hupewa nafsi na utu;

2) Picha ni sifa muhimu ya ushairi;

3) Ushairi huweza kuwa na mpangilio wa maneno usio wa
kawaida;

4) Ushairi una ridhimu, mlingano wa sauti na mapigo;

5) Shairi ni lazima lionyeshe sifa ya kiumbaji, lisiwe ni
nakala ya shairi jingine.

Yote haya ni sawa, ila sisi tutajaribu kuyafafanua zaidi
na kuongezea sifa zingine ambazo hazikutajwa. Suala hili
tutalijadili kwa kufuata vichwa hivi:

1) Mpangilio wa maneno

2) Picha

3) Tamathali za usemi

4) Takriri na ridhimu

5) Hisia za kishairi

6) Fani na maudhui

Mpangilio wa maneno

Watu wengi wameichukulia kuwa kweli isiyopingika kuwa
mpangilio wa maneno (mfuatano wa vipashio vya sentensi)
katika ushairi ni tofauti na ule ulio katika nathari. Mpangilio
wa maneno hufuata kanuni za miundo inayowezekana katika

26

lugha fulani. Tukichukua Kiswahili, kwa mfano, sentensi
iliyozoewa sana ni ile yenye muundo huu:

Kiima - Kitenzi - changizo...
Nomino - kimilikishi - kitenzi - kielezi...

Katika Kiswahili tunaweza kusema:
Baba hujua kulima
Mama hujua kusaga
Mimi sijui chochote
Baba yangu anajua kulima kwa plau

Hii ni miundo ya kawaida ambayo imezoewa sana na
wasemaji wa Kiswahili. Lakini, mzungumzaji anaweza
kuipangua miundo hiyo, na kutumia miundo isiyo ya kawaida
sana, kwa madhumuni ya kuleta msisitizo wa jambo fulani:

Kulima baba hujua
Kusaga mama hujua
Chochote mimi sijui...

Jambo la kusisitiza hapa ni kuwa mtu yeyote, mradi awe ni
mzungumzaji wa lugha fulani, anaweza kutunga muundo wa
kawaida au usio wa kawaida sana (pengine bila yeye kujua).
Mzungumza lugha anao uhuru wa kutamba katika uwanja wa
lugha yake ili aweze kueleza hisia na mawazo yake. Jinsi
atakavyopanga maneno katika sentensi itategemea ujuzi na
ustadi na uzoefu wake katika jambo hili. Je, mshairi
anautumiaje uhuru huu wa kutunga miundo iliyo ya kawaida
sana, na ile isiyo ya kawaida sana?

Jambo la kusisitiza hapa ni kuwa mshairi si mtu wa pekee
katika ujuzi wa lugha aitumiayo kutungia mashairi yake.
Jambo tuwezalo kulisema pasipo wasiwasi wowote kuhusu
tofauti baina ya mshairi na mtu wa kawaida ni hili: mshairi
anao uzoefu katika kutunga mashairi, lakini mtu wa kawaida
hana uzoefu huo. Uzoefu huu katika sanaa hii humwezesha
mshairi kuitumia miundo ya lugha hiyo kutimilizia malengo
yake ya kishairi. Uhuru wa mshairi wa kuchagua muundo
fulani na kuacha muundo mwingine, kupanga vipengele fulani
kwa njia fulani na kuacha kuvipanga kwa njia nyingine, ni
uhuru unaotawaliwa na kanuni za sanaa yake, uwezo wake wa
kuvipanga vipengele hivyo ili vilete athari iliyokusudiwa
hutegemea uzoefu wake, ubingwa wake, na hali aliyo nayo
wakati wa kutunga shairi lake.

Katika ushairi wa Kiswahili, mbinu ya upangaji wa
vipengele vya sentensi kwa njia isiyo ya kawaida hutumika

27

sana. Utakuta washairi wanasema: mzuri msichana, wangu mke,
n.k. badala ya msichana mzuri, mke wangu. Miundo mingine ni
kama ile tuliyoitoa mfano hapo juu (kulima baba ajua n.k.).
Ipo miundo mingine isiyotumika sana katika mazungumzo ya
kawaida inayotumiwa na washairi. Mpangilio huu usio wa
kawaida huvuta udadisi kuliko ligha ya kawaida, na
hutumika katika kusisitiza vipengele fulani vya hisi au wazo
la mshairi.

Lakini shairi siyo lazima liwe na mpangilio wa maneno
usio wa kawaida ili lipendeze. Shairi linaweza kuwa na
mpangilio wa kawaida tu, na athari ya mguso ikaletwa na
vipengele vingine kama vile picha, takriri, n.k. Kwa hiyo,
ingawa mpangilio tulioujadili unaweza kuwa alama
mojawapo ya ushairi, lakini si lazima kila shairi lithibiti
mpangilio huo.

Picha

Picha ni matumizi ya lugha yanayopambanuliwa na utenzi
mzuri wa maneno, uangalifu na udhahiri wa maelezo wenye
kuhusisha na kujumuisha dhana mbali mbali tofauti ndani ya
dhana moja ili kuleta taswira na athari maalum katika
mawazo ya msomaji (au msikilizaji). Kezilahabi ameeleza
kuwa athari hiyo aipatayo msomaji au msikilizaji wa ushairi
inaweza kuwa ni ya aina ya vionjo vyenye kuhusiana na
milango ya fahamu ya kusikia, kuona, kunusa na kugusa. Kwa
hiyo, kwa kutumia picha, mwandishi anaweza kumfanya
msomaji wake asisimke, aogope, afurahike, avutike,
akirihishwe, alie, anyamae au aghadhabike kwa kuathiriwa na
picha zilizoteuliwa na kusanifiwa kwa ufundi. Ugumu wa
kutunga mashairi ya mtiririko uko katika utenzi na upangaji
wa picha na tamathali za usemi zenye kuoana na maudhui
yaliyokusudiwa zisizotengua ridhimu ya shairi na zisizofanya
lugha ya shairi ipoteze uasili wake. Wakati huo huo, shairi hili
liwe na uwezo wa kindanindani wa kuvutia na kudumisha
hamu ya msomaji au msikilizaji hadi mwisho. Katika ushairi
wa fasihi-simulizi, hamu ya hadhira hudumishwa na uteuzi wa
maneno, muziki (kama ala za muziki zinatumika), mazingira
au sherehe inayoambatana na tungo hiyo, ushirikishaji wa
hadhira kwa kutumia kibwagizo, makofi na vipengele vingine,
na umuhimu wa kijamii au kihistoria wa yale yanayoelezwa.

28

Katika ushairi-andishi wenye vina na mizani, hamu ya
msomaji zaidi hudumishwa na ulinganifu wake wa ridhimu na
sauti unaotokana na vina na urari wa mizani. Mapigo ya
shairi la aina hiyo hufuata mgawanyo wake katika vipande
vyenye mizani sawa na shairi husomeka upesi upesi bila
kuitumikisha sana akili ya msomaji. Kifani, vina na urari wa
mizani katika ushairi-andishi hufanyakazi ya ala za muziki
katika ushairi-simulizi.

Ushairi wa mtiririko ni wa kiwango cha juu zaidi kwa
sababu unakataa kupata uhai wake kutokana na mbwembwe
za kijuujuu, mambo ya nje ambayo ni nyongeza muhimu juu
ya ushairi, lakini si lazima yawe sehemu ya ushairi: vina na
urari wa mizani. Ushairi huo unapata uhai wake na utamu
wake kutokana na mfumo wake wa ndani ambao ni
fungamano la matumizi mahususi ya lugha nzito, hisia nzito
na maudhui ya kishairi. Mashairi haya yanamlazimisha
msomaji atumie akili zaidi, ajihusishe zaidi kijaziba katika
hisia za mtunzi, na atafakari zaidi, badala ya kumkokota
kikuku kwa utamu wa kijuujuu wa muziki wa vina na urari wa
mizani. Mtiririko ni mashairi yaliyokusudiwa yasomwe na
watu wazima, mengi hayafai kusomwa na watoto wa shule za
msingi kwa sababu uwezo wao wa kuichambua fasihi bado ni
mdogo. Hivyo hapana shaka kuwa kwa miaka mingi ijayo
mashairi yenye vina na mizani yataendelea kupendwa zaidi na
watoto wadogo, mradi lugha yake isiwe ngumu sana. Kwa ajili
ya adhira hiyo, mashairi ya aina hiyo ni lazima na bora yaen-
delee kutungwa. Bali kwa ajili ya watu wazima waliofikia
kiwango fulani cha ufahamu wa fasihi, mashairi ya aina hiyo
si lazima, ingawa si mwiko kuyatunga. Kila mshairi apewe
uhuru wa kutumia fani inayofungamana vizuri zaidi na
maudhui yake, uwezo wake, na pia hadhira aliyokusudia.

Ingawa matumizi ya lugha huweza kuzindua hisi na
maono fulani katika akili ya msomaji juu ya kile
kinachozungumziwa, lakini ni muhimu kukumbuka kuwa
uhusiano huo unaozinduliwa kati ya picha ya mawazoni na
kitu halisi kinachozungumziwa (kinachochorwa) ni wa
kinadharia, si wa kimaumbile au wa moja kwa moja. Hakuna
uhusiano wa moja kwa moja kati ya maana au umbile la kitu
na uwakilishaji wa kitu hicho katika lugha - katika neno
mofimu na fonimu. Kifasihi uhusiano tuupatao tunapotumia
picha ni ule unaoumbwa na akili ya msomaji mwenyewe

29

inapozinduliwa na ustadi wa mshairi wa matumizi ya lugha
na kunga nyingine za ushairi. Usanifu wa mashairi humfanya
msomaji wake awe msanifu vile vile; mshairi hudokeza,
msomaji hukamilisha; mshairi huumba, msomaji
humalizia na kuhusisha kile kilichoumbwa na hali halisi
anayoijua. Kwa hiyo msomaji wa mashairi si mpokeaji tu wa
sanaa hiyo bali ni mpokeaji msanii vile vile.

Hebu tuutazame mfano ufuatao unaotoka katika shairi la
Shaaban Robert, "Mtu na Malaika".

Mtu Na Malaika

Neno lenye mzunguko, halipatikani mwisho,
Wa huku hafiki huko, wala halina malisho.
Halishibishi huchosha, njiaye ina uchovu,
Na tabu isiyokwisha, wala hupati utuvu.
Heri ya mtu ni kwenda, njia iliyonyooka,
Na milima akapanda, apendako akafika.
Mabondeni akashuka, mwituni akatumbua,
Na mitoni akavuka, hata alikonuia.
Na mzunguko wa dira, mwisho wake ni dirani,
Hupati kupanda bara, na hushuki baharini.
Tazama mashaka gani, njia ya dira si njia.

Katika dondoo hii tunapewa picha tatu mahsusi. Picha ya
kwanza ni neno linalozunguka... Mshairi anatuambia kuwa neno
ambalo halifuati njia iliyonyooka 'neno lenye mzunguko"
halifikii mwisho wake na halileti mradi uliokusudiwa "halina
malisho". Hapa neno limefanywa kuwa kitu chenye uwezo wa
kutembea, kuzunguka. Athari ya neno hilo kwa anayehusika ni
kwamba halileti shibe wala utulivu, linachosha: "Halishibishi
huchosha". Hapa tunapewa picha ya shibe, neno linapewa
uwezo wa chakula - kitu yakini kinachoshikika na
kinacholiwa. Bali mtu hatosheki na "chakula hicho" hatatui
matatizo yake iwapo njia anayotumia ni ya mzunguko, ya
kulegalega, ya ugeugeu na woga.

Picha ya pili tunayopewa ni ya mtu aendaye safari ngumu
kwa ujasiri na moyo na dhati, akipanda milima na kushuka
mabonde, akipenya misitu na kuvuka mito, hadi kufika kule
anakokwenda. Huyu ni mtu asiyeogopa matatizo,
anayeshikilia njia ngumu lakini nyoofu, alimradi anajua kuwa
itamfikisha kwenye lengo lake. Ni mtu anayepambana na

30

matatizo badala ya kuyakimbia. Mtu wa aina hii ndiye hupata
mafanikio. "Heri ya mtu ni kwenda, njia iliyonyooka".

Picha ya tatu tunayopewa ni dira. Dira ni chombo
kitumiwacho na mabaharia na wasafiri wengine kusahihisha
majira yao ili wasipotee njia. Dira ni chombo cha mviringo na
mshale wake aghalabu huzungukia pale pale ulipo, katu
hautoki nje ya dira. Picha hii inasisitiza wazo la mwandishi
kuwa njia yenye kuzunguka haiwezi kumfikisha mtu kwenye
lengo lake. Mshale wa dira huzunguka daima lakini haufiki
kokote.

Picha hizi tatu kwa pamoja zinafaulu kutupa ujumbe wa
mwandishi kuhusu maisha na namna ya kuyakabili:
tuyakabili kwa juhudi na ujasiri na nia. Tuamue jambo na
tulifanye bila kutetereka. Tusiogope vikwazo wala matatizo.
Maisha ni mapambano.

Kwa kutumia picha hizi tatu, mwandishi kafaulu
kufikisha kwetu ujumbe wake wa kishairi. Maudhui yake ni ya
kishairi, yanapatikana kwa kuzichambua na kuzifafanua
picha alizozitumia. (Shairi hili lingeweza vile vile kufasiriwa
kidini kama alivyofanya J. Ramadhani katika makala yake
"Ustadi wa Shaaban Robert Mshairi" Mulika No. 7, uk. 46-48)

Mpangilio wa lugha

Katika dondoo tulilolichunguza picha imejitokeza kwa
njia ya sitiari (kitu kimoja kuwa badala ya kitu kingine kilicho
tofauti: k.m. "msitu" badala ya "matatizo", "dira" badala ya
"tabia ya kukwepa matatizo" n.k.) na mpangilio wa lugha na
mawazo. Dhana tatu zinazotofautiana - neno linalozunguka
mtu anayesafiri kupitia msituni na baharini, n.k. na dira
inayozungukia mahali pale pale ilipo zinaleta wazo moja
mahsusi. Zote zimechangamana ili kujenga dhana moja.
Umoja wa wazo linalozungumziwa unaimarishwa pia na
mfungamano wa ubeti mzima - pana mfululizo wa fikra na hisi
tangu mstari wa kwanza hadi wa mwisho, kifungu kizima ni
ubeti mmoja, hakuna mgawanyo wa beti za mistari miwili
miwili au minne minne. Wazo linafululiza bila kusita au
kukatishwa hadi mwisho kama vile ambavyo maudhui ya
shairi lenyewe yanavyotuhimiza kufululiza katika njia moja
bila kutetereka hadi mwisho. Muundo wa shairi umeoana na
maudhui yake.

31

Mpangilio wa lugha - herufi, silabi, mofimu hadi maneno
na sentensi ni sharti uoane na maudhui. Washairi hutumia
kunga mbali mbali za kisauti na kimpangilio ili kuleta hisia
fulani. Baadhi ya kunga hizo ni onomatopea, mizani, vina,
asonansi (mlingano wa sauti za irabu), konsonansi (mlingano
wa sauti za konsonanti) takriri-konsonanti (marudio ya kon-
sonanti) takriri-vina, n.k. Vipengele vyote hivi, isipokuwa
onomatopea, ni aina ya takriri na tutavijadili chini ya mada
ya takriri.

Onomatopea

Onomatopea ni mwigo wa sauti. Hii ni kunga inayotumiwa na
washairi ili kutoa picha au dhana ya kile kinachowakilishwa
au kupambanuliwa na sauti hizo. Kwa mfano tukisema:
"Maji yalimwagika mwa" neno mwa ni onomatopea,
linawakilisha sauti au kishindo cha maji yanayomwagika.
Baadhi ya onomatopea ambazo zimekwisha kuwa sehemu ya
msamiati wa kawaida wa Kiswahili ni: pikipiki, bombom,
mbwa, yowe, ngurumo, bunduki, gumia, kata, n.k.

Katika shairi lake la "Cheka kwa Furaha" Shaaban
Robert ametumia onomatopea ili kuleta ile dhana ya kucheka:

Dhiki ni kama mzaha, asiyecheka ni nani?
Haya cheka ha! ha! ha! ndiyo ada duniani.
Basi cheka kwa! kwa! kwa! kwa! usafike moyo wako
Pamoja na malaika, wema mbinguni waliko;

Maneno yaliyoandikwa kwa italiki ni onomatopea, yanatoa
picha ya kusikika ya sauti ya mtu anayecheka. Huu ni
mpangilio maalum wa sauti ili kutoa picha ya kusikika ya
dhana inayozungumziwa.

TAMATHALI

Tamathali za usemi ni vifananisho au viwakilisho vya dhana
fulani kwa dhana nyingine tofauti au zinazofanana. Ni usemi
wenye kupanua, kupuuza au kubadilisha maana za dhahiri au
za kawaida za maneno ili kuleta maana maalumu ya kishairi
iliyokusudiwa na mtunzi. Tamathali nzuri hupanua,
huyakinisha na huipa uhai na uhalisi zaidi dhana

32

inayoelezwa, huburudisha na kuzindua akili ya msomaji au
msikilizaji wa shairi, na huacha athari ya kudumu katika hisi
na mawazo yake.

Tamathali zinazotumika zaidi katika ushairi ni tashbiha,
meonymy, uhaishaji (personification) (Tashihisi) synecdoche,
baalagha, kejeli na sitiari.

Tashbiha

Hi ni tamathali ya ufananisho au mlinganisho wa vitu viwili
au zaidi. Katika tashbiha, kama ilivyo katika sitiari, huwa
kuna vitu vitatu vinavyofananishwa ambavyo wataalamu
wameviita kizungumzwa, kifananishi na kiungo. Kifananishi
ndiyo usemi wenye kuzingatia maana-dhahnia, ni chombo
kinachobeba mlinganisho. Kizungumzwa ndicho kitu halisi am-
bacho kinazungumziwa na kifananishi kwa mafumbo. Kiungo
ni zile sifa ambazo zinapatikana katika kizungumziwa na
kifananishi na hivyo kuhusisha vitu hivyo viwili. Katika tash-
biha, kizungumzwa na kifananishi huhusishwa bila mafumbo
kwa uwazi, moja kwa moja, kwa kutumia maneno fulani ya
ulinganisho, km. "kama" "fanana na", "mithali ya" n.k.
Katika tashbiha hakuna maana dhahnia, bali kuna
ulinganishaji wa vitu viwili vilivyo bayana. Angalia mfano
ufutao:

Kweli ni sawa na radi inapotoa kauli...
Kweli kinywani ikiwa sawa na Mto wa Nili
Kweli kama msumeno hukereza sawa kweli.

Katika dondoo hilo maneno yaliyochapwa kwa italiki
yanaunganisha vitu viwili vinavyotofautiana na
kuvifananisha. Mstari wa kwanza "kweli" inalinganishwa na
radi, mstari wa pili inalinganishwa na "Mto Nili" na mstari
wa tatu inalinganishwa na "msumeno".

Tashihisi (uhaishaji)

Washairi mara nyingine huweza kukipa kitu kisichokuwa na
uhai sifa za kitu chenye uhai, hasa za binadamu. Matumizi ya
lugha kwa njia hiyo ndiyo huitwa uhaishaji au tashihisi.
Kisanaa maelezo ya kitashihisi huwa na upekee unaomwingia

33

msomaji akilini haraka, kwani si jambo la kawaida,
mathalan, kuona mti "ukimpungia mtu mkono" au nyumba
"ikimkodolea macho" mgeni. Tashihisi, basi, ni aina ya sitiari
na kisanaa kazi yake ni kama ile ya sitiari, japo kwa kiwango
cha kidhahnia zaidi.

Mfano wa matumizi ya tashihisi:

Kimya hakineni jambo, si kimya chawatazama...
Kimya chaja zua mambo, pasiwe mwenye kusema...
Kimya kipimeni sana, msione kutosema
Kimya hakichi kunena, kitakapo kusimama
Kimya chaja watukana kizuwe yaliyozama...

Katika dondoo hili, "kimya" (ambayo ni nomino-dhahnia)
kimepewa sifa za binadamu, kinaweza kunena, kutazama,
kuzua mambo, kusimama nakutukana.

Katika shairi lake la "Fedha", Shaaban Robert anaipa
fedha sifa za binadamu:

Fedha huita wazuri,
Wakaitika labeka,
Wakenda bila hiari,
Mahali wasikotaka.

Mfano mzuri wa matumizi ya tashihisi kishairi tunauona
katika shairi la Bwana Rajabu M. Kianda (Selukindo) liit-
walo "Jembe".

Jembe wangu nifariji, nami nikupe uzima,
Jembe wewe ndiye jaji, twakuenzi zote dhima,
Jembe wewe ni mpaji, wa baba na kina mama,
Jembe ndiwe mtawala, tangu enzi za wahenga.

Jembe wewe msifika, utuonee huruma,
Jembe shamba tukifyeka, njoo ufanye kulima,
Jembe njoo pasi shaka, ukija lete mtama,
Jembe ndiwe mtawala, tangu enzi za wahenga.

Jembe kwetu ukifika, tunapata usalama,
Jembe kote umeshika, ukweli tunausema,
Jembe yakija masika, nawe fika nyuma nyuma,
Jembe ndiwe mtawala, tangu enzi za wahenga.

34

Jembe jua likitoka, nawe usife mtima,
Jembe usije kuchoka, au kupatwa na homa,
Fanya bila kukongoka, fanya usirudi nyuma,
Jembe ndiwe mtawala, tangu enzi za wahenga.

Mola akupe hakika, usende kamwe mrama,
Nenda upate kufika, kama tunavyokutuma,
Sote huko tukifika, tutaishi kwa neema,
Jembe ndiwe mtawala, tangu enzi za wahenga.

Katika shairi hili "Jembe" limepewa sifa za binadamu: ni
mfariji, jaji, mpaji, mtawala, mkulima; linaweza kusafiri,
kubeba mtama, kufa mtima, na kupatwa na homa. Ingawa
tunajua wazi kuwa jembe ni kifaa tu kinachotengenezwa na
kutumiwa na binadamu, kuwa halina hata mojawapo ya sifa
hizo, lakini tunaposoma shairi tunaathirika na kushawishika
kuwa yasemwayo ni kweli na sana maana. Tunalikubali kwa
sababu tunaelewa kuwa tukisomacho ni kiwakilishi tu, ni
ishara ya dhana nyingine nzito na muhimu: Umuhimu wa
kilimo katika uchumi na uhai wetu, na katika historia wa
binadamu. Mtunzi katumia uwezo wake wa kisanaa kuumba
picha hii ya jembe, nasi wasomaji inatubidi tutumie uwezo
wetu wa kuumba na kutafsiri ishara ili tulielewe na
kulifurahia shairi hili. Matumizi ya tashihisi yanaliongezea
shairi hili uzito wa kimaana, na yanatushirikisha sisi
wasomaji katika ufumbuzi wa "kitendawili" chake. Hivyo
shairi hili linatuathiri sana kwa kuwa linatushirikisha akili
zetu katika kutafakari vipengele vyake na maana yake.

Karibu.
Jambo!
Habari yako?
Hujambo?
Sijambo!
Habari za safari?
Nimefurahi kukutana na wewe.
Jambo.
Hamjambo.
Hatujambo.
jambo.
karibu.
habari yako?
hujambo?
sijambo.
habari za safari?
nimefurahi kukutana na wewe.
habari?

